Adeladius Makwega-MWANZA
Mwanakwetu alifika katika taasisi hiyo mapema kidogo , siku
hiyo ilikuwa ya mvua kubwa ikinyesha, hivyo mwili wake wote ulikuwa umelowa kwa
mvua hiyo. Kwa kuwa ulikuwa wito wa kisheria kutokwenda lilikuwa kosa moja
kubwa .
Alipofika hapo alipokelewa na ndugu mmoja ambaye sura yake
haikuwa ngeni machoni mwake. Mwanakwetu alikaa kimya lakini ndugu huyu alisema ‘Naona
kama ninakufahamu vile.’ Mwanakwetu nayeye akasema hata mimi naona sura
yako si ngeni.
Mwanakwetu alipewa huduma hiyo vizuri na ndugu hao , hapo walionekana
ni watumishi waungwana na alipomaliza alitoka zake kupanda basi kurudi nyumbani
kwake.
Safari ya kurudi nyumbani kwake ilikuwa ndefu kidogo, ambapo
Mwanakwetu alibahatika kupata kiti jirani na dirisha huku akipigwa na upepo wa
eneo hili.
Baada ya mwendo wa dakika 20 hivi, Mwanakwetu ikamjia picha
ya tukio moja la zamani.
“Baba wa Mwanakwetu anasafiri kwenda ng’ambo, mshahara wake
mzee huyu anawaachia watoto wake, kazi hiyo ya kupokea mshahara huo anapewa
dada/shangazi wa Mwanakwetu-anayeitwa Otilia Makwega , sasa Mwanakwetu
anatakiwa kwenda shuleni, Shangazi wa Mwanakwetu akasema ’Mwanangu ngoja mshahara wa baba
yako utoke, ili nikununulie vifaa vya shuleni na karo yako. Nakuomba ugoje mwisho
wa mwezi.’ Kweli Mwanakwetu anagonja mshahara huo . Mazungumzo haya ya
Mwanakwetu na shangazi yake yanafanyika huko Mbagala Kibonde Maji. Mwanakwetu
akala ugali wa usiku huo kwa shangazi yake huyu alafu na kuanza safari ya
kurudi Mbagala kwa Mangaya. Alifika Mbagala Mangaya majira ya saa 4. 30 usiku.
Alipofika hapo nyumbani alipokuwa akiishi yeye na wadogo zake, alipewa ujumbe
na rafiki yake anayefahamika kama Idi Mangaya kuwa ’Hapa wamefika jamaa wawili, wanashida
nawe . Wamesema watarudi tena’. Kweli Mwanakwetu na Idi Mangaya walikaa
hapo barazani kwa nusu saa na ndugu hao wawili walirudi alipo Mwanakwetu.
‘Kaka kwema? Tunakuomba chemba kidogo.’
Mwanakwetu alimuacha Idd Mangaya na kuongea na ndugu hao.
‘Kaka sisi tumekuja kwako, tuna shida, mimi unanifahamu nilisoma
Shule ya Mtakafifu Peter Morogoro(ST Peter Seminary) na huyu ni ndugu wa
shemeji yangu na huyo bwana mdogo ni mtoto kwa kaka yangu, anasoma shule ya sekondari
Makongo. Huko shuleni kumetokea vurugu, hivyo wamesimamishwa shule na kesho wanatakiwa
waende na wazazi wao, kwa namna tunavyomfahamu kaka, tukimwambia kesi hii
itakuwa mbaya na kijana huyu atapoteza masomo yake ,kaka hatoweza kulipa ada
tena, atarudi kijijini kwa mama yake, tunakuomba wewe ukamuwakilishe kaka yetu
, wewe tunakuamini kazi hii utaifanya vizuri.’
Mwanakwetu akasema, sasa baba yake akijua kuwa mimi ndiye
niliyeubeba ubaba bila idhini yake itakuwaje ? Na kama huko shuleni mambo yakiharibika
hilo litakuwaje? Jamaa hawa wakajibu kuwa hilo halina neno maana wameshirikisha
mama wa kijana huyu na babu yake na hayo ni maamuzi ya familia kumuokoa na balaa
kijana huyo.
Mwanakwetu akakubaliana kuwasaidia, hivyo jamaa kuondoka zao
na kulipokucha Mwanakwetu akavaa vizuri na kupanda basi na kijana huyu hadi sekondari
ya Makongo. Mkuu wa Shule hii wakati huo alikuwa nadhani Kanali Kipingu ,
wakati huo shule hii haikuwa maarufu sana maana jina lake la zamani lilikuwa ni
Lugalo
Jioni. Jina la Makongo ndilo linaanzaanza , wazazi walioitwa walifika
katika ofisi ya mkuu huyu wa shule na wanafunzi hao kutengwa katika makundi
mawili wenye wazazi wale ambao wazazi wao walichelewa kufika. Wale wenye wazazi
waliingia kwa Kanali Kipingu na kuelezwa shida ya kila mmoja alafu ikatolewa
adhabu hiyo na kila mzazi kukubaliana nayo akiwamo Mwanakwetu .
