NITAKUSEMEA KWA AFANDE MWALUKASA









 

 Lucas Masunzu – MAKOLE

SIKU ya tarehe 24 Novemba 2023 Nduguyetu alishiriki ibada takatifu. Mara baada ya ibada alipigiwa simu na mama yake wakasalimia na kuongea mambo ya kifamilia lakini kabla ya mazungumzo kumalizika swali alilotegemea kuulizwa liliulizwa. Mwanangu umekwenda kuabudu? Nduguyetu alijibu. Mama huyo naye  akajibu ubarikiwe mwanangu na simu yake ikaishia hapo.

Dakika chache simu ikaingia tena mama huyo akasema “wajomba zako wanataka kukusalimia”. Hapohapo nduguyetu akasikia “Shikamo uncle”. Mazungumzo yakaendelea vizuri kwa bahati aliyesalimia ni mtoto mdogo bado yu chekechea hana maneno mengi yeye ni mkimya akahitimisha kwa kuomba peremende mbili na pesa ya sadaka kwa wiki inayofuatia. Nduguyetu aliahidi kutimiza. Simu ikachukuliwa na mtoto mwingine wa pili ambaye yeye kanyimwa ukimya mazungumzo yakaanza hapo hapo; Mjomba unakuja lini? Kwani sasa uko wapi? Njoo umsaidie bibi kulima ananyeshewa mvua wewe haupo. Nduguyetu akajibu maswali yote hayo lakini hoja ya kunyeshewa mvua wewe haupo iligoma kuyeyuka kichwani mwake.

Ikumbukwe kwamba Nduguyetu yu mbali na nduguze si kwamba hataki kuchakalika katika kilimo la hasha, ni katika mambo ambayo hayakuzuilika kama ujuavyo dunia huwa na  mambo lukumbalukumba.


Hapohapo nduguyetu akageuza ubao wa maswali kwa huyo mtoto wa dada yake, kwa kuwa ilikuwa siku ya ibada nduguyetu aliuliza mmejifunza nini leo kanisani? Jibu likatoka alikuja Afande kanisani tukajifunza kuhusu ukatili wa kijinsia. Nduguyetu akamuuliza huyo mtoto kama ameelewa somo ampe mtihani? Mtoto akajibu kwa kujiamini nimelielewa lete mtihani.

Hapohapo nduguyetu akamwambia sikiliza kwa makini kisa hiki halafu nitakuuliza maswali.

 

Mjomba ni mwalimu wa shule. Mara nyingi anapenda kutoa adhabu kwa wanafunzi wavulana na wasichana. Kuna siku katika adhabu zake aliwaamuru wanafunzi hao wapandishe miguu ukutani huku wakielekeza vichwa vyao chini na baada ya hapo akawachakaza kwa kuwanyuka fimbo nzito. Adhabu hizo zilikuwa zikifanywa mbele ya kundi la wanafunzi na wewe ukiwemo, gauni lako ikashuka likakufunika uso wako. Adhabu za mwalimu Mjomba zimepelekea uanze kuchukia shule.

Maswali yalifuata kwa huyo mtoto; umeona nini katika kisa hiki? Je, ni aina gani ya ukatili wa umejitokeza? Mtoto huyo alijibu kwa usahihi maswali hayo. Kumbuka hapo nduguyetu anaongea na watoto wa dada yake akiwa amelowea mkoa kutafuta maisha. Nduguyetu aliuliza tena; Ninahitaji kurudi nyumbani kumsaidia bibi yako kulima, nikuletee zawadi gani mjomba? Jibu likatoka naomba uniletee zabibu.

Swali la mwisho likafuata nikirudi nyumbani halafu nikupe adhabu ya kupandisha miguu ukutani uning’inie mithili ya popo aliyepotea pango lake utafanya nini? Nduguyetu alijibiwa kuwa Nitakusema kwa Afande Mwalukasa. Kabla nduguyetu hajauliza Afande Mwalukasa ni nani, ikasika sauti ikisema mnamalizia dakika zangu na mjomba wenu. Kwa heri uwe na siku njema na simu ikakata.

Nduguyetu anasema nini siku ya leo?

Kunyamazia ukatili wa wanawake na watoto ni ukatili zaidi. Nduguyetu anapaza sauti yake kuungana na ASP Ndimbwelu Mwalukasa, Felista Shika (Mkaguzi Msaidizi wa Polisi – Dawati la Jinsia)  pamoja na Jeshi la polisi Wilaya ya Urambo katika siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto nchini.

Nakutakia siku njema, kwa heri.

theheroluke23@gmail.com

0762665595

@ 2023

 

 

 

 

 

 

0/Post a Comment/Comments