TUENDELEE KUMNANGA JAJI WARIOBA TUONE KAMA TUTABAKI SALAMA

 


Adeladius Makwega-MWANZA

Kwa hakika kumekuwa na mshangao mkubwa wa baadhi ya wanaccm na wale wanaoitakia mema Tanzania juu ya kauli kadhaa za CCM ambazo zinatolewa na viongozi wake katika majukwaa ya siasa, iwe kwa viongozi wastaafu au kwa Watanzania wengine.

Katika kutolewa kauli hizo kumekuwa na madai kuwa je hizo ni kauli halali za  CCM au ni kauli za mtu mmoja mwenyewe? Mwanakwetu anasema wazi wazi kuwa kauli hizo ni za CCM , na kujiuliuza kama ni kauli za CCM swali hilo halina maantiki yoyote.

Kwanini Mwanakwetu anaamini hivyo?

Mosi hakuna kiongozi yoyote wa ngazi ya juu aliyesimama kuzikana au kuzikanusha kauli hizo. Pili huyo anayetamka hayo hapo amefikishwa kawa usafiri wa CCM na nyuma yake akiwa na mavazi ya CCM na ulinzi wa chama hiki tawala. Na akiwa mbele ya marufaa ya CCM, Jukwaa la CCM kando yake kuna meza ya CCM.

Mwanakwetu hakuna ubishi hizo ni kauli za CCM.

Kwa hakika wanachama wa ngazi za chini kutoka mashinani wanajaribu kuzitenganisha kauli hizo na CCM yao lakini wakubwa wamekaa kimya. Huku vyombo vya habari vikitimiza wajibu wake ipasavyo kwa kuripoti kila kinachosemwa.

Kuzirudia hoja hizo haina maana yoyote kwa Mwanakwetu huko ni sawa na kumpigia makofi mtu anayemtusi mzazi wako, mbele ya umma na mbele ya familia yako, hilo likiwa kosa kubwa la uandishi.

Maswali yanayoulizwa ni mengi ,

“Kuchaguliwa kuwa Kiongozi wa ngazi ya juu wa CCM hivi sasa hicho ni kibali cha kutoa kauli za kebehi kwa viongozi wastaafu? Je kuingia katika ukumbi ambao vikao vya juu vya kamati za CCM ni kibali cha kutoa kauli za kebehi kwa wastaafu? Je Kusimama mbele ya majukuwa ya CCM ukiwa na cheo cha kuteuliwa na mkubwa ni kibali cha kutoa kebehi kwa viongozi wastaafu ? Je inakuwaje kwa viongozi wale waliopigiwa kura na majina yao kushindanishwa na wagombea zaidi ya mmoja na kushinda katika nafasi za CCM wao wanasemaje? Je unapoingia katika vikao vya juu vya CCM wewe unabeba dhamana ya kuamua lolote lile utakalo na kutamka lolote dhidi ya Mtanzania yoyote yule? Je ile misingi ya imani, utu na ahadi za wanaccm inawekwa kapuni unapokuwa na cheo kikubwa?”

Haya ni maswali ya kujiuliza pia msomaji wangu, ambayo leo hii Mwanakwetu anayapa sauti zaidi.

“Hakuna la kuficha, Jaji Joseph Warioba ni miongoni mwa Watanzania wachache mno waliopo hai sasa, waliofanya kazi kwa karibu na Mwalimu Julius Nyerere. Yeye ni miongoni mwa Watanzania wachache walioweka misingi ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977. Jaji Warioba yeye ni miongoni mwa Watanzania wachache mno walioshika nafasi kubwa za taifa hili ambao wamebeba kamusi yenye majibu ya hoja nyingi zinazohitaji majibu kutoka kwa walioliongoza taifa hili na majibu ya Jaji Warioba yakiaminiwa kuwa ya haki na ya kweli tupu. Jaji Warioba ni miongoni mwa vijana wa TANU na CCM walioweka misingi ya taifa hili inayoheshimika hadi leo”

Mwanakwetu anakumbuka sana Jaji Warioba alisema mengi wakati wa Utawala wa Benjamin Mkapa, pia alisema mengi wakati wa utawala wa Jakaya Kikwete na hata enzi za Utawala wa John Magufuli .

