MAMA MWENYE KUBAZI KWAPANI

Adeladius Makwega-MAKOLE

Septemba 27, 2022 Mwanakwetu alikuwa nyumbani kwake Kijijini Chamwino Ikulu majira ya jioni sana, alibaini kuwa hakuwa na pesa ya kufanya matumizi mbalimbali nyumbani kwake, hilo likamlazimu atoke nyumbani kwenda benki iliyokuwa jirani katika ofisi na mkuu wa wilaya ya Chamwino.

Alitoka kwake kwa mguu hadi pahala pa kupanda bodaboda, alipofika hapo kwa kuwa alikuwa hana pesa yoyote mfukoni alimtafuta bodaboda anayemfahamu ili aweze kumbeba na hata akienda benki akikosa pesa isilete maneno na ugomvi, awe mwepesi kumuelewa. Kweli akiwa hapo bodaboda huyu anayemfahamu hakuwepo, alipompigia simu alimjibu anafika baada ya dakika kenda na zilipopita dakika hizo tisa alifika na kumpakia kuelekea ilipo benki hiyo.

Wakiwa njiani walikutana na mama mmoja akitembea kwa miguu nadhani akitokea Bugiri (Njia panda ya Chamwino Ikulu) kwenda Chamwino Ikulu huku akipachika kubazi lake moja kwapani na moja likiwa limevaliwa, hili la kwapani likiwa limekatika mikanda ikining’inia mithili ya pweza aliyevuliwa pwani ya Kilindoni Mafia.

Walimpita na wakasema labda mama huyu anaenda Chamwino Ikulu, umbali huu wa kilomita zinazokaribia 10 kwa mguu ni mwendo mrefu sana, zaidi ya saa moja, walimuonea huruma na kupishana naye kwenda zao benki.

Walipofika benki, kwa bahati nzuri alitoa pesa aliyoikuta na kumpa bodaboda huyu shilingi 10,000/- ili akate shilingi 3,000/- na akapakia kuanza safari ya kurudi kijijini Chamwino Ikulu.

Wakiwa wanarudi wakakutana na yule mama na kubazi lake kwapani, Mwanakwetu akamsihi bodaboda huyu anayefahamika kama Joseph, akisema tumbebe mama huyu ili tufike naye anapokwenda. Bodaboda alisimama kando ya mama huyu, akamsalimu, aliitikia, akauulizwa unakwenda Chamwino Ikulu? Akajibu ndiyo.

Akamuomba apakie nyuma ya Mwanakwetu ili kuepusha kumbahashia akiwa mbele yake akapanda na wakaendelea na safari.



Wakiwa safarini alimuuliza mama unaishi Chamwino Ikulu?Mama huyu  alijibu,

“Hapana, natokea Mwanza lakini nakwenda Ikulu ya Chamwino kwenda kumuona Rais Samia Suluhu Hassan, kwani huko ketu nimedhulumiwa ng’ombe zangu.”

Akamuuliza huku Mwanza walishindwa kukusaidia? Alijibu kuwa imeshindikana na ndiyo maana anakwenda kumuona Rais Samia..

Mwanakwetu akafika pahala pa kushuka na mama huyu akasema anashuka hapo hapo.

“Niliposhuka nikamuuliza mbona ulikuwa unatembea kwa miguu?”

Akajibu,

“Pesa yote nilitumia kwenye nauli kwa hiyo nimewaagiza wanangu wauze ng’ombe alafu pesa wanitumie nikiwa njiani, kwa hiyo nikichaji simu nitawasiliana nao ili niweze kupata fedha za matumizi na za nauli ya kurudi Mwanza nikishamuona rais.“

Kumbuka boda boda alipewa shilingi 10,000/- pale benki , akamwambia mpe mama huyu shilingi 3000/- atengeneze makubazi yake ni aibu kwenda Ikulu akiwa na Kubazi Kwapani.



Mama huyu akasema asante na huku akiomba tumuoneshe duka la dawa anunue dawa za kupunguza maumizi za shilingi 500/- akapewa noti ya 10,000/- akanunua dawa hizo  duka jirani na huku akiomba achajiwe simu yake ya tochi na akarudisha chenji kwa bodaboda.

Wakiwa naye pale mama huyu akaulizwa una hakika mheshimiwa rais yupo? Mama huyu akajibu  ndiyo , akisema alisikia katika redio yupo Dodoma na ndiyo maana amekuja kwa kushitukiza na pesa pungufu.

Nikamuelekeza ramani ya Chamwino ilivyo, Mwanakwetu akapewa pesa yake iliyobakia shilingi 4000/- akaenda zake kwake na yeye (mama huyu)akabaki anachaji simu na bodaboda akaendelea kuwasaka wateja wengine.

Baada ya siku moja Mwanakwetu akasafiri kwenda Zanzibar, huku akiambiwa kweli simu ya mama huyu ilipopata chaji alitumiwa pesa na kukaa Kijijini Chamwino Ikulu kwa siku kadhaa, bali haikufahamika kama mama huyu alimuona mheshimwa huyo au la, hilo Mwanakwetu hakujaliwa kulifahamu.

