HONGERA CWT WILAYA MAGU

 



Adeladius Makwega –MWANZA

Novemba 11, 2023 Mwanakwetu alikuwa nyumbani kwake, gafla alijulishwa na ndugu mmoja kuwa katika viwanja vya Chuo Cha Maendeleo ya Michezo Malya kuna mashindano kadhaa ya michezo baina ya wanachuo na Wanachama wa CWT Magu.

Mwanakwetu alitoka zake kuelekea uwanjani, japokuwa katika michezo yote aliyotajiwa hakukuwa na mchezo hata mmoja ambao  Mwanakwetu anahusudu.

Nakuuma siko msomaji wangu kuwa Mwanakwetu anapenda sana  mchezo wa Gofu na Mchezo wa  Mashindano ya Magari, mara nyingi akiwa Morogoro huwa anakwenda kutazama mchezo wa Gofu namna mikwaju inavyopigwa viungani .

Mwanakwetu pia amekuwa na uraibu na namna magari yanavyoshindana  katika barabara mbovu zenye kona nyingi na mavumbi tele yanavyofurushwa. Yote hayo Mwanakwetu hawezi kabisa kucheza Gofu  wala hajui kuendesha  gari huo ni ulevi wake wa kutazama tu.

Mwanakwetu alifika uwanjani hapo, lakini alipokuwa hapo hali ya hewa ilibadilika hivyo mvua kuanza kunyesha, yeye na wenzake walitoka hapo mbio kuelekea kujificha mvua hii katika majengo ya chuo hiki cha umma.

Wakiwa hapo macho yake yalikutana na basi moja nzuri limesimama ambapo alipouliza aliambiwa ndilo basi lillowabeba hawa walimu kutoka Magu kwa kukodi kuja hapa Malya kushiriki michezo hiyo.

Alikimbia haraka na kufika katika jengo la pili la mkahawa la chuo hiki, hapo sasa macho yake yaliweza  kuliona basi hilo vizuri ambalo lilikuwa na ilani moja kubwa ikitambulisha mmiliki wa basi hilo kuwa ni CWT MAGU.

Jambo hlo lilimvutia sana Mwanakwetu, akasema haya ndiyo mambo yanayotakiwa kwa taasisi kuweza kumiliki mabasi na hata malori ambayo yanasaidia wanachama kuweza kufika eneo moja kwenda lingine.

Mwanakwetu akawaomba ndugu hawa kutoka Magu awapige picha wakiwa na basi lao, na kweli alikubaliwa .

Mwanakwetu alipotoka hapo alikutana na ndugu mmoja anayefahamika kama Mtweve Kayanda ambaye ni mkufunzi wa Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya.

Ndugu Kayanda alipoliona basi hilo akasema ,

“Nilipokuwa Chuo Kikuu, nilikuwa na jamaa yangu Muisilamu, aliniambia kuwa katika maisha jitahidi uwe na usafiri , kwa zamani haukuwa na budi kuwa na punda au hata ngamia ili uweza kutoka sehemu moja kwenda nyingine. Lakini kwa sasa ngamia na punda ndiyo magari , mabasi ,malori na na hata ndege. Kunapotokea dharura kwa hakika chombo hicho kinaweza kukutoa kutoka sehemu moja kwenda nyingine bila tabu.”

Baada ya mazungumzo haya Mwanakwetu na ndugu Mtweve wakaenda kuangalia michezo kadhaa uwanjani sasa mvua ilikuwa imekata.



Mwanakwetu alitazama michezo kadhaa alafu kuanza kurudi nyumbani kwake na akiwa njiani akajisemea mwenyewe ,

“Inawezekana hapo Wilaya ya Magu, Mkuu wa wilaya ana gari zuri, Mkurugenzi hivyo hivyo lakini Wilaya au Halmashauri haina basi lakuwabeba watumshi katika shughuli mbalimbali huku tu CWT wakiokoa jahazi hilo . Uwepo wa basi au lori la taasisi una maana kubwa katika michezo, misiba , harusi na hata mikutano ya jamii, mitihani na hata  nyakati za uchaguzi , huku kama Halmashauri haina vyombo hivyo vya usafiri ikikodi kwa pesa nyingi katika mazoezi kama hayo ya kitafa.”

Kumbuka msomaji wangu Mwanakwetu anaelekea nyumbani kwake huku viatu vyake vimeloana na matope kweli kweli , akajisemea moyoni,

“Basi lenye nembo ya taasisi linapokuwa barabarani linaonesha kuwa taasisi hiyo imejipanga , taasisi hiyo iko makini na inaongozwa na watu makini, hiyo ni sifa moja kubwa huku ikitangaza jina zuri la taasisi hiyo. Hongera Katibu wa CWT wilaya ya MAGU .”

Mwanakwetu akafika nyumbani kwake na kuvua viatu vyenye tope na kuingia ndani kwake.

Mwanakwetu siku ya leo anasema nini?

Mwanakwetu ana hakika kuwa katika Tanzania Bara yenye halmashauri zaidi 180 pengine zipo Halmashauri  kiduchu zinazomiliki basi mpya kama hilo. Halmashauri nyingi siyo kweli kama hazina uwezo wa kununua malori na mabasi kama hilo, Shida ni vipao mbele vyetu tu.

Mwanakwetu ana hakika zipo Halmashauri nyingi zina maombi ya ununuzi wa magari madogo ya kifahari lakini siyo basi na lori vibali vya ununuzi vimeombwa  vilipitishwa na vitapitishwa  hata baada ya kutoka makala haya, Mwanakwetu anawapa heko waombaji wa vibali na wapitishaji wa vibali vya ununuzi.

Haya ni mambo ya TAMISEMI, Mwanakwetu akakumbuka simu ya ndugu yake mmoja  juuya TAMISEMI akisema,

“Mbona Mwanakwetu unamsimanga sana  mhe Mohammed Mchengerwa? Mbona wapo mawaziri wengi ukiwapima katika mizani ya utendaji wao na Mchengerwa, Mohammed Mchengerwa ana nafuu, sasa kaka ebu tumpe nafuuu mhe Mchengerwa afanye kazi ”

Mwanakwetu akakumbuka jibu lake kwa ndugu huyu,

“Shida ni maboresho ya TAMISEMI katika Nyanja mbalimbali, ambazo kalamu ya Mwanakwetu inatupia jicho yeye kama waziri mengine hayafahamu. Maboresho ya TAMISEMI ni maboresho ya maisha ya Mtanzania masikini.”

Mwanakwetu Upo?

Hongera Katibu CWT MAGU

Nakutakia siku Njema.

makwadeladius@gmail.com

0717649257




1/Post a Comment/Comments

Post a Comment