HASA WEYE KIKWETE

 



Adeladius Makwega

Mwanakwetu amepigiwa simu Wakwere wa Chalinze, wanamlingishia kuwa hajaalikwa kwa mheshimwa Ridhiwani Kikwete katika shughuli hapo kwakwe, kwa kuwa kuna shughuli kama ya kuwatoa wali, waungwana hao ambao ni rafiki wa karibu wa Mwanakwetu walisema wanajipanga kuweka mambo sawa kuelekea katika shughuli hiyo.

Mwanakwetu akasema aaha kumbe Ridhiwani anawatoa wali eee?

Jamaa wakasema ndiyo. Mwanakwetu akawaambie, mimi nitaalikwa na Mbunge Mbagala na hata Mbunge wa Ulanga huko ndiyo kwetu.

Katika kuambiwa hivyo Mwanakwetu akawa na hamu ya kutaka kujua, hao wali ni wa kike wa kiume? Jamaa wakasema hilo halikuhusu kabisa hii shughuli ya Wakwere, Wapogoro kaeni mbali.

Mazungumzo yakaendelea kama nusu saa nzima, jamaa mmoja miongoni mwa hao Wakwere akasema,

“Mwanakwetu mimi nakwenda huko, tayari viwalo vyangu nimeshaanda lakini nina shida moja tu, sina kibwaya, hivi nitavipata wapi ?”

Mwanakwetu akacheka sana alafu akaanza kuwananga Wakwere hao,

“Nyinyi, nyinyi si mmeikata miukindu yote, mnajifanya nyie mahodari wakutengeneza makapu na mikeka ya kuuza, sasa shauri lenu,mnategemea mtatambika vipi wakati ukindu wote mmekata?”

Mwanakwetu akawambia kama mnayo laki mbili nikutafutie vibwaya maridadi cha Ukindu, jamaa hawa wakawa wanacheka , alafu mmoja akasema Mwanakwetu acha kukomoa.

Mwanakwetu akasema kama mnataka niwaelekeze vilipo vibwaya vya bei poa, basi na mimi mniambie hao wali wanaotoka ni wa kike au wakiume?

Jamaa mmoja miongoni mwao, kuyafanya mambo yawe mepesi akasema ni wakike, jibu hilo Mwanakwetu alitambua siyo la uhakika bali limejibiwa tu ili waelekezwe namna ya kupata vibwaya.

Mwanakwetu akawaonea huruma sana Wakwere hao alafu akawambia,

“Chukueni majani ya mgomba yaliyokauka, yasokoteni vizuri, alafu chukueni kamba ya mgomba iliyokauka ilowekeni katika maji alafu yale majani yaliyokauka ya mgomba yaliyosokotwa yafungwe katika kamba hiyo kwa kuning’iniza na kama ukiyasokota vizuri , kibwaya chako kitakuwa kizuri na kwa hakika mambo yatakuwa mazuri.”

Ndugu hao wakashukuru sana, wakawa na amani ya kujianda na sherehe hiyo ya ndugu yao mhe.Ridhiwani KIkwete, Mbunge wa Chalinze inayotarajiwa kufanyika hivi karibuni.

Mwanakwetu akawaambia hawa jamaa jambo,

“Zamani Wakwere walikuwa na msemo- MWALI KALOZA, hilo lilikuwa ni jambo la hatari mno, maana anayetajwa kwa neno hilo alikuwa hawezi kuolewa kabisa. MWALI KALOZA maana yake mwali huyo mambo yameharibika kabla ya harus/ndoa.Kuelekea hatua za kutambua MWALI KALOZA, mabibi wa Kikwere kikosi kisichozidi watu wanne kilifanya kazi hiyo katika chumba cha siri na kumfanyia ukaguzi mwali, ukisikia vigelegele ujue mwali yupo salama, ukiona kimya ujue MWALI KALOZA.Hivi sasa hilo ni jambo adimu.”

Ukisikie binti anaambiwa ,

“Utaniambia nini wewe, wakati mtu mwenyewe MWALI KALOZA.”

Hayo yalikuwa matusi makubwa sana wakati huo.



Jamaa hawa wakawa wanacheka sana, hapo hapo wakaagana na Mwanakwetu na kila mmoja kuchukua njia yake.

Kwa kuwa sherehe hii kama alivyoumwa sikio Mwanakwetu itafanyika Nyumbani kwa Mbunge  wa Chalinze ambaye ni mtoto wa Rais wa Awamu ya Nne wa wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mhe .Jakaya Kikwete, Mwanakwetu anaomba ayaseme maneno haya kwa mheshimwa Jakaya Kikwete.

“Chiza chee, Mose iwakulu mwilihano…

Hasa weye Kikwete,

Kulonda zina jako dilawe,

Mzukulu wake iyo ino hano,

Kahala dizina jako-da Kikwete,

Volelo,umlekese, yakale goya,

Umkuze, uakule kama mgobaandizi,

 Ubozi wako uleke wa kutesa iwana.

Upele uo na msele,

Mkagone kama vaagonile fungo,

Mose kama vaatendaga Mhango na Sagara, Wasawi na wafe! Na wage!

Mzimu naugone !-Naugone!”

Mwanakwetu upo?

Wakwere wote wa Chalinze nawatakia sherehe njema.

Msomaji wangu na wewe nakutakia siku njema.

makwadeladius@gmail.com

0717649257



0/Post a Comment/Comments