WAZAMANI HAANZI MOJA

 


Adeladius Makwega-MWANZA

Mwanakwetu aliingia katika kundi mojawapo la mtandao wa kijamii na kukutana na bango moja zuri la Chama Cha Walimu Tanzania (CWT). Bango hlo lilimvutia sana Mwanakwetu, hivyo alilitazama na kulifungua na kukutana na picha moja nzuri ya viongozi CWT huku wakitoa ujumbe wao kwa wanachama wao.

Baadaye alilikuza na alipotazama picha hiyo alikutana na picha ya mama mmoja anayemfahamu. Mama huyu sasa ni mtu mzima, anakaribia miaka 50, ni mrembo vile na anazeeka na urembo wake.

Msomai wangu usiulize swali mbona Mwanakwetu anamsifia sana mama huyu?

“Unaweza kuwa mrembo na hata mtanashati ukiwa kijana lakini ukizeeka unakuwa tofauti, lakini mama huyu anazeeka na urembo wake.”

Mwanakwetu akaikuza picha hiyo na kukata kipande cha huyu mama mtu mzima, anayezeeka na urembo wake na kiongozi wa CWT, alafu akawauliza wenye kundi.

“Jamani hamjambo?”

Maneno haya ya Mwanakwetu akayaweka chini ya picha ya mama huyu, wana kundi waliibuka huko walipo, wengi wakamtumia ujumbe Mwanakwetu kwa siri na wengine wakatuma hapo hapo katika ukurasa wa kundi hilo hadharani.

“Mwanakwetu vipi? Unafahamu?Mwanakwetu umevutiwa na rangi? Mwanakwetu umependa mvi?”

Mwanakwetu akajibu akisema kuwa anamfahamu vizuri sana mama huyu maana amesoma naye Chuo cha Ualimu Kasulu Kigoma mwaka 2001-2003 Stashahada ya Ualimu.

Wadau wa kundi hilo wanashangilia mno ,

“Kweli penzi ni kikohozi, kulificha hauwezi. Mwanakwetu kaongea hadharani juu kiongozi wetu wa CWT?”

Mwanakwetu akaulizwa unataka kujiunga na CWT? Naye muungwana Mwanakwetu akajibu,

“Hapana jamani, mimi ni mwanachama wa CWT mstaafu na hata nimewahi kuwa Katibu wa CWT wa Tawi,japokuwa kuna wakati cheo hicho huwa ninakisahau katika wasifu wangu”

Wadau wanauliza kwa kurudia,

“Kumbe Mwanakwetu ni Katibu Mstaafu wa CWT?”

Mwanakwetu akajibu,

“Mimi ni mtu wa Solidarity Forever na nilipokuwa Katibu wa CWT tawi, vikaoni wimbo huo ulikuwa ukiimba mashairi yote kwa vitendo na mwenyekiti wangu alikuwa Mwalimu Gange  pale Isimani sekondari Iringa Vijijini.“

Mjadala ndani ya kundi hilo unaendelea , hapo hapo Mwanakwetu akaomba namba ya simu ya mama huyu.



Jamaa mmoja akatuma ishara ya upendo wa agape na vidole viwili na mdau mwingine akaandika maneno haya.

“Wazamani Haanzi Moja.”

Wadau wa kundi hilo wanaendelea kujadili wanasema,

“Kumbe Mwanakwetu ni mchangamfu namna hiyo! Mara zote tumezoea kusoma makala zako ndefu,  kumbe na yeye ni bingwa wa kuchangamsha  kundi eee, uwe unafanya hivi kila mara kaka.”

Hapo Mwanakwetu anacheka tu.Hapo hapo mdau mwingine akarudia kuandika maneno haya,

“Chezea CWT wewe! Kiongozi wa CWT, anayeisifia mvua imemnyea-  Wazamani Haanzi Moja.”

Mama mmoja muungwana ambaye ni mwalimu akamtumia ujumbe Mwanakwetu kwa siri,

“Ni kweli unaitaka namba ya huyo kiongozi?”

Mwanakwetu alijibu ndiyo na kupewa miadi ya kutumiwa nambari hiyo. Kweli baada ya siku mbili Mwanakwetu alitumiwa namba hiyo ya ndugu yake huyu aliyesoma naye Stashahada ya Ualimu mwaka 2001-2003.

Mwanakwetu akampigia simu na kuongea naye mengi, na kukumbushana maisha yao ya zamani wakati wanasoma Stashahada hiyo ya Ualimu.

Mwanakwetu alimkumbuka dada wa huyu mama mrembo kuwa walisoma naye na dada yake ambaye alikua akisoma masomo mengine ya ualimu kazini , Je yu wapi?

“Dada anaumwa sana na tunatarajia kukamilisha matibabu yake ya kufanyiwa upandikizaji wa figo na gharama yake karibu milioni 30, hivyo tunaomba mchango wako.”

