Adeladius Makwega-MWANZA
Hivi karibuni Mwanakwetu alitembelea ukurasa wa Instagram wa
Julius Mtatiro ambaye ni kijana wa Kitanzania ambaye Mwanakwetu anamfahamu ,
Julius Mtatiro akiwa kijana pekee mwanasiasa wa Tanzania ambaye alipachika Nyaraka
ya Kanisa Katoliki, inayoeleza kuhusu kuundwa kwa mahakama ya kijimbo ajili ya kutangazwa
Mwenye heri na Mtakatifu -Mtumishi wa Mungu Julius Kambarage Nyerere.
Ukurasa huu ni miongoni mwa kurasa maarufu kiasi, mpaka
Novemba 19, 2023 unamatukio ya kupachikwa 5791, ukifuatwa na watu 287K na
akiwafuata watu 2862. Kwa tabia ya ukurasa wake na tabia za uandishi wa Mtatiro,
zamani kijana huyu alikuwa anapachika habari ya ukosoaji kwa serikali sasa
anaweka habari za kijamii mno maana yeye sasa ni sehemu ya serikali na ukosoaji
wake upo likizo.
Kitendo cha Mtatiro kuipachika Nyaraka hiyo katika ukuta wa
mtandao wake wa kijamii, kilimsaidia Mwanakwetu aliiona na kuisoma taarifa hiyo
na baadaye kubaini kuwa Julius Mtatiro aliinakili kutoka ukurasa mmojawapo Instagram
wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dare s Salaam.
Taarifa hiyo katika aya ya pili inasema,
“Tunawaalika waamini wote kuwasiliana nasi moja kwa moja au
kutuma kwenye Mahakama ya Jimbo Kuu la Dar es Salaam inayoshughulikia mchakato
huu, taarifa yoyote Iwe ya kufaa au isiyofaa-kuhusu maisha na fadhila kubwa
sana za mtumishi wa Mungu, kama mwamini mlei mkatoliki na baba wa familia, pia
taarifa kuhusu sifa zake za utakatifu na nguvu ya maombezi yake.”
Msomaji wangu taarifa hiyo ya Kanisa Katolilki iliongeza
kuwa,
“Kwa taratibu za ushahidi wa kisheria, maandiko yote
yanayodhaniwa kuwa yake yanapaswa kukusanywa, Kwa Tangazo hili tunaelekeza kwamba
yeyote ambaye ana maandiko hayo ayatume kwa umakini kwa mahakama hiyo
iliyotajwa, nyaraka zozote zilizoandikwa na mtumishi wa Mungu ambazo bado
hazikabidhiwa kwa mratibu wa mchakato.”
Msomaji wangu hayo
maandishi yaliyokaa kwa milazo ni aya ya pili na ya tatu ya barua hiyo kwa
waamini iliyosainiwa na Askofu Mkuu wa Dar es Salaam Jude Thaddaeus Ruwa’ichi.
Kwa hakika waraka huo Mwanakwetu
aliona unaomba nyaraka, maandishi na miswada yote ya Mtumishi wa Mungu Julius Kambaraege
Nyerere , pia umeyatazama maisha binafsi ya Mtumishi wa Mungu huyu kwa kuomba anayefahamu
tabia zake njema na hata tabia zisizofaa.
Huku ukitaja taarifa
za kiroho za nguvu za maombezi yake kwa sasa kama zipo.
Mwanakwetu kama mwanahabari
anatumia kalamu yake kukumbusha umma wa waamini kujitokeza tu kutoa ushirikiano
kwa Mahakama hiyo ya kiroho, bila ya woga wowote, hilo ni suala la imani yetu
na lenye heshima kubwa kwa kila mlei mkatoliki.
Kama Mtumishi wa Mungu Julius Kambarage Nyerere atakuwa Mtakatifu, vizazi vyetu vitajifunza kwakwe kwa matendo yake na ucha Mungu na hata kama jina la likagoma na kutupwa katika mchakato huo waamini tutajifunza ubora ya kuishi ucha Mungu kiwango cha juu zaidi.
Mwanakwetu anaona kuwa
mbiu ya mgambo ya waraka huo wa Kanisa unahitaji kujua zaidi maisha ya kiongozi
huyu yalikuwaje? Na Majibu hayo yapo kwa wanaombwa ambao walikaa na kuishi na
Mwalimu Nyerere wakati wa uhai wake.
Mwanakwetu kwa heshima
zote anauombea heri mchakato huo, kwanza uweze kuzifikia nyaraka zote alizawahi
kuandika Mwalimu Nyerere hasa hasa zile za siri, hapo wanaweza kumfahamu kwa
karibu Mwalimu Nyerere na hapo hata hotuba zake za siri katika vikao ambavyo
havikuwa wazi na pengine hadi kesho zinawezekana kuwa bado ni siri.
Mathalani mjadala wa
waliwahi kunyogwa wakati wa utawala wake, mahakama iliamua kwa mujibi wa sheria,je
alipopelekewa hati hizo Mwalimu Nyerere alikuwa anatoa maelezo gani kwa walio chini
yake ? Je alikuwa anasikitishwa na hali hiyo au alikuwa anafanya hivyo kama kuwalipizia
kisasi waliuwa wenzao?