“Wako Watanzania wengi wameshika nafasi mbalimbali katika taifa hili na jamii haiwaamini kuwa kamusi yenye majibu. Jaji Warioba popote unapomuuliza kukupa majibu, siyo shida kwake huku mashine  za kurekodia, vipaza sauti na kamera zikimtafuta zenyewe kutokana na UKAMUSI wake.”

Mwanakwetu anaamini kuwa hata kama yupo mtu yoyote yule, kwa nafasi yake, iwe kubwa au ndogo hamuheshimu Jaji Warioba anajidanganya mwenyewe. Mtu huyo hata kama hamuheshimu Jaji Warioba kwa nafasi alizoshika katika taifa hili , Mwanakwetu anamuomba ajaribu kumuheshimu Jaji Warioba kwa umri wake.



Kwa heshima ya msomaji wa Mwanakwetu nakuomba nikukumbushe tukio hili la kweli baina ya Jaji Warioba na stephern Wassira (Tyson)

“Jaji Joseph Warioba na Stephern Wassira waligombea ubunge nadhani wa Musoma, matokeo Jaji Warioba alishinda na kuwa Mbunge . Stephern Wassira alikwenda mahakamani na shauri hilo  mahakama ilitengua ubunge wa Jaji Warioba.

Jaji Warioba aliposhinda ubunge huo awali Rais Ali Hassani Mwinyi alimteuwa kuwa Waziri, baada tu ya maamuzi ya mahakama Rais Mwinyi alimteua waziri mwingine kushika nafasi ya Jaji Warioba. Jamii ya Watanzania ilihoji kwa nini Rais Mwinyi asingalimpa ubunge wa kuteuliwa Jaji Warioba ili abaki katika serikali na Uwaziri wake?

Au nia ya Rais Mwinyi ilikuwa ni kuwapoteza vijana waliofanya kazi kwa karibu na Rais Nyerere? Mjadala ulikuwa mkubwa lakini ndivyo ilivyokuwa hivyo na Joseph Warioba alipoteza Ubunge na Uwaziri wake.”

Haya Mwanakwetu anayambuka tu, kwa waliokuwepo wakati huo wanaweza kukumbuka mwaka na hoja hata za kesi hiyo ya ubunge mahakamani zilivyotolewa mbele ya mahakama yetu .

Mwanakwetu anasema nini leo hii?

Jaji Warioba amezaa watoto na kujukuu, wapo ambao sasa ni wakubwa, wamesoma wakiwa na ujuzi wa aina mbali kama vile walimu, wauguzi, matabibu , wanasheria na wapo ambao ni wanasiasa, je tunataka wasimame huko walipo waibuke kujibu hoja? Walipize kisasi kwa walimpiga kibao mzee wao?

Jaji Warioba alipigwa Kibao wakati wa utawala wa Jakaya Kikwete, leo hii Jaji Warioba ananangwa hadharani na vijana ambao ni wajukuu zake ambao hawakuchuliwa hatua yoyote kwa kumpiga kibao, huku baadhi ya watu wakishangilia wakijidai kuwa wao ni wazalendo . Mwanakwetu anawaita  hao ni Wazalendo wa Vibao tu na siyo Wazalendo wa kweli.

Mwanakwetu anauliza je hoja ni ile ile ya Rais Ali Hassani Mwinyi ya wakati ule ya kuwaweka kando na kutowasikiliza wale vijana waliofanya kazi vizuri na karibu na Mwalimu Nyerere?

Mwanakwetu anasema kukumbuka siyo kosa kama nia ni hiyo, basi wanaomnanga Jaji Warioba waendelee kumnaga tuone kama watafika salama .

Mwanakwetu Upo?

Kumbuka tu Tuendelee Kumnanga Jaji Warioba tuone Kama Tutabaki Salama.

Nakutakiwa Siku Njema.

makwadeladius@gmail.com

0717649257



 


 

0/Post a Comment/Comments