ASIYE NA MSIMAMO NDUMILA KUWILI


Adeladius Makwega-MWANZA

Tangu uteuzi wa Dkt Emmanuel Nchimbi kuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi, Mwanakwetu hakutaka kuandika chochote juu ya kiongozi huyu mahiri wa Tanzania ambaye amewahi kuwa Waziri katika Wizara kadhaa , Balozi na hata kuwa Mwenyekiti bora wa Umoja wa Vijana wa CCM Taifa UVCCM.

Lakini asubuhi ya Januari 18, 2024, macho ya Mwanakwetu yalishuhudia picha moja nzuri ikionesha mabalozi wawili yaani Balozi Hoyce Temu na Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi. Kwa Mwanakwetu hawa ndugu wote wawili ni viongozi anaowapenda kutoka moyoni, anawakubali , hivyo aliamua kukuza zaidi picha hiyo na kuwaona vizuri ndugu hao wawili.

Balozi Temu alivalia gauni lenye rangi ya kijivu -nyeusi likiwa na visanduku na kichwani kwake kavaa kilemba huku akiwa amefumbata mikono , fumbato hilo la mikono la Balozi Temu lilisindikizwa na tabasamu kubwa.

Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi ambaye sasa Mwanakwetu anamtambua kuwa ni Katibu Mkuu -Mwenyekiti, hilo jina nitalieleza baadaye, Katibu Mkuu.... Balozi Dkt Nchimbi amevalia shati jeupe lenye vidoti vidoti vyeusi na huku akivalia suruali nyeusi.

Alipoikuza zaidi picha hiyo Mwanakwetu aliona kuwa ahaa kumbe Katibu Mkuu- Mwenyekiti sasa nywele zake zina mvi. Nayo mazingira nyuma ya picha hiyo yalikuwa mazuri sana na yalipendeza mno machoni paa Mwanakwetu.



Chini ya Picha ukurasa huo wa Instagram wa Balozi Temu alimpongeza Balozi  Dkt. Emmanuel Nchimbi kuteuliwa kuwa katibu Mkuu.

Mwanakwetu alitiririka na maoni katika ukurasa huu na kuna jamaa mmoja anaitwa Masaweessau  yeye aliibuka akisema sasa chama cha nimoto alafu akaibuka mwingine kutoka huko alipo ndugu Ussiankhomawa,

“Pongezi nyingi sana kwa Balozi Dkt. Nchimbi, huu ni moja ya teuzi moto moto moto, Mungu wetu amsimamie.”

Mwanakwetu alipokuwa akiutazama ukurasa huu wa instagram wa Balozi Temu akakumbuka baadhi ya maneno ya ya awali ya Katibu Mkuu-Mwenyekiti Balozi Dkt Emmnauel Nchimbi aliyoyasemba punde alipoteuliwa tu .

“... Nafasi ya Katibu Mkuu wa chama chetu, siyo nafasi nyepesi na haina majukumu mepesi maana sisi ambao tumeanza kuifuatilia tangu inaanzishwa toka mwaka 1982 , tulipoamua kuachana na Katibu Mtendaji  na kuwa Katibu Mkuu wa Chama, maana awe mtendaji na mwanasiasa tumeipa uzito nafasi hii...

Kuna watu wengine wanasema Nchimbi kuna wakati mwingine ana misimamo hivi, eee ni kweli kwenye mambo ya msingi mimi nina misimamo na hili lazima tuelewane na kama mkitaka kunitimua kwa misimamo nitimueni leo ...eee kwenye mambo ya msingi lazima uwe na msimamo na ndiyo moja ya viapo vya chama chetu, MwanaCCM asiye na msimamo wewe ni ndumila kuwili, Undumila kuwili siyo sifa ya kuwa mwanaccm.

Nitasimulia hizo habari eee, mwaka 2005 eee.. mzee Mohahamed Gharibi Bilali alipokuwa anataka kugombea Urais wa Zanzibar, maana wakati ule tulikuwa na Rais wa Zanzibar Amani Abeid Karume, ameshamaliza temu moja anakwenda temu ya pili, alikuja kuniona kuniomba nimuunge mkono kugombea , ili yaani Amani Abeid Karume amalize temu moja aende zake off-course mimi napenda sana watu wenye akili, kwa hiyo Mohammed Bilali ni moja ya watu ninawaopenda sana , nilipata nafasi ya kuzungumza naye kwa kituo, wakati huo