HONGERA RIDHIWANI KIKWETE


Adeladius Makwega-MWANZA

Chuo Kikuu cha Dodoma kinatarajia kufanya mahafali yake ya 14 hivi karibuni, baada ya wanachuo wake kadhaa kufuzu katika kozi mbalimbali za ngazi kadhaa ikiwamo Shahada, Shahada za Uzamili na Shahada za Uzamivu .

Kulingana na taarifa iliyotolewa kwa umma na chuo hiki inanadi kuwa,

“Umma wote unajulishwa kuwa majina yafuatayo ya wanachuo wetu wamefuzu vigezo vyote vya taaluma na watapewa shahada zao  katika mahafali hayo ya 14 chuoni hapa.”

Mwanakwetu alipofuatilia orodha hiyo alibaini kuwa kwa ngazi ya shahada ya uzamivu kulikuwa majina sita,

“Sinyati Ndiango ambaye atatunukiwa Shahada ya Uzamivu ya Falsafa na wengine watano ambao ni Phesto Namayala, Mwaija Ngenzi, Deodatus Kazawadi, Thobias Mwesiga na Raymond Mukulasi Chrales.”

Mwanakwetu alipoendelea kusoma orodha hiyo, namba 51 alikutana jina la mh.Ridhiwani J.Kikwete ambaye hadi sasa ni Waziri Mdogo wa Tanzania anayehusika na masuala ya utumishi na katika mahafali  hayo ya 14 atatunikiwa Shahada ya Uzamili ya Mahusiano ya Kimataifa.

Mwanakwetu kwa heshima zote anawapongeza wanachuo wote wa chuo hiki waliokidhi vigezo hivyo na majina yao kuwemo katika orodha hiyo.

Mwanakwetu anapongeza wahadhiri wote waliofanya kazi hiyo kwa haki na bila upendeleo wowote ule, anawaomba waendelee na moyo huo.

Kwa namna ya pekee Mwanakwetu anampongeza mhe. Kikwete kwa kufuzu vigezo hivyo vya kuhitimu mafunzo hayo na anamtakia mahafali mema.

“Elimu hiyo uitumie katika kuwatumikia wananchi wa Tanzania, katika jukumu ulilo nalo sasa.”

Mwanakwetu anaongeza kuwa mhe. Kikwete afahamu kuwa siasa ili ziweze kufanyika vizuri mheshimiwa huyu anatakiwa awe jirani na wananchi wanyonge na wao watambue kuwa yupo nao jirani.

“Wizara yako inashida hasa ya kuweza kupenya katika wizara zingine za umma kutatua kero za watumsihi wa umma kama vile motisha, uhamisho na upandaji wa madaraja na mishahara, fanyia kazi hayo.”

Katika orodha hiyo ya wanaohtimu, mhe. Kikwete afahamu,

“Wapo wahitimu ambao wanajiuliza je vyeti vyao vitatumika lini? na watapata kazi wapi ? Hata wapo wengine ambao watapewa vyeti katika mahafali hayo na ni  watumishi wa umma lakini vyeti vyao haviwezi kuwasaidia chochote kutokana na miongozi iliyopo ambayo inahitaji maboresho madogo.Wapo wengine  wanahitimu nawe hata nauli ya bodaboda kufika katika mahafali hayo itakuwa ngumu na wapo wengine wanajua kuwa sasa wanahitimu pesa  na bodi ya mikopo hawapati tena je wataishije?.Waziri Mdogo wa Utumishi unatakiwa kuvaa viatu vya hao jamaa wote”

Mwanakwetu anamalizia kwa kusema kuwa,

“Mhe Kikwete umehitimu masuala ya mahusiano ya kimataifa, fahamu kuwa hakuna mahusiano mazuri ya kimataifa kama mahusiano ya ndani ni mabovu, lazima kuhimizwa zaidi kujenga mahusiano mazuri ya ndani ya kidugu zaidi kwa kila mmoja wetu.”

Mahafali mema.

Pia wakati wa kutafakari majibu ya masuala hayo.

Mwanakwetu Upo?

Hongera Ridhiwani KIkwete.

Nakutakia Siku Njema.

Makwadeladius @gmail.com

0717649257




0/Post a Comment/Comments