UHAI HAUNA MBADALA

 



Adeladius Makwega-MWANZA

Novemba Mosi, 2023 Rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier aliomba msamaha kwa Tanganyika juu ya madhila yaliyofanywa na taifa lake mwaka 1905-1907 wakati wa vita vya Maji Maji huku ikikadiliwa kuwa watu kati ya laki mbili na tatu walifariki katika kadhia hiyo.

Mara baada ya tamko hilo la Rais wa Ujerumani akiwa katika ardhi ya Tanzania, Mwanakwetu alijaribu kujiuliza maswali mengi,

“Je ni kweli Ujerumani inaomba radhi ?Je kwanini maombi hayo ya radhi yanatamkwa sasa? Je vyombo vya Habari vya Ujerumani vimeipa kipao mbele gani taarifa hiyo?.”

Mwanakwetu kwanza alitembelea ukurasa wa DW Kiswahili ambalo ni Shirikla la Propaganda za taifa hilo duniani, hapa alikutana na picha moja kubwa akionekana Rais huyu wa Ujerumani mbele ya Kaburi la mashujaa hao wa Wangoni walionyongwa na Wajerumani wakati huo.

Rais huyo alionekana akifumbata mikono yake mbele ya kaburi hilo kama akisali na mbele yake wanaonekana machifu wa Kingoni ambao ndugu zao walinyongwa katika kadhia hiyo ya kusikitisha.

Mwanakwetu alipofuatilia zaidi matangazo ya mchana ya Redio ya DW KISWAHILI, siku hiyo mwongozaji akiwa Sudi Mnette ambaye ni mzaliwa wa Tanzania na huku habari hiyo ilisomwa na Amina Abubakari(Amina Mjahidi) ambaye ni mtangazaji mwenye asili ya mwambao ya Kenya.Mwanakwetu alibaini kuwa habari za siku hiyo za shirika hilo zilihusisha mataifa ya Kenya (Mfalme Charles MauMau) na Tanzania(Rais wa Ujerumani MajiMaji).



Huku akijiuliza je mataifa haya ya Ulaya yana nini na MajiMaji na MauMau ambapo wazee wetu walifariki dunia.

Mwanakwetu anaendeleau kufuatilia vyombo vya Habari vya Ujerumani.

 “DW ENGLISH walikuwa na video ya dakika tano na sekunde moja, kazi hiyo ilitayarishwa na Katharina Kroll ambaye ni raia wa Ujerumani, kwa hakika Katharina alielezea tukio hilo kama lilivyokuwa pale Songea. Japokuwa picha ya utambulisho wa Video hii mwanzoni hakuonesha Rais wa Ujerumani katika kaburi pale Songea, ambayo ilipaswa kuwa picha ya utambulisho mwanzoni.Kwa hiyo kwa katharina  Kikao cha machifu na  rais wa UJermani kilikuwa na umuhimu kuliko heshima kwa kaburi hilo.Japokuwa picha heshima ya Rais wa Ujerumani iliwekwa ndani ya video hiyo.”

Mwanakwetu anafuatilia je hawa Wajerumani wanaomba msamaha kweli? Maana waliofariki katika vita hivyo si Wangoni peke yao bali makabila mengi ya Tanganyika. Kwani hata hawa Wangoni wanaotajwa kama Wangoni wao walikuwa mabwana wa vita walioleana na makabila mengine mengi, iwe kwa kuwachukua mateka au kwa hiari.



Msomaj wangu kwa bahati nzuri, wakati tukio hilo la kuomba radhi linaendelea huko Songea, Mwanakwetu alikuwa jirani na mtu mmoja ambaye yeye ana asili ya Songea na ni Mngoni kwa baba na mama yake.

Ndugu  huyu alisema maneno haya,

“Ni kweli Rais. Frank-Walter Steinmeier ameomba msamaha, na mtu anapokuomba msamaha lazima umsamahe. Yule anayekuja kuomba msamaha anaweza akawa kauliza, ‘je nikiwaomba msamaha hawa jamaa watasamehe?’ Anaweza akajibiwa na wale anaowauliza, ‘Hawana shida wape ujimbi(pombe) tu na posho kidogo watasame na mambo yataenda vizuri.’ Inawezekana maombi ya msamaha huo yana jambo. ”

Ndugu huyu akaongeza kuwa huyu anayekuja kuomba msamaha, anakufahamu kuwa wewe utasamehe na atakuyarishia ujimbi na pesa.