Maana mafaili ya
kiserikali yanakuwa na hoja, alafu mjadala unaanza kwa dokezo hadi kukamilika na kwa utaratibu wa
zamani mafaili hayo na mjadala huo mhusika (kiongozi ) na wenzake walio chini waliandika
kwa mikono yao mwenyewe, miandiko yao itaonekana.
Je mijadala hiyo
ilikuwaje? Mwalimu Nyerere alikuwa mtu wa namna gani?
Hapa shauri la mfano
ni la kunyongwa kwa Said Abdalah Mwamwindi aliyempiga risasi alyekuwa mkuu wa
mkoa wa Iringa Dkt .Kreluu. Je Mwalimu Nyerere alikuwa analipiza kisasi
kunyongwa Mwamwindi ili kumkomesha ndugu huyu kwa alichokifanya kwa mkuu wa mkoa
wa Iringa wakati huo?
Hapo Mwanakwetu
anakubaliana kabisa na nyaraka hizo ziifikie mahakama hiyo, kama ilivyosisitizwa
na waraka huo wa Kanisa katika aya yake ya tatu kwa walei wanaofahamu hayo na
maisha ya kiongozi huyu wafanye hivyo.
Msomaji wangu katika aya
pili ya waraka huu inayataja maisha ya Mwalimu Nyerere kama Baba wa familia.Kwa
hakika Mwalimu Nyerere akiwa ni mkewe Mama Maria Nyerere, walikuwa na watoto
kadhaa.
Kwa muda mrefu kumekuwa
na mjadala juu ya maisha ya ndoa ya Mwalimu Nyerere. Kumekuwa madai juu
mahusiano ya Mwalimu Nyerere na Waziri wake mdogo wa Afya Bi Lucy Lameck Somi,
ambaye alikuwa muuguzi awali na mzaliwa wa Mkoa wa Kilimanjaro, akiwa ni Waziri
wa kwanza mwanamke wa Tanganyika huru (1962) na baadaye Tanzania 1964.
Je hayo ni kweli?
Kama ni kweli mwalimu
alikuwa mtu wa upendeleo kwa kumuhonga uwaziri Bi Lucy Lameck?
Mwanakwetu anaamini jibu
moja kati mawili lipo kama ndiyo au hapana.
Kama ni kweli, Je Mwalimu
aliungama katika hilo?
Hapo mchakato huu utakuwa na majibu.
Mwanakwetu anatambua
kuwa suala la mitala kwa walei waliopitia mchakato wa Kanisa Katoliki kuwa Watakatifu
linaonekana sana kwa Mashihidi wa Uganda (22) wale waliuwawa na Kabaka Mwanga(1885-1887)
japokuwa baadhi ya watakatifu hao wengine hawakuwa na wake kabisa. Waliokuwa na
mitala hiyo baada ya kuwa Wakatoliki walichagua mke mmoja na kufunga ndoa .
Mashahidi wa Uganda
walikwenda mbali na kuwagawia ardhi na mifugo wake zao wa zamani kwa haki bila
upendeleo wowote na hakukuwa na malalamiko yoyote baada ya kuwa Wakatoliki.Tena
hawa mashahidi wa Uganda-walikuwa na watoto waliozaliwa na wake wengine kabla ya
kuwa Wakatoliki.
Mwanakwetu anasema nini
siku ya leo?
Katika maisha ya
Mwalimu Nyerere yapo ambayo yatabaki ya kujifunza sote kwa ndugu yetu huyu baada
ya mchakato kukamilika, kwa hiyo kuna umuhimu wa kutoa ushirikiana mkubwa
katika mchakato huo.
Mwanakwetu anapuliza kipenga
chake kuelekea katika mahakama hiyo, huku akijiuliza je Mtumishi wa Mungu
Julius Nyerere wakati wa Ubatizo alipewa kitambaa cheupe, je kitambaa chake
kilibaki kuwa cheupe?
Swali hilo Mwanakwetu
anajiuliza na yeye mwenyewe
“Je tangu nibatizwe mwaka 1974 je Kitambaa changu cha Ubatizo bado
Cheupe ?”
Jamani tujitokeze kutoa ushirikiano kwa mahakama hiyo inayosimamiwa na Buruda(kaka) Reginald D Cruiz wa Shirika la Wamisionari wa Afrika aliyeteuliwa na Vatikani kusimamia mchakato huo.
Mwanakwetu Upo?
Kitambaa Changu cha
Ubatizo Bado Cheupe?Cha Mwalimu Nyerere tutapata majibu.Je wewe msomaji wangu chako je ?
Nakutakia Siku Njema
makwadeladius @gmail.com
0717649257
Huyu ndiye msimamizi wa mchakato huo Bruda Cruizi(Kama picha ilivyotafutwa na Mwanakwetu kama siyo hiyo tunaomba radhi)
0717649257
Post a Comment