Siku ya leo anataka kusema nini?

 Wakati wa Utawala wa Mwalimu Julius Nyerere kumuona kiongozi huyu kidogo ilikuwa kazi kubwa sana lakini Rais Ali Hassani Mwinyi ukiweka kando yale anayoyalalamikiwa katika utawala wake, Rais Mwinyi alijitahidi mno kujenga ujirani wa Urais wake na Watanzania.

Mwanakwetu anakumbuka  aliona Rais Mwinyi alikuwa akisikiliza malalamiko ya wananchi mmoja mmoja kila baada ya muda fulani pale Ofisi Ndogo ya CCM Lumumba- Dar es Salaam na Watanzania walijaa kupeleka malalamiko yao.

“Nalikumbuka hilo kwa kuwa wakati huo mimi nilikuwa mwanafunzi wa shule ya Msingi Mnazi Mmoja inayotazamana na ofisi hii na huo ulikuwa wakati wa chama kushika hatamu.“

Rais John Magufuli akiwa hai alijitahidi sana kutoa nafasi ya mabango ambapo wananchi waliweza kunyanyua sauti zao, vilio vyao japokuwa si kweli kwamba yale yote yaliyokuwa mioyoni mwa Watanzania yaliweza kuandikwa katika mabango au yale mabango yote yaliruhusiwa kuonekana na kutatuliwa  kero hizo.

Wengine wakidhihaki yale yaliyolalamikiwa na Watanzania kwamba mengi yalikuwa si ya kweli katika mikutano hiyo. Labda yalikuwa ni ya mahakama na taasisi zingine.

Mwanakwetu Ifahamike wazi kuwa yawe ya kweli yawe ya uwongo, yawe yamefanyiwa kazi au laa wenye nchi yao walimwambia rais wao, sawa na baba/mama (mzazi) anapoambiwa jambo lolote na mwanae.



Hiyo ni haki ya mwana kwa mzazi wake. Mzazi ndiyo anawajibu wa kupima jambo hilo lifanyiwe kazi namna gani siyo mtu mwingine yoyote.

Hoja kubwa ni kwamba mtu anaweza akawa anamlalamkiia yule ambaye amepewa dhamana ya kusikiliza hayo malalamiko kiwilaya, kimkoa,kiwizara au kitaasisi yoyote ya umma  je inakuwaje? 

Kwa hiyo kwa hekima ili kusikia wenye nchi yao wanashinda gani ninashauri kinachoweza kufanyika kwa Rais, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu wanapokwenda pahala popote wanaweza kuwatangazia umma kuwa kesho rais/ makamu / waziri mkuu atapokea malalamiko ya mwananchi mmoja, uso kwa uso, bila bughuza yoyote ile kwa saa 5 kuanzia labda saa 2-7 mchana ndani ya ofisi ya mkoa, akishazungumza na mtu mmoja mmoja ndipo ufanyike mkutano wa hadhara.

Ili zoezi hilo liwe na haki na uwazi wasimamizi wa zoezi hilo wawe wasaidizi wa Rais.Makamu wa Rais au Waziri Mkuu wenyewe aliyotoka nao katika msafara wake makao makuu na wale watendaji wa vyombo vya mkoa husika wasiwabughuzi wananchi kwenda hapo na wasiulizwe wanakwenda kuongea nae nini kiongozi wao.

Mtoto anapokwenda kuongea na baba/mama yake haulizwi anakwenda kuzungumza naye nini na mjomba au shangazi.

Kwa sasa mikutano inafanyika sana lakini ina kasoro kubwa wanaopata nafasi ni  wakubwa tu na mikutano mingi mambo mengi yanatoka kutoka kwa wakubwa kwenda kwa wananchi huku wenye mkutano huo wanakuwa wasikilizaji wa hotuba tu.Hilo halikubaliki.

Kama litafanyika hivyo jambo hilo litasaidia mno kupunguza malalamiko mengi, mabango mengi ya moyoni na  safari ndefu kama za mama huyu niliyekutana naye na kubazi kwapani, akisafiri anaumwa, huku akiwa hana pesa za kutosha, akiuza ng’ombe wake nia amuone mheshimiwa.

Kwa sasa Rais Samia Suluhu Hassani mwenyewe anao nafasi ya kuchagua cha kufanya ili kuleta ujirani baina yake na wananchi anaowaongoza ili asije kusimuliwa kuwa alifunga milengo ya watu wa kawaida kuzungumza naye wakati wa utawala wake.


makwadeladius@gmail.com

0717649257

NB Kwa wale wapenzi wa lugha ya Kiswahili Fasaha wafahamu kuwa neno KUBAZI/KUBADHI yote ni maneno sahihi katika lugha hii.




0/Post a Comment/Comments