Adeladius Makwega-MWANZA
Mwanakwetu amekuwa akitafakari utenguzi wa aliyekuwa Naibu Waziri wa Katiba na Sheria wa Tanzania Bi
Pauline Gekul umefanyawa kwa haraka sana, huku akisikiliza hoja mbalimbali na mazingira
ya kazi ya mwanasiasa huyu wa Tanzania ambaye ana asili ya upinzani na sasa yu
chama tawala cha taifa hilo lililopo Mashariki ya Afrika.
Mwanakwetu yupo upande
wa wanaoamini kuwa jambo hilo lilipaswa kupewa muda mrefu ili kuweza kutambua
shida ya tukio hilo linalodaiwa kufanya na mheshimwa Gekul linatokana na nini?
Katika hoja hiyo, kumekuwa madai kuwa Pauline Gekul ni mwanachama
wa Umoja wa Wanawake Tanzania(UWT). Wanaodai hivyo wanakwenda mbali na kuyataja
majina ya waliokuwa na nafasi za juu wakati wa kura za maoni CCM mwaka 2020,
walikuwa pia wanachama wa UWT, yakitajwa pia majina mawili ambayo inadaiwa miongoni
mwao ni Wakuu wa Wilaya katika serikali ya sasa ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania ambayo ni nafasi ya kuteuliwa na rais, lakini pia hoja hiyo
inasindikizwa na bashilafu ya hata Rais mwenyewe wa sasa wa Tanzania Samia
Suluhu Hassan anayo kadi ya UWT na ni mwanachama wa umoja huo wa wanawake unaotokana
na bendera ya CCM yenye nyundo na jembe.
Huku utenguzi huo uikitazamwa kama nyundo ya kumponda Pauline
Gekul na jembe kujimba shimo na kumfukia mwanasiasa huyu katika kaburi la kwa
heri siasa mapema kabla ya 2025 ambapo uchaguzi Mkuu wa Tanzania unatarajiwa
kufanyika.
Watoa hoja hii akiwamo Mwanakwetu wanaamini kuwa viongozi
wajuu wa Serikali katika mataifa masikini na yale yanayosonga mbele wajitahidi
mno kuwa wavumilivu kuelekea kufanya maamuzi maana katika mataifa hayo, nyadhifa/cheo ni chanzo cha kipato na kupoteza nafasi ni kupoteza kipato, watu wanapigania
nafasi hizo kwa uvumba na ubani.
Mtazamo huu unakwenda na ukimtazama Pauline Gekul akiwa na
asili ya upinzani,
“Je anafanyiwa hivyo kwa kuwa hana asili ya CCM?"
Hilo ni swali .
Madai hayo yanachagizwa pia na hoja kuwa Pauline Gekul ni
miongoni mwa wanasiasa ambao waliandaliwa katika ulimwengu wa siasa za Tanzania
na Dkt Wibload Slaa ambaye nayeye alifutiwa hati ya heshima ya kibalozi mwaka
huu huu 2023 na rais wa sasa wa Tanzania.
Malalamiko hayo juu ya maamuzi hayo yanajengwa na dhana moja juu
ya mgogoro wa Pauline Gekul na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Manyara wakati huo
ndugu Charles Makongoro-Nyerere juu ya hoja ya mwekezaji aliyetaka kuwekeza
katika mojawapo wa maeneo hapo Babati Manyara ambapo Bi Pauline Gekul alipinga.
Kwa hakika Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu
Hassan alimuhamisha ndugu Makongoro na kumpeleka mkoa mwingine. Hapo hapo
kukiwa na maswali ya hulka za Charles Makongoro-Nyerere , kwa desturi huwa ni
mtu mpenda furaha ambaye hapendi mikwaruzano. Swali iweje kutokee mikwaruzano
baina ya Charles Makongoro Nyerere na Pauline Gekul wakati hao wote waliwahi
kufanya siasa za upinzani kwa nyakati tofauti?Huku Charles Nyerere siyo kiongozi
mwoga?
Hapo wapo wanasiasa wengi wa upinzani ambao ni rafiki wa Charles
Makongoro Nyerere na marafiki wa Pauline Gekul? Charles Nyerere amewahi kuwa
Mbunge wa Arusha Mjini na anaifahamu mno Babati na wapo rafiki zake kadhaa wa
NCCR Mageuzi wakati huo na sasa wapo CHADEMA?
Mwanakwetu anamfahamu Charles Makongoro Nyerere wa mwaka 1996
wakati Augustine Mrema anagombea Jimbo la Temeke kupitia NCCR Mageuzi ambapo
Mwanakwetu alikuwa anaishi jirani na ofisi ya Wilaya ya NCCR Mageuzi Keko
Magorofani.
“Charles Makongoro tangu wakati huo alikuwa anashiriki siasa,
anafanya mikutano ya wazi, akimaliza wanarudi NCCR Mageuzi Ofisini wilayani
Temeke wanaingia ndani, wanakaa kidogo alafu wanaingia mitaani kuishi vizuri na
jamii ya Keko na baadaye usiku kuondoka zake nyumbani kwake, yeye alikuwa ni mtu
furaha na siyo mtu wa ugomvi na mashindano yasiyokwisha.”
Katika hili juu, maswali yakiwa mengi,
hasa hulka za Charles Makongoro Nyerere, hapa kuna ufanyaji wa kazi wa Mkuu wa
Mkoa yoyote katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, unaongoza kwa karibu na
wajumbe wa kamati ya ulinzi a usalama ya mkoa huo. Je walikuwa wanamshauri nini
Mkuu wa Mkoa Charles Makongoro Nyerere?
