KUBALI KUNYESHEWA MVUA

 


Adeladius Makwega-MWANZA

Alfajiri ya Novemba 30, 2023 Mwanakwetu aliamka mapema mno, kufanya shughuli kadhaa nyumbani kwake, alafu kufungua simu yake na kutembelea makundi kadhaa, kundi mojawapo lilikuwa la Shule ya Msingi Mnazi ambalo wapo karibu wanachama 75 ambapo wote hao walisoma Shule ya msingi Mnazi Mmoja .

Kundi hili wapo Watanzania wengi na wengine wenye uraia wa mataifa mengine kadhaa waliosoma shule hii kati ya mwaka 1983-1989 wakiwa na mikondo minne A, B, C na D , huu mkondo D ndiyo alikuwamo Mwanakwetu, kila mkondo ukiwa na wanafunzi 100-120 huku darasa zima likiwa na watu karibu 500.

Kwa hiyo katika watu hao 500 kuwapata wote ni kazi maana wengine inakuwa ngumu, wengine hawataki kabisa matumizi ya mitandao ya kijamii na wengine wamefariki dunia.

Kundi hilo wapo wafanyabiashara, wapo wasomi, wapo Mashekhe wakubwa tu na wapo Mapadri na Wachungaji kadhaa. Mwanakwetu anaamini panapo majaliwa tutapata Mashehe Wakubwa, tutapata Maaskofu Wakubwa huku wapo wengi wao wamejukuu, isipokuwa Mwanakwetu peke yake lakini na yeye yuko mbioni kujukuu.

Hili ni kundi vijana wa Dar es Salaam wa zamani na wanaifahamu Dar es Salaam ya kitambo na hata ya sasa, akiwamo muungwana Mwanakwetu.

Kundi hilo wakiwa na jambo la kufanya iwe sherehe, iwe msiba kwa imani ya Ukristo au Usilamu wamekamilika, kama kafariki Mwanakwetu, parokia yake wakimtuma Katekista kuja kumzika, kundi hilo kwa hakika watatuma Padri kusalisha Misa ya Mazishi hapo itakuwa siyo Ibada tena ya Katekista.



Hilo kundi la Mnazi Mmoja limekamilika vizuri.

Katika kundi hilo saa moja na dakika 37 ya usiku wa Novemba 29, 2023 mdau mmoja alituma picha ya katuni moja ambayo imechorwa na Said Michael.

“Katuni hii inaonekana ngalawa inasafiri kutoka eneo moja kwenda lingine, ngalawa hii inasafiri katika maji ya rangi ya samawati, kwa hakika hiyo ni bahari na tena bahati kubwa, maana ngalawa hiyo inaonekana katika eneo ambalo halionekani sura yoyote ya nchi kavu kama vile miti, nyumba au mimea, ngalawa ipo Bahari Kuu.

Ngalawa hiyo siyo zile zinazotumia mashine, ni zile ngalawa za kizamani ambazo zinaendeshwa kwa upigaji wa kasia tu.-Hiyo ni Ngalawa Kongwe. Ngalawa hiyo imepachikwa nembo yenye alama mbili za rangi ya njano -Nyundo na Jembe ambazo ni alama za Chama Cha Mapinduzi(CCM), chama tawala nchini Tanzania, Taifa lililopo kando ya Bahari ya Hindi huko Afrika Mashariki.

Ngalawa hii inapita katika Bahari Kuu na huku kukiwa na vitu vyenye ncha kali vinaienga ngalawa hii kwa chini.

Ngalawa hii ina abiria watatu wanaonekana, kwa mbele yupo baba mwenye uwalaza amevaa shati la kijani, yeye anapiga kasia, katuni hii inaonesha anapiga kasia mkono wa kulia ambapo mtindo ni kulia kushoto, huyu baba mwenye uwalaza ukimtazama vizuri anashabiana fika na Makamu Mwenyeki wa CCM Taifa Mzee Abdu-rahaman Kinana. Huyu mzee mwenye uwalaza anaoneka anapiga kasia huku anapigwa na mvua, anaonekana akipiga kasia hilo kwa kasi kweli kweli, akilenga vizuri na kuyakata mawimbi na kazi hiyo inaoneka nzito.

