BORA KUMSHUKURU MUNGU



 

Lucas Masunzu – MAKOLE

KATIKA nenda rudi nenda rudi ya safari za jiji la Dodoma nduguyetu alikutana na kutengeneza udugu na ukaribu kwa watu wengi wakiwamo viongozi wa kisiasa, watumishi wa umma na vijana wa mtaani. Pitapita zake jijini hapo zikamkutanisha na ndugu Hamza Saire kijana muungwana mwenye asiyebeba uzandiki wala makuu kwa watu. Katika mazungumzo na ndugu huyo yapo mambo walitofautiana na nduguyetu na mengine walikubaliana wakaunga tela kwa pamoja. Kukubaliana na kutofautiana ni kawaida kwa binadamu na huo ndiyo usahihi wa mawazo.

Kadri siku zilivyoongezeka nduguyetu alibaini muungwana huyo alikuwa katika safari ya kusaka elimu maana alikuwa ni mtahiniwa wa shahada ya uzamili katika chuo kikuu cha Dodoma. Kwa udugu na ukaribu wao ilikuwa ni kawaida kupigiana simu, kujuliana hali na kutakiana heri japokuwa kuna kipindi grafu ya mawasiliano ilishuka, nduguyetu alijiuliza kulikoni?

 

Katika nenda rudi hiyohiyo mwaka mwingine wakakutana tena na muungwana huyo katika jiji hilohilo la Dodoma. Kipindi hicho sasa muungwana huyo alikiwa katika hatua ya utafiti ili aweze kuhitimisha safari yake ya elimu na hiyo ndiyo ikawa sababu ya kushuka kwa mawasiliano maana muungwana alikuwa ametingwa mno na shughuli nyeti ya utafiti. Nduguyetu anakuuma sikio kuwa yeye ni mbumbumbu wa mambo hayo ya kitaaluma lakini hali hiyo haikupunguza ukaribu wala haikuzuia kumtembelea rafiki yake.

Mazoea ya kutembeleana yakampeleka nduguyetu hadi maskani kwa huyo rafiki yake, alipongia sebuleni nduguyetu alilakiwa na muziki uliosikika kwa sauti ya juu mno kiasi kwamba wa hapa na hapa wakiongea hawatasikiana. Masikio ya nduguyetu yetu yalinasa vizuri baadhi ya maneno ya wimbo huo yaliyokuwa kwa kurudiwarudiwa.

 Bora hata nimshukuru Mungu kwa hivi nilivyo

Maana hata kuna wengine hawajafika nilipo..

Bora hata nimshukuru Mungu kwa hiki nilichopata,

Maana hata kuna wengine wamekosa kabisa.

Nduguyetu ni shabiki mzuri wa muziki, sauti ya juu hata iwe nzito inaweza kuwa tabu kwa wengine lakini si kwake.  Nduguyetu akajisemea moyoni hapa kuna jambo utomvu wa furaha kama hii kwa Saire si bure. Muungwana huyo alikuwa amehitimisha salama salimini safari yake ya masomo ndiyo maana alikuwa katika kilele cha furaha siku hiyo. Kwa hakika ukurasa umahiri kwa muungwana Saire umefungwa rasmi na ukurasa wa uzamivu unamkaribisha muungwana huyo.

Nduguyetu anasema nini leo?

Hongera ndugu Hamza Saire kwa kuhitumu shahada ya umahiri katika uongozi na usimamizi wa elimu, chuo kikuu cha Dodoma. Hongera pia kwa wanafunzi wote waliokidhi vigezo wakahitimu masomo 2023 Chuo Kikuu cha Dodoma. Nduguyetu anawapongeza wahadhiri wote Chuo Kikuu cha Dodoma kwa kufanya kazi ya kutoa elimu kwa wahitimu hao.

 

Bora hata kumshukuru Mungu, Kwa heri.

theheroluke23@gmail.com

0762665595

@ 2023 




 


 

 


0/Post a Comment/Comments