Kijana alipewa adhabu hiyo mbele ya umati wa wanafunzi wa
Makongo na baada ya tukio hilo Mwanakwetu alitoka hapo shuleni alitembea kwa
mguu hadi Mwenge na akapanda basi hadi Mbagala. Alipofika kwake alienda
nyumbani kwa hii familia na kutoa mrejesho kwa yule mseminari wa zamani na
kuwaeleza kama ilivyotokea na wao kushukuru sana.
Mwisho wa Mwezi ulifika Mwanakwetu alipewa ada na shangazi
yake na kuelekea shuleni huko Ndanda
Sekondari.”
Kumbuka msomaji wangu Mwanakwetu yupo
katika basi anarudi nyumbani kwake kutoka ofisi hii ya umma ambapo aliitikia
wito wa kisheria na hayo ameyakumbuka tu , maana kijana huyu sasa ni afisa mkubwa
ambaye amemuhudumia Mwanakwetu siku hii.
Mwanakwetu ndani ya basi akasema
moyoni,
“Mungu amemsaidia yule kijana alisoma, kumbe na mimi nimetia
mkono wangu na sasa ana mamlaka katika taasisi hiyo ya umma.”
Mwanakwetu akafika kwake salama
salimini huku akiikumbuka mno familia hiyo. Siku akienda Mbagala ataitafuta hii
familia.
Je siku ya leo Mwanakwetu anasema
nini?
Kijana huyu kwa sasa anaonekana ni
mkubwa sana kwa mwili na pia ni mkubwa kwa mamlaka kuliko Mwanakwetu. Kwa ukweli
wa Mungu Mwanakwetu ni kaka mkubwa wa ndugu huyu kama tukio hilo
linavyosimuliwa maana yeye alikuwa kidato cha tatu huku Mwanakwetu kidato cha
sita.
Kwa dunia namna ilivyo ndugu huyu
anaweza kumtendea mema mtu aliyemsaidia au anaweza hata kumfanyia mabaya kwa
sababu nyingi, mojawapo ni kusahau ule wema.Wako watu wanafanya ubaya si kwa kupenda
bali wanafanya ubaya huo kwa kushinikizwa kufanya hivyo.
Ndiyo maana Jaji Joseph Warioba
katika Ripoti yake ya Tume ya Rushwa ya mwaka 1996 alisema,
“Hakuna askari mbaya kama yule mwenye cheo cha juu, maana anaweza
kuamrisha chochote kikafanyika kwa amri yake tu. Tujitahidi kuepukana na hilo lazima
tuwe na askari kwa ngazi za juu wenye maadili mema na tabia njema.”
Huo ni mfano wa Jaji Warioba kwa
Jeshi la Polisi, Mwanakwetu anautumia
kulinganisha tu hilo hata kwa taasisi zingine za uchunguzi na hata mahakama ni vizuri kuwa na viongozi
waadilifu , wema, wenye huruma , wenye mioyo ya heshima , mioyo ya utu,wenye mioyo ya kumuogopa Mungu, ilikukwepa
kutoa maagizo ambayo yanakiuka hayo.
Mwanakwetu anatambua kuwa Jeshi la
Polisi Tanzania linajitahidi mno katika hilo maana tangu mkoloni limepitia
changamoto nyingi, hivyo Polisi Tanzania wanayo mifano kedekede ya kukumbukwa
ambayo inabaki kuwa darasa kwao ambapo taasisi zingine zinapaswa kujifunza
katika hayo.
Makala haya leo yanasema nini?
“Mwanakwetu anayatumia kukumbusha tu kwa kila mmoja wetu,
kulipiga chapuo hasa hasa kwa wenye nafasi kujitahidi kutoa maagizo ya haki ,
maagizo halali ili haki iweze kustawi katika jamii ya Tanzania, haki itamalaki maana
hawa Watanzania ni ndugu wanakutana na ndugu zao wa damu pengine hata bila ya mtoa
maagizo kufahamu hilo. Pata picha kama huyu kijana angemfanyia ubaya
Mwanakwetu, pengine huyu kijana angeweza hata kupata radhi, duu angepata radhi
ya Mwanakwetu.”
Mwanakwetu Upo?
Wengine ni Ndugu wa Damu, angepata radhi
ya Mwanakwetu.
Nakutakia siku njema.
0717649257
Post a Comment