Je hao wajumbe ndiyo waliweza
kubadilisha hulka za Charles Makongoro Nyerere? Je hao wajumbe wa kamati hii ya
usalama wilaya na mkoa ndiyo walikuwepo wakati kura za maoni CCM 2020
zinafanyika?
Je wakati Charles Makongoro Nyerere
anahama kwenda mkoa mwingine, je wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama tangu
wilaya ya Babati na mkoa walibaki wangapi? Je mwenendo wa utoaji wa taarifa
dhidi ya Pauline Gekulwa wajumbe hao ulikuwaje ?
Je ulikuwa na mazuri mengi au mabaya
mengi?
Jeshi la Polisi Tanzania ni miongoni mwa wajumbe wa kamati hizi
za Wilaya na Mkoa, nakuomba msomaji wangu hawa mara nyingi Wakuu wa Polisi Wilaya
na Mikoa wanahamishwa sana sana , katika hili tunawaondoa na hatupaswi
kuwasonta kidole hata mara moja. Hapo zinabaki idara na taasisi zingine je
mwenendo wao ulikuwaje tangu mwaka 2019 hadi kutokea utenguzi wa Pauline Gekul
Novemba , 2023.
Nakuomba msomaji wangu tusema, wajumbe hao wa kamati hii walibaki
wakapata mkuu wa mkoa mpya, je mgogoro huo wa Charles Makongoro Nyerere na
Gekul utakuwa umeondoka au umebaki?
Msomaji wangu jibu unalo.
Mwanakwetu ana hakika kuwa Gekul kwa muda mrefu alikuwa na
mahusiano mazuri na Katibu Tawala wa Wilaya hiyo, maana akiwa Naibu Waziri wa
Habari na baadaye Naibu Waziri wa Utamadani , huyu katibu tawala ndiye mwenyekiti
kamati ya michezo ya wilaya na mara
nyingi alishiriki vikao vya kiongozi huyu, hapo Mwanakwetu ameona kwa macho
yake.
Hadi tukio hilo lililosababisha Gekul kupokwa Unaibu Uwaziri,
Rais Samia Suluhu Hassan alifanya mabadiliko ya Baraza la Mawaziri ambapo Waziri
Dkt .Damas Ndumbaro alihamishiwa Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo naye
Pindi Chana kuhamishiwa Katiba na Sheria. Kupelekwa Pindi Chana Wizara ya Katiba
na Sheria maana yake Pauline Gekul alikuwa chini ya akina mama mwenzake.
Kwa hakika Pauline Gekul kule jimboni, jimbo hilo ni la
mkoani, Gekul yupo chini ya mama mwenzake Mkuu wa Mkoa.
Swali ni je mahusiano baina ya Pauline Gekul na wanawake
wenzake yakoje? Je Pauline Gekul anaweza kufanya kazi vizuri akiwa chini
wanaume au chini ya wanawake wenzake? Katika hilo yupo anayefahamu jibu.
Je kuwa chni ya wanawake, mwanasiasa huyu ilikuwa ni makusudi
au ilitokea tu?
Kwa bahati nzuri Mwanakwetu hilo alilifanyia kazi kwa kina na
kuzungumza kwa kirefu na mwanasiasa mmoja wa Tanzania ambaye ni mwanamke
anawafahamu kwa karibu Gekul na hata aliogombea nao kura za maoni CCM na huyu
aliyeongea na Mwanakwetu ni mwenyeji wa huko huko.
“Kaka Makwega, kusema ukweli wa Mungu mahusiano ya Gekul na
wanawake wenzake yana shida.Hilo ndiyo lilivyo kwa wanawake wengi na hata mimi
naamini huwa hatupendani.”
Hilo Mwanakwetu lilimpa picha kuwa kama hilo ni kweli, Je Pauline
Gekul kuzungukwa na akina mama wenzake ulikuwa mtego wa kumkwamsia ili aharibakiwe?
Hilo ni swali la kujiuliza.
Hapa tunaweza kwenda mbali zaidi, hawa akina mama waliongoza kura
za maoni miongni mwao ni Wakuu wa Wilaya Je waliteuliwa kipindi cha John
Magufuli ? Je hao akina mama hao wana mahusiano gani na mwenyekiti wa sasa wa CCM
taifa?
Msomaji wangu Mwanakwetu ameukumbuka wimbo huu wa CCM wenye
jina Kuzaliwa Kwa Chama.
.........................................................................................................................................
“Kuzaliwa Kwa Chama,
Cha Mapinduzi,
KImetuongezea Wananchi
Imaniiii,
Matumainiiiiiii Na
nguvu Mpya ,
Katika Kuendeleza
Mapambano ya Ukombozi wa Afrika,
Sisi WanaCCM Lazima Tujenga
Siasa ya Kweli ya Kijama,
Tujihadhalishe na Tabia
Mbaya,
Kama Vile Rushwa, Wizi Magendo Upendeleo na Ulevi ooo Jamaa
Kwani Vitendo Hivyo
Hudhohofisha Lengo Letu
Kwani Vitendo Hivgo
Hudhofisha lengo Letu
La Kujenga Ujamaa na
Kujitegemea.
..........................................................
Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?
Msomaji wangu kwa hakika utenguzi wa Pauline Gekul ulifanywa
kwa haraka, viongozi wetu wajenge tabia ya uvumilivu kwa wenzao, wananchi wa
Tanzania ni wavumilivu mno kwa viongozi wao. Huko mtaani nchini Tanzania yapo
mengi. Kwa hakika kila kiongozi wa taifa hilo tangu mkubwa na hata mdogo
afahamu hilo, jamani vumilianeni.
Mwanakwetu Upo?
Mtaani Yapo Mengi, Kwa Wakubwa na Wadogo, Vumilianeni, Utenguzi
Gekul Umeharakishwa.
Nakutakia siku njema.
0717649257
Post a Comment