Adeladius Makwega–MWANZA
Mwanakwetu ana dada zake binamu kadhaa ambao wanazaliwa kutoka
kwa baba wa makabila mbalimbali, maana Mwanakwetu ni tajiri wa mashangazi, hata
akiamua kuwataja dada zake hao binamu katika makala mmoja baada ya mwingine ,
makala zitakuwa nyingi.
Mmoja wa binamu zake anayezaliwa na shangazi zake, anaitwa
Piensia Nyema, mara kadhaa amekuwa akitajwa katika makala za Mwanakwetu, kwa
tabia tangu utoto Piensia alikuwa binti mkimya mno, si muongeaji sana, mwenye machache
maneno na hata kama anaongea basi kwa yule anayempenda.
Hiyo ni haiba ya binamu huyo wa Mwanakwetu, katika ya miaka
kati ya 30 na 40 iliyopita,hiyo ni miaka mingi, msomaji wangu ni siku nyingi,haya
ni kwa mujibu wa shajara ya Mwanakwetu yanakufikia hapo ulipo.
Wakiwa wadogo ndugu hao, huyu Piensia alikuwa ni mpikaji
mzuri wa chakula hasa wali, kwa kuwa yalikuwa mazingira ya Pwani uungaji wa
vyakula ulikuwa ni wa nazi tu, nyakati hizo ulaji wa vyakula kwa mapishi yaliyoungwa
na mafuta ulikuwa mdogo sana kwa makabwela labda kwa mabepari waliweza kununua
makopo ya mafuta, mwendo ulikuwa nazi, machicha ya nazi na jalalani vifuu vya
nazi kibao.
“Wali wa Piensia Nyema ukipikwa ulikuwa hauwi ubwabwa, unakuwa
wali mzuri , huku punje za wali huo zikihesabika vizuri , moja baada ya
nyingine.”
Sifa hiyo ya mapishi hayo Mwanakwetu anakumbuka sana, maana
yeye ni Mpogoro, Mpogoro wali, sifa hii ilikuwa ya binamu pekee hapo nyumbani ,
yalipokuwa makazi ya Fidelis Makwega, babu wa Mwanakwetu.
Wengine hawakujaliwa hata kuisogelea sifa hiyo , yaani
upikaji huo mzuri wa wali, kwao hawa wengine ulikuwa ni mapishi mabaya na safari
ya mapishi mazuri na mabaya ilikuwa sawa na mbingu na ardhi.
Piensia alipopata dharura maneno yalikuwa mengi,
“Ubwabwa leo, utadhani wagonjwa wa Mwaisela.”
Msomaji wangu Mwaisela ni jina la wodi mojawapo maarufu
katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili jijini Dar es Salaam wakati huo hakuna
Mloganzila.
Piensia Nyema ambaye sasa ni mama wa watoto kadhaa, akikaribia
kujukuu, akiwa ni Afisa Utumishi Mwandamizi katiika Serikali ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, yeye alikuwa na sifa nyingine, wakati anapika alikuwa
kimya jikoni na sauti yake ilisikika tu chakula tayari mezani katika sinia,
“Jamani njooni mle.”
Palipakuliwa masinia mawili, moja la wanaume na moja
wanawake, sinia la wanaume lilikuwa na watu wachache hivyo baadhi ya wasichana
waliongeza nguvu ya kutupa mawe pangoni katika sinia la wanaume, ili kuwianisha
chakula cha sinia la wanawake na la wanaume. Hapa Piensia aliweza kupima kipimo
cha haki cha chakula hicho na kila mara yalisikika maneno haya,
“Jamaniee, hilo sinia lenye wanaumeongezeni chakula, wao
wanakula sana.”
Hapo sinia la wanaume
mezani, sinia la wanawake katika mkeka na waungwana walianza kula wali
unaohesabika punje uliopikwa na Piensia Nyema, binti wa Kingoni na Kipogoro.
Maswali yalikuwa mengi, inakuwaje mapishi ya Piensia Nyema ya
Wali mazuri kuliko ya wengine?
Kumbuka kwa Baba ni Mngoni Kwa Mama ni Mpogoro wa Mbagala. Wadau nyumbani wakisema,
“Piensia ni hodari wa kupika, hizo ni juhudi zake binafsi na
huyu ataolewa mapema.”
Hizo zilikuwa dua za kina Mwanakwetu
kwa binamu yao, mambo yakawa hivyo hivyo na alipomaliza chuo kikuu Mzumbe
aliolewa.
