HEKO TRAFIKI 9299 MWANZA




Adeladius Makwega-MWANZA

Oktoba 30, 2023, Mwanakwetu alikuwa katikati ya Jiji la  Mwanza, akiwa hapo alipomaliza kile kilichompeleka alipanda Hiace inayokwenda Nyamhongolo, ya Nyashishi-Nyamhongolo.

Hiace hii ilianza safari na huku vijana hawa waliokuwa wakiendesha walionekana waungwana sana na hata walipopewa pesa yao ya nauli walichukua na kuirudisha chenji hiyo mara moja.

Mandhari ya ndani ya Hiace hii kulikuwa na viti vilivyojaa abiria vizuri na mizigo kila kona.

Wakiendelea na safari hiyo, mara Hiace hiyo ilisimama na dereva kushuka na kondakta, kila mmoja na mlango wake, muda huo huo na kurudi nyuma ya hiace hiyo.

Baada ya dakika kama mbili, alifika Trafiki na kutoa ilani ,

“Jamani nawaombeni mshuke hapa hapa niwatafutie usafiri mwingine, kwani hiace hiii haiwezekana tena kuendelea safari.”

Abiria wakaanza kushuka mmoja baada ya mwingine, mama mmoja mrefu mweusi akauliza ,

“Afande kwani hawa vijana wamefanya nini?”

Abiria mwingine akasema, hawa vijana tabu sana wanaendesha magari mabovu barabarani


.




Trafiki huyu ambaye kwa upande aliosimama Mwanakwetu aliona namba yake 9299,  huku akiwa amevalia sare zake nyeupe na mabegani, akiwa na mbawa kama mbili hivi .

“Mama ee hawa jamaa hawajakata bima yao kwa miezi sita, hili jambo halivumiliki kabisa na ndiyo maana ninawatafutia basi lingine muondoke.”

Mama huyu akasema sawa sawa, hongera sana, hiyo ni kazi nzuri na hongera kwa waliokupanga ufanye kazi katika  mkoa huu wa Mwanza.

Hayo yakiwa majira kama ya saa 7.10 kuelekea saa  7.20 mchana hivi , hapo kando kondakta wa Hiace hii akasema. kwa kunong'ona .

“ Hii ni gari ya trafiki mwenzake , wao wenyewe watamalizana ,  mimi kondakta sihusiki na kulipia hiyo bima.”

Mama huyu kando ya Mwanakwetu akasema hata kama mmiliki ni askari mwenzake , yeye ni nani akalipe bima hiyo au kama hawezi basi aliweke uani liwe linabeba ndugu zake tu.

Gafla ikafika daladala kubwa, abiria wote wakaingia ndani yake na kuchapa mwendo hadi kufika Nyamuhongolo na hapo Mwanakwetu kushuka na kupanda mabasi ya kwenda Malya Kwimba Mwanza.

Mwanakwetu siku ya leo anasema nini?

Kubwa ni kumpa heko Trafiki 9299 kwa kazi nzuri ya kusimamia Sheria za Usalama Barabarani, usimamizi thabiti wa sheria hii ni kulinda uhai wa bindamu.Inawezekana kwa vijana hawa wanondesha  hiace hiyo wakawa na makosa mengi kisa  anyemiliki ni afande. Mwanakwetu anatoa pongezi kwa  Mkuu wa Trafiki Mkoa wa Mwanza na pongezi hizo kwanza  ziitolewa na abiria wenzake Mwanakwetu na sasa Mwanakwetu anazipa sauti pongezi hizo kwa  umahiri wa Trafiki 9299 mkoani Mwanza.

Mwanakwetu Upo?

Heko Trafiki 9299 Mwanza.

Nakutakia siku Njema.

makwadeladius@gmail.com

0717649257

0/Post a Comment/Comments