ZAWADI YETU KWAKE



Lucas Masunzu- MAKOLE

SIKU hiyo nduguyetu aliamka mapema mno akashika njia moja kwa moja kuwahi hilo basi hapo stendi na ilipotimia saa 12 : 00 asubuhi dereva aling’oa gia na safari hiyo ya mbali ikaanza. Kwa bahati katika basi hilo hapakuwa na redio wala runinga hivyo utulivu ulitawala kwa baadhi ya saa, na kwa saa zingine kama ilivyo kawaida kwa wasafiri utani na soga za hapa na pale zilichipua. Safari hiyo ilikuwa ya pekee mno maana basi hilo lilikatiza mkoa kwa mkoa nao abiria walioketi upande wa madirisha walipata nafasi ya kufanya utalii wa ndani na kushuhudia maeneo mazuri ya nchi na yale mabaya.  

Ilikuwa ni robo tu ya safari mazungumzo ya hapa na pale yakaanza abiria mmoja aliyekuwa upande wa dirisha ambaye alichangamka akiwa si mgeni wa hiyo njia alisema nchi hii bado ina maeneo mengi sana ambayo yako wazi, bado kabisa yana rutuba hayajaguswa tangu enzi ya mkoloni. Inatakiwa watu waongezeke ili maeneo kama haya yapate watu ambao watayatumia kwa uzalishaji na uchumi wa taifa letu utazidi kupaa. Abiria mmoja aliyeonekana kuyajua mno mambo alidakia akasema “kwa takwimu za sensa ya watu na makazi idadi ya watu imeongezeka na sisi wanawake ndiyo tulio wengi”

Mjadala ulizidi kupamba moto abiria huyohuyo mwenye kuyajua mambo akasema ni kweli idadi ya watu imeongezeka lakini ingeongezeka maradufu ila hawa wasomi ndiyo wanaotuangusha. Ukifuatilia familia nyingi za wasomi wanazaa kwa woga mno, sasa tutaongezeka lini kama wenzetu wanazaa kwa woga?  Nduguyetu si mzungumzaji sana hasa kwa watu asiowajua, muda mwingi yeye alikuwa akisikiliza na kadri safari ilivyoendelea aliuchapa usingizi.

Masaa yakasonga basi likawa limefika sehemu yenye matuta ya karibu karibu, nduguyetu akamshwa na hayo matuta akauliza kwa jirani yake hapa ni wapi? Akajibiwa. Safari hiyo ndefu ikazidi kuendelea huku mazungumzo nayo yakipata nafasi ya kuendelea.

Kumbuka safari inaendelea muda huo ni adhuhuri wakafika eneo ambalo li wazi halina miti. Abiria mmoja ambaye alionekana kuvaa nadhifu na kudhaniwa kuwa ni mtumishi alisema sisi binadamu ni waharibifu sana. Swali la kwa nini liliulizwa abiria huyo nadhifu akasema miaka ya nyuma hapa kukuwa ni pori kubwa mno likipendeza lakini sasa hebu tazama hakuna miti ni visiki tu ndiyo vimebaki vimechuchumaa. Katakata mbao na katakata mkaa tukasahau ule usemi wa kata mti panda miti. Aliendelea kusema unajua bado kurudisha miti yetu inawezekana kabisa kama tukitambua kuwa ni jukumu la kila mmoja. Abiria huyo nadhifu aliendelea kutawala mazungumzo akasema mimi nimekaa ughaibuni kwa mlongo mmoja katika nchi niliyokaa ili mwanafunzi ahitimu ni lazima apande miti kumi na aihudumie na siku anahitimu masomo lazima aikabidhi ndiyo aende zake.



 

 

Kwa kuwa ni jukumu letu sote kwa mfano tukisema hapa kwetu kila mwanafunzi wa sekondari apande na kutunza miti mitano tu halafu una wanafunzi alfu moja tayari hapo ni miti alfu tano na hiyo ni shule moja tu zoezi linakuwa endelevu, baada ya miaka mitano kwa idadi ya wanafunzi nchi nzima tunakuwa tumestawisha miti mingapi? Hapo hatujarejesha miti yetu? Hivyo hivyo hata kwa familia zetu kila familia ikastawisha miti mitano tu kila mwaka ya matunda mitatu na ya kivuli miwili serikali ikabaki kututafutia mbegu bora tutakuwa tumepiga hatua mno. Nduguyetu alijikuta kajiingiza katika ulingo wa mjadala huo akasema “hili linawezekana kama jamii itaelimishwa, kupenda na kutunza mazingira itakuwa jadi yetu sote, vilevile ule utamaduni wa kata mti panda miti ukarejea, kila mtu ataona soni kukata miti kiholela na kutupa uchafu ovyo iwe katika barabara zetu au katika vyanzo vyetu vya maji.  Utunzaji wetu wa mazingira ndiyo itakuwa zawadi yetu kwa waziri mwenye dhamana mheshimiwa Dkt. Seleman Jafo.” Mazungumzo haya yalichukua nafasi kubwa mno vidole vikinyoshwa waziwazi pale ni pazuri na pale.

 

 

Safari ikaendelea na pole pole ndiyo mwendo. Saa za alasiri basi liliegesha stendi nduguyetu akashuka akawaacha wale abiria wengine wakiendelea na safari huku akiwaombea dua nao wafike

alama. Hapo hapo nduguyetu akashika boda boda na kuanza kukitafuta kijiji chao cha ujamaa. Akiwa kwenye bodaboda aliendelea kutafakari mazungumzo hayo huku akikumbuka kuwa ni jukumu letu sote. Ilipofika saa mbili kamili usiku nduguyetu aliwasili nyumbani kwao salama salimini akapokelewa na nduguze kwa furaha.

 

Nakutakia siku njema, Kwa heri.

theheroluke23@gmail.com

0762665595

2023





 

 

 

 

 

0/Post a Comment/Comments