Ndiyo kusema dada wengine wa Mwanakwetu wakiwa jikoni hapo tulisikia
maneno mengi ,
“Haya leta chujio la nazi, leta chumvi, choteni maji, unga
umekwisha ”
Jikoni ukishaona Piensia hayupo, kumbuka hapo hautotoka
nyumbani hadi mapishi yakamilike,
“Miito hiyo itajirudi
mithili ya santuri iliyogoma kucheza usiku wa manane katika ukumbi wa muziki.”
Hawa binamu wote wa Mwanakwetu walikuwa na faida, siyo
Piensia peke yake, hawa waitaji wa kila mara walisaidia vijana wa kiume kuweza
kujifunza kiasi namna ya kupika , japokuwa walimu wenyewe walikuwa si wapikaji
wazuri, lakini walimtoa mtu kutoka hatua moja kwenda nyingine.
“Jamani mjifunze funze
hata kuchemsha chemsha, maana mkianza maisha yenu, mtafakamia mapishi ya watu,
mtalishwa na visivyolika. Hata wasichana nyinyi mjifunze funze shughuli za
akina baba kuna leo na kesho, unatakiwa kuokoa jahazi.”
Hawa mabigwa wa kuita walipata nguvu zaidi baada ya kusikia
Bi Getrude Mongella kaingia katika Mkutano wa Bejing’ mwaka 1995 sasa ikiwa ni
miaka 28 iliyopita tangu mkutano huo kufanyika nchini China.
Jamani mjifunze funze hata kuchemsha chemsha, maana mkianza maisha yenu,
mtafakamia mapishi ya watu, mtalishwa na visivyolika. Hata nyinyi mabinti
mjifunze shughuli za kina baba kuna leo na kesho unatakiwa kuokoa jahazi.
Haya Mwanakwetu anayakumbuka tu
maisha ya nyumbani kwao Mbagala miaka karibu 40 iliyopita yeye na ndugu zake.
Mwanakwetu siku ya leo anasema nini?
Mwanakwetu siku ya leo amekumbuka kisa
hicho cha dada zake nyumbani kwao, akiamini kwamba siyo kwamba Mkutano Beijng’
ulikuja na kitu kipya la hasha bali ulikuja kuipa nguvu mijadala ambayo ilikuwa
inajadiliwa na jamii, nyumbani, shuleni na katika maeneo mengine.
Huu Mkutano wa Beijing ‘ uliwapa
nguvu dada za Mwanakwetu waliokuwa wanapika wali vibaya lakini walitoa nafasi
ya vijana wa kiume kujifunza kupika angalau kuchemsha chemsha ili wasilishwe
limbwata/ litambulila baadaye wakiwa watu wazima.
Ndiyo kusema Mkutano wa Beijing’ pia ulisaidia
vijana wa kiume wa wakati huo kuwafahamu wanawake ni watu wa namna gani? Ulimwengu
wao una nini? Hata kuwalinda vijana hao kutoingia katika matatizo wanapokuwa
watu wazima ambayo mengine yanaweza hata kusababishwa na wanawake , kama ilivyo
baadhi ya wanaume wanavyoweza kusababisha shida kwa wanawake.
Popote ulipo Piensia Nyema, salaam
tele kutoka kwa nduguyo Mwanakwetu anakusalimia sana leo hii umesababisha
amkumbuke bi Getrude Mongella na Mkutano wa Beijing’,
“Piensia Nyema dada yangu, nakujulisha kuwa Noeli ya mwaka
huu hodi nyumbani kwako .”
Kwako Bi Getrude Mongella ,kwanza shikamoo ! popote
ulipo, tunashukuru kwa kutuwakilisha vema huko Beijing’ China wakati huo, Mwanakwetu
anauliza swali, ameona picha moja uliyopiga na Mummar Gaddaf inamtia mashaka na wivu kwa
urafiki wako na kiongozi huyu wa Libya ambaye ni marehemu , angeweza kumuuliza
Gaddaf lakini hayupo katika upeo ya macho yetu, tunakuuliza wewe bibi yetu mpendwa, tupe siri na hekima ya ujirani wako na kiongozi huyu, hadi kakuegemea? Bibi Gerude Mongella ,Je Jamhuri ilitoa kibali?
Mwanakwetu Upo?
Mama Mpogoro Mbagala
Nakutakia siku njema.
0717649257
Post a Comment