Na Eliasa Ally
MKURUGENZI wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, Bw Kastori Msigala ameliomba Baraza la Madiwani wa halmashauri hiyo kurudisha faini ya Sh 200,000 kwa bajaji zinazopita njia zilizozuiliwa.
Kwa sasa bajaji zinazokamatwa kwa makosa hayo, wamiliki wake wanatozwa faini ya Sh 100,000 kiwango kinachoonekana hakiwapi maumivu kwa kurudia kufanya makosa hayo.
Katika kikao cha Baraza la Madiwani kilichofanyika mjini Iringa leo, madiwani wa manispaa hiyo walitaka kujua ni hatua gani zinachukuliwa na menejimenti yao kuwadhibiti madereva wa bajaji wanaopita barabara ambazo hawajapangiwa ili wasilete matokeo hasi na kuvuruga utulivu.
“Moja ya barabara hizo ni barabara kuu kutoka mnara wa manispaa kwenda Kihesa. Madereva wa bajaji ambao hawaruhusiwi kupita barabara hiyo wanazidi kuongezeka,” alisema mmoja wa madiwani wa manispaa hiyo, Pascalina Lweve.
Akijibu changamoto hiyo, mkurugenzi wa manispaa hiyo alisema kuna shinda kubwa ya madereva wa vyombo hivyo vya moto kukiuka miongozo inayohatarisha usalama wao na wengine barabarani.
“Tumekuwa tukiwakamata na kuwatoza faini ya Sh 100,000. Kiwango hicho kinaonekana ni kidogo, wengi wanalipa na kurudia makosa yale yale. Nashauri turudishe faini ya Sh 200,000 huenda itawapa maumivu,” Msigala alisema.
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Iringa Ibrahim Ngwada aliiagiza menejimenti ya halmashauri hiyo kukaza kamba kwa kuhakikisha bajaji zinatoa huduma kwa kuzingatia njia walizopewa na utaratibu uliowekwa.
“Lakini pia tuanze kufikiria kuanzisha huduma ya usafiri wa abiria katika njia ya Wilolesi kuelekea Lugalo ambako watu wake wanalazimika kutembea umbali mrefu kufuata huduma hiyo,” alisema
Post a Comment