Mwanakwetu akajibu kuwa hakuna neno, ikifika mwisho wa mwezi wapangaji wake wakimlipa kodi atatuma mchango wa laki moja kwa ajili ya zoezi hilo.

Mama huyu mwalimu akamuunganisha Mwanakwetu katika kundi la familia yao na kuona mwenendo wa michago, ilipofika Oktoba 30, 2023 wapangaji wa Mwanakwetu wakampa haki yake, akachukua pesa hiyo aliyoahidi na kutuma kwa mhusika.

Hadi tarehe hiyo karibu milioni 29 zilishakusanywa.



Hapo hapo Mwanakwetu akajifunza mambo mengi ,

Zoezi hilo linaendelea, mama huyu ni mtumishi wa serikali mstaafu lakini huduma hiyo haikuwapo katika mfuko wa NHIF ambayo amechangia tangu mwaka 2000 hadi anastaafu.Mama huyu akiwa miongoni mwa wachangiaji wa kwanza kwanza  wa NHIF.

“Moyo wa familia hii wanavyojitoa kuokoa uhai wa ndugu yao, Muda wa kuchangia fedha hizo ni mrefu huko afya ya mgonjwa lazima izolote.”

Haya yanakuja akilini mwa Mwanakwetu .

“Namna NHIF inavyoshindwa kutoa huduma za matibabu kwa wanachma wake, Je huo mfuko wa BIMA YA AFYA KWA WOTE unaweza kutoa majibu ya matibabu kwa mgonjwa kama huyu?”

Hapo hapo Mwanakwetu akamkumbuka mgonjwa kama huyu ambaye awali alikuwa raia wa Tanzania na sasa ni raia wa Ireland, taifa hilo linampatia matibabu hayo. Akiwa amelitumikia taifa hilo kwa miaka 17 aliyofanya kazini katika taifa hilo.

Wakati amezidiwa ndugu huyu wa Ireland, aliombwa na nduguze arudi nyumbani Tanzania  mwenyewe alijibu,

“Jamani mimi kwa sasa ni raia wa taifa hili, huko Tanzania ni nyumbani kwetu lakini mifumo ya matibabu ni migumu nitakufa mapema niacheni huku huku nisogeze mbele siku zangu za kuishi duniani ili nitubu dhambi zangu.”

Mwanakwetu siku ya leo anasema nini?

NHIF mpaka sasa imeshindwa kutatua kero za wanachama wake wanaochangia kila mwezi na wengine ndiyo hawa tunahangaika kwa kuwachangia kujaribu kuokoa maisha ya ndugu zetu.

Jambo hilo linaweza kumkuta mtu yoyote yule, iwe anayeandika makala haya au wewe unayeyasoma makala haya, au wewe ulipo NHIF kwa sasa au wewe unayeshiriki kuuandika muswada wa BIMA YA AFYA KWA WOTE.


Mfuko wa Bima ya Afya kwa Wote hauwezi kutatua kero ya matibabu kwa Watanzania wote. Mfuko wa Bima ya Afya kwa wote lazima kwanza upunguziwe mzigo kwa wale NHIF wabaki na mfuko wao waendelee kufanya maboresho nak uendelea kuwahudumia wanachama wao huku wakitatua kero zilizopo.

Mfuko wa Bima ya Afya kwa wote wenyewe uanze na ambao hawana Bima ya Afya ambao ni Watanzania wengi ambao ni ndugu zetu.

NHIF isiguswe kwa chochote, iwe mali zake, wala mtaji wake wale majengo yake. Kitendo cha Kuiunganisha NHIF na Mfuko wa Bima ya Afya Kwa Wote hilo ni kosa aubwa, hicho ni Kichaka cha kuficha madhaifu ya NHIF na kuupoteza uzoefu wake miaka karibu 24 ili kuunda mfuko mwingine ? Hilo halikubaliki..



Mwanakwetu Upo?

Kumbuka tu msomaji wangu na kundi lile walivyokuwa wakimtania Mwanakwetu ,juu ya yule mama mrembo, aliyesoma na Mwanakwetu ualimu, wakasema Wazamani mara zote Haanzi Moja. Hata hilo liwe kwa NHIF yeye ni wazamani karibu miaka 24 sasa, hao BIMA YA AFYA KWA WOTE waanze moja na wao tuone kama watafika wapi?

Kuiunganisha NHIF na BIMA YA AFYA KWA WOTE ni kosa kubwa.Bima ya Afya Kwa Wote isisafilie nyota ya NHIF iwe nyota nzuri na hata iwe mbaya.

BIMA YA AfYA KWA WOTE ianze kwa uwekezaji wake wenyewe

 

Nakutakia siku Njema.

makwadeladius@gmail.com

0717649257




0/Post a Comment/Comments