TUNABAKI KATIKA VIGODA VYETU

 



Adeladius Makwega-MWANZA

Mwanakwetu hadi sasa ameshafundisha katika hatua nne za elimu; Shule ya Msingi, Shule ya Sekondari, amesomesha Vyuo Vikuu na hatua nyingine ya Elimu anaendelea kuifanyia kazi ambayo leo hii haitaji.

Katika hatua hizo nne za elimu siku ya Disemba 22 kuamkia Disemba 23, 2023, Mwanakwetu alizikumbuka hatua mbili kwa namna ya kipekee sana, upekee huo ulimshangaza mno Mwanakwetu, hivyo anaamua kuyatayarisha makala haya kama heshima ya hatua hizo mbili za elimu.Mambo yalikuwa hivi, Mwanakwetu alilala na kuota ndoto moja,

“Watoto wadogo kama wa Chekechea au Shule ya Msingi wanacheza, mmojawapo alichimba shimo ambalo lilikuwa kama handaki lenye kina kifupi, alipomaliza akaingia wenyewe alafu akaulaza mwili wake vizuri t na akawa anaujaza udogo katika sehemu za mwili wake tangu miguuni hadi shingoni , hapo mikono yake inafanya kazi hiyo. akabakiza sehemu ya kichwa na mikono , alipomaliza hivyo akawa anaizamisha mikono yake katika handaki na kuanza na mkono wa kushoto na kumalizia mkono wa kuume.”

Taswira hiyo ni ya ndotoni usiku wa kuamkia Disemba 23, 2023 , Mwanakwetu ndotoni na kando ya harakati za mtoto mchimba handaki anaona haya,

“Watoto wadogo wenzake wapo katika makundi mawili wanacheza michezo yao, kundi la kwanza wanacheza KULA MBAKISHIE BABA na kundi la mwisho wanacheza BABA KASEMA.”

Taswira hizo tatu; MTOTO MCHIMBA HANDAKI, KULA MBAKISHIE BABA na BABA KASEMA Mwanakwetu aliziona kwa mara ya mwisho mwaka 2003 akiwa mwalimu wa Shule ya Kimataifa ya Dar es Salaam, akifundisha KISWAHILI, huku Mwanakwetu akiwakumbuka wanafunzi watatu wa shule hiyo wakati huo Daniel Kishimba(Grade 7) Susana(Grade 7), Masamba Masamba (Grade 4) na Upendo Kisai(Chekechei). Haya Mwanakwetu anayakumbuka sasa wakati anaandika makala haya.



Katika kundi hilo la wanafunzi wanne Kisimba, Susana, Masamba na Kisai , huyu Upendo Kisai alikuwa mtoto sana hawezi kumkumbuka Mwanakwetu lakini Kishimba, Susana na Masamba wanawasiliana sana na Mwanakwetu.

“Mr Makwega ulikuwa unapenda sana kusema , Msome , Msiposoma Mtafeli.”

Susana anamwambie Mwanakwetu kila mara akikutana naye.

Mwanakwetu ndotoni akamtazama yule mtoto mchimba handaki aliyejifukia kwa mchanga, akawauliza wale watoto, nyinyi vipi mbona mnamuacha mtoto mwenzenu anacheza mchezo huo hatari?

Huyu anacheza mchezo wa kufa , kesha kufa huyu achana nae.”

Mwanakwetu yupo ndotoni akasema kwa sauti,

“Nyie watoto acheni ujinga , hapo mnamchokoza jaji, hapo mnaichokoza mahakama atatufunga sote, ebu tumuokoa huyu mtoto haraka.”

Watoto hawa wakawa wanacheka, huku wakisema,

“Mzee watoto huwa hatufungwi , wanafungwa wakubwa tu.”

Mwanakwetu akajibu zipo mahakama za watoto, hapo hapo na wale watoto na Mwanakwetu wakaanza kufukua udongo aliyojikandika mtoto huyu, kumbe ule udongo ulikuwa sasa unaibua maji na maji yalikuwa yanakaribia katika shingo, hapo mtoto huyu kumbe alikuwa katika hali mbaya anahema vibaya , wenzake hawajui  wakidhani wakidhani mwezao anacheza.



Kazi ya kumuokoa mtoto huyu ilifanyika na kumtoa katika shimo lile, huyu bwana mdogo alipookolewa alichomoka mbio kukimbilia nyumbani kwao akiwa salama.

Kumbuka msomaji wangu hapo Mwanakwetu yupo ndotoni, akawaambia wale watoto wadogo msicheze michezo hatari.

Hapo Hapo gafla Mwanakwetu akashituka ndotoni, akashangazwa na ndoto ile hapo ndipo akakumbuka hatua zote alizosomesha maishani mwake.

Sasa Mwanakweu akamkumbuka mwanafunzii wake mmoja aliyemsomesha hatua ya Elimu ya Sekondari sasa ni mwanazuoni, bado kijana mdogo sana.Akamtafuta usiku huo huo, akazungumza naye, wakafanya tafsiri ya ndoto hiyo usiku wa manane , baadaye huyu msomi akamwambia Mwanakwetu maneno haya,

“Nyie Chama Cha Mapinduzi(CCM) mna shida kubwa, haya Mwalimu nakwambia uwaambie wanachama wenzako, nyie mnasema Anaupiga Mwingi wengine wanasema Anaupiga Mchache. Kama anaupigwa mwingi mbona wachezaji wachache? Ukipigwa mwingi wachezaji ni wengi.Mimi nawaambia 2025 kama wananihitaji kufanya nao kazi , pesa yangu waliniweke katika akaunti yangu mapema ndipo nitafanya nao kazi siyo kama nilivyofanya nao kazi 2020.”

Mwanakwetu akamwambia mwanafunzi wake, hata katika soka, huyu Mbwana Samatta akiupiga mwingi wachezaji ni 22 na refa na wasaidizi wake jumla kuu ni  25, wengine mnabaki watazamaji.

“Tunasikia mnasema Ooo Anatosha Sana, sawa anatosha  sana , hilo jambo zuri na nyinyi mshampima anatosha na sisi tupeni nafasi ya kupima kama anatosha au la. Ohh Mitano Tena, sawa mitano tena, lakini ipi mitano iliyopita au mitano ijayo”

Hapo Mwanakwetu anacheka kwa mazungumzo hayo na mwanafunzi wake, kumbuka yote haya yamekuja baada ya kuomba tafsiri ya ndoto.

“Mwalimu sisi tunashangaa kila mnapotoa mikeka yenu, wanaokuwemo katika mikeka hiyo, muda mfupi mikeka yao inachanika. Mtu anakaa kidogo mara mkeka umechanika. Mikeka mingine haichaniki, hivi sasa mkeka wa Daniel Chongolo umechanika. Mwalimu waambe mimi ninabaki katika KIGODA maana vigoda vyetu havichanikagi, nyie endeleeni na mikeka yenu.”

Mwanakwetu aliendelea kucheka kwa maneno hayo na baadaye kuagana na mwanafunzi wake huyo wa sekondari , huku kibindoni akiwa kwanza na tafsri ya ndoto ile ya wale watoto waliokuwa wanacheza na vicheko hivyo



Kumbuka tu msomaji wangu,

“Mikeka yenu inachanika, sisi tunabakia katika vigoda vyetu.”

Mwanakwetu Upo ?

Nakutakia Siku NJema.

makwadeladius@gmail.com

0717649257




0/Post a Comment/Comments