Mvua inanyesha mzee mwenye uwalaza analoa na hana hata koti la mvua wala sweta. ‘Mzee wa Uwalaza Kuna Nimonia’ kwa hiyo maji ya mvua yanaingia ndani ya ngalawa kupitia haya matone ya mvua.Kwa nyuma anaoneka jamaa mmoja ambaye anashabiana fika na Daniel Chongolo amabaye alikuwa Katibu Mkuu wa CCM Taifa akiyatoa maji hayo kwa kutumia ndoo, huku akiwa amechomekea shati la rangi ya kijani ambayo ni sare ya CCM. Kazi hiyo ya kuchota maji inaonekana ni nzito mno, maana maji yanatolewa na mengi yanaingia ndani ni ya ngalawa nayo safari ni ndefu.

Ukiitizama katuni hii vizuri maji yote yanaingia kutoka juu yaani ya mvua ya Mwenyezi Mungu ambayo mwenyewe kairuhusu inyeshe.

Katikati ya katuni ya jamaa anayeshabiana Chongolo na huyu kama mzee wa uwalza -Kinana yupo mama mmoja ambaye amevalia sare za CCM kavaa miwani mieusi huku kajifunika mwavuli wenye rangi mbili kijani na njano. Mama huyu yeye haangalii ngalawa inakotoka wala iendapo, yeye atazama mshazari, katuni ya mama huyu anashabiana fika na Mwenyekiti wa CCM Taifa Mhe. Samia Suluhu Hassan ambaye ndiye Rais wa taifa hilo la Tanzania ambalo Rais wake wa kwanza alikuwa ni Mwalimu Julius Nyerere.

Safari ya hii ngalawa inaendelea, mama na mwavuli wake anajikinga mvua, mzee wa uwalaza anapiga kasia naye Chongolo akitoa maji katika ngalawa.

Chini ya hii katuni kuna maneno haya-Mwanahabari;

hivyo wataalam tunaomba tafsiri ya hii Picha. www. Mwanahabaridigital.co.tz

Mwanakwetu ameandika matini haya leo hii anawajibu kuwa Mwanahabari; hii ndiyo tasfri ya katuni hiyo,





“Katika ngalawa hiyo wanaonekana ni baadhi ya viongozi wa CCM Taifa kabla ya Novemba 29,2023 na inaonesha wazi kuwa vongozi wachini wa CCM wanafanya kazi vizuri kukipambani chama hicho kila mmoja na jukumu lake, shida ipo kwa mwenyekiti wa CCM Taifa. yeye mujibu wa katuni hii hasadii chochote katika kuzifanya shughuli hizo za chama hiki kikongwe japokuwa nayeye yu safarini. Kibaya zaidi mchoroji wa katuni hii ndugu Said Michael analipiga chapuo kuwa Mwenyekiti wa CCM Taifa badala hata ya kuchukua upande mmoja wa wasaidizi wake yeye anaangalia mshazari na hataki hata kunyeshewa na mvua inayowanyeshea wenzake kutoka juu; Mwanakwetu anaamini kuwa kama mvua ikiendelea kunyesha Mwenyekiti huyu atanyeshewa na mvua vizuri maana mvua zingine zina upepo mkali zinaweza hata kuupeperusha mwavuli huo.Mwanakwetu anaamini kuwa kutokana na kujihuzulu kwa Daniel Chongolo hilo linaonesha kuwa Komredi Chongolo alichoka na hilo, sasa anawaacha wengine wakaendelee na kazi hiyo. Huku Mwanakwetu aliamini kuwa ndugu Kinana ndiye alipaswa kuchoka mapema kuliko huyu kijana. Je vijana siyo wavumilivu kama wazee? Mchoraji wa Katuni hii analipiga chapuo la kumshinikiza Mwenyekiti wa CCM taifa afanye mambo kadhaa mosi akubali kunyeshewa na mvua mapema na mwavuli aliyojifunika auweke chini ya ngalawa, ashirikiane na mwenzake katika safari hiyo. Mwisho mwenyekiti achague upande kama anatazama mbele au anatazama nyuma na aache kutazama mshazari.”

Mwanakwetu Upo?



Mwanakwetu anasema,

“Mwenyekiti Shusha Mwavuli, Usitazame Mshazali na Shirikiana na Wenzako. Hapo tunaweza kufika salama safari yetu lakini hata kama tukipata katibu wa CCM Taifa mwingine tusipoyafanya hayo mambo matatu hatuwezi kufika salama safari yetu.”

Nakutakia siku Njema.

makwadeladius@gmail.com

0717649257






 

0/Post a Comment/Comments