“Rais huyo wa Ujerumani Frank-Walter Steinemeier pamoja na kueleza fedheha iliyosababishwa na madhila hayo amesema Ujerumani iko tayari kushirikiana na Tanzania kuelekea mchakato wa pamoja wa kuyaangalia madhila ya kihistoria,huku akitilia mkazo kwamba kilichotokea ni historia ya pamoja kati ya Ujerumani na Tanzania inayowahusisha wazee waliotangulia wa pande zote mbili.

Ameahidi kuufikisha ujumbe nchini Ujerumani kwa yaliyotokea  ili watu wengi zaidi nchini Ujerumani wayafahamu. Kadhalika aliwaahidi Watanzania kwamba atahakikisha kwamba Wajerumani watakuwa tayari kuyatafuta majibu kwa pamoja na Watanzania ya maswali ambayo hayajapatiwa ufumbuzi na ambayo yanawakosesha usingizi Watanzania.”

Ujerumani yawaomba radhi Watanzania kwa madhila ya Ukoloni – DW – 01.11.2023

Hayo yalikuwa maelezo ya DW KISWAHILI, hoja ni ileile Ujimbi na Pesa.

Hapo  hapo Mwanakwetu akayakubali maelezo ya ndugu yake huyu Mngoni wa Songea.

Jambo la kusikitisha hata Watanzania wasomi ambao walihojiwa na vyombo vya habari vya kimataifa Novemba Mosi , 2023 waliingia kuicheza ngoma hiyo ya Ujimbi na Pesa.



Kwa mfano,

Sudi Mnette wa DW KISWAHILI aliongea na Mtanzania aliyemtaja kama Mwanahistoria ambaye alikubaliana na maombi hayo ya radhi, ambalo hilo Mwanakwetu anakubaliana nalo na hata huyu Mngoni wa Songea anakubaliana nalo. Msomi huyu alisema mabaki ya miili ya mashuja hayo yarudishwe na kuzikwa kwa heshima zote, hilo Mwanakwetu anakubaliana nalo na hata huyu Mngoni wa Songea anakubaliana nalo.

Shida ilikuja katika swali la mwisho la Sudi Mnette,

“Unajua inapotokea suala la radhi na mambo kama hayo inatajwa suala la fidia.”

Dkt Mohammeda Said akajibu,

“Kama umemdhulumu mtu lazima umlipe fidia .”

01.11.2023 Matangazo Ya Mchana – DW – 01.11.2023

Msomaji wangu hoja ni ileile ya Ujimbi n a Pesa.

Je Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?

Mwanakwetu anasema kuwa ndugu zetu hawa mashujaa wa vita vya Maji Maji malipo yao siyo ujimbi na fedha, kama malipo yao yangalikuwa hayo  wasingeweza kuingia katika kuhatarisha uhai wao.

“Hakuna mtu yoyote anayeweza kulipa gharama ya uhai kwa mtu aliyeupoteza.”

Shida ni moja kwa sasa anayeomba msamaha na hata anayesamehe hawakuwepo wakati tukio hilo linatokea ndiyo kusema kuomba msamaha ni kwepesi na hata kusamehe pia ni kwepesi.

Funzo kubwa hapa ni kuwa,

“Kila serikali zinapokuwa na mamlaka yake kuna vipindi zinaweza kuingia katika migogoro iwe ya Kisiasa na hata kiuchumi. Migogoro isipelekwe katika kupoteza uhai wa watu , maana hao wanaofanywa hivyo hawawezi kulipa uhai huo na uhai hauna mbadala wake.”

Mwanakwetu Upo?

Uhai Hauna Mbadala

Nakutakia siku Njema.

makwadeladius@gmail.com

0717649257

 


 


0/Post a Comment/Comments