Adeladius Makwega-DODOMA
Nilipokuwa mwanafunzi wa shule ya msingi nakumbuka katika
somo la Kiswahili tulikuwa tukifundishwa mada mojawapo ya kukuza misamiati ya
lugha. Hapa tulitakiwa kutaja kinyume cha maneno na neno majawapo ambalo
lilikuwa likiulizwa kinyume chake ni neno MCHOYO, ilikuwa tabu sana kupata,
masahihisho hapo ndipo nilitambua kinyume cha MCHOYO ni MKARIMU.
Neno Mchoyo linatokana na neno Choyo ni tabia anayokuwa nayo
mtu kutotaka kutoa kitu kwa mtu mwingine. Pia uchoyo unaweza kuitwa kuwa ni
UBAHILI, UROHO, UNYIMIVU na UGUMU.
Kwa hiyo unapoweka kiambishi M+CHOYO anakuwa mtu mwenye tabia
hizo.
Neno Mkarimu linatokana na neno Karimu ni tabia ya mtu kutoa
na kuwasaidia watu wengine/mtu mwenye tabia hizo. Pia inamaanisha enye KUTOA au
KUKIRIMU.
Mwanakwetu leo kwanini anayakumbuka haya?
Julai 2, 2022 nilijifunza jambo moja kubwa kutoka jamii kwa
wakazi wa Chamwino Ikulu, mkoani Dodoma.
“Ndugu yangu kanisa langu ninalosalia haina hadhi yangu
naombeni msaaada tunataka kuliboresha sasa naomba mchango wako.”
Nilimsikia kwa masikio yangu akipiga simu kwa marafiki zake
wakati tunaanza ujenzi wa kanisa letu, alisema ndugu mmoja mtoa ushuhuda ambaye
alikuwepo siku hiyo.
Kweli simu zake zote alizopiga kwa watu kadhaa zilizaa
matunda na tukaweza kujenga kanisa letu hadi leo hii linaonekana namna lilivyo.
Ndugu yetu huyu hakuishia kujenga kanisa lake tu bali, mbinu
hiyo hiyo ilitumika kuujenga msikiti kando na eneo letu ambapo lipo umbali
mchache kutoka Ikulu ya Chamwino na kweli ndoto ya kuwa na majengo ya ibada
ilikamilika kwa baadhi ya dini na madhehebu.
“Wengine wanaweza kudhani kwa kuwa alikuwa rais basi alikuwa
akihomola (akichota) pesa kutoka huko serikalini akatoa ili tujenge kanisa na
huu msikiti la hasha hilo hatukulishuhudia, bali masikio yetu yalisikia sauti
ya simu zilizopigwa kwa watu mbalimbali na macho yetu kuona watu hao kuchangia
nyumba hizi za ibada kila walipojulishwa.”
Alisema ndugu huyu.
Kiu ya walio wengi kutoka madhehebu ambayo hayakujaliwa
kunufaika na harambee zake ilikuwa je akimaliza msikiti atasaidia dini au
dhehebu lipi? Hapa Chamwino Ikulu. Bilauli hiyo yenye maji ya kukata kitu kwa
dini na madhehebu yaliyosalia hapa Chamwino Ikulu ilizikwa kaburini kwake huko
Chato mkoani Geita.
Swali ambalo ninakuacha nalo msomaji wangu kwa leo ni Je
Magufuli alikuwa mchoyo au mkarimu? Nawewe unayesoma makala haya ni MCHOYO au
MKARIMU?
Nina hakika msomaji wangu jibu lako unalo.
Nakutakia mwaka mpya mwema wa 2024.
makwadeladius@gmail.com
0717649257
Post a Comment