KRISIMASI INATUKUMBUSHA KUTIMIZA WAJIBU-PADRI MASANJA



Adeladius Makwega-MWANZA

Wakristo wameambiwa kuwa kuzaliwa Kwa Yesu Kristo kulikuwa na dhumuni la kuleta amani zaidi kwa mwanadamu ambalo ni tukio lililotokea miaka zaidi ya 2000 iliyopita , hivyo kwa sherehe ya Noeli kila mwanadamu anatakiwa kuwa na furaha zaidi na kujipanga upya huku kila mmoja kutimiza wajibu wake, maana mkombozi amezaliwa.

Hayo yamesemwa katika misa ya mkesha wa Noeli katika Mlima wa Hija, Disemba 24, 2023 kuamkia Disemba 25, 2023 kando ya viunga vya Parokia ya Malya, Jimbo Kuu Katoliki la Mwanza na Padri Samsoni Masanja ambaye ni Paroko wa Parokia hiyo .

“Furaha inayotakiwa na kupokelewa ni ya kuzaliwa Yesu Kristo na iwe katika mioyo yetu na furaha hiyo idhilike katika kila yeye anayesherekea sikukuu hii.”

Akiendelea kuhubiri katika misa hiyo Padri Masanja alisema kuwa Familia ya Yusufu, Maria na Yesu ni Familia Bora na siyo Bora Familia na ndiyo maana hii ni Familia Takatifu.

Usiku wa mkesha huu wa kuzaliwa kwa Yesu Kristo kila mmoja anawajibu wa kuiga mfano huo na kuwa na Familia Bora inayotimiza wajibu wa kila mwanafamilia.

“Katika injili ya leo tunaambiwa Yesu Kristo alipozaliwa tu alivishwa mavazi ya kitoto, maana yake wazazi wake walitimiza wajibu wao ipasavyo. Eee na wewe muumini unatimiza wajibu wako kwa familia yako ? Iwe katika mavazi, maladhi na chakula? Unakutana na mtoto amevaa vilaka huku tochi zinamulika, hilo halikubaliki na siyo mafundisho ya Ukristo, wakati baba/mama/ mlezi anavaa vizuri, huku watoto wakiwa na hali mbaya, jamani imani yetu inatufundisha kutimiza wajibu wetu ipasavyo, iwe kwa baba, mama na hata watoto.”

Akihubiri usiku huo, Padri huyu kijana aliweza kutoa mahubiri yaliyowaingia vizuri waamini wake, huku akichanganya Kiswahili na Kisukuma ambapo kwa hakika kila alipouliza swali iwe kwa Kiswahili au Kisukuma nao waamini walijibu kwa lugha iliyoulizwa.



Padri Masanja alisema kuwa mwaka mpya wa 2024 umekaribia, hivyo kama kuna mlei hajajipanga vizuri kwa mwaka kwa mwaka mpya ajipange sasa na kama hakufanya vizuri kiroho na kimwili kwa mwaka 2023 ajipange vizuri maana Sikukuu ya Noeli inatukumbusha kutimiza wajibu wetu maana Bwana Wetu Yesu Kristo amezaliwa.

Misa hiyo iliyoanza saa nne kamili ya usiku ilikamilika majira ya saa 9 usiku, huku watoto kadhaa wakibatizwa na ikuhudhuliwa na viongozi kadhaa wa Hija wa Jimbo Kuu Katoliki la Mwanza, Makatekista na walei, nayo historia ya kuingia Ukristo Tanzania ikisomwa, ambapo Mlima wa Hija hapa Malya Wamisionari wa kwanza walisali Krisimasi ya kwanza wakati Ukristo Ukatoliki ulipokuwa unaingia Jimbo Katoliki la Mwanza mwaka 1878.







0/Post a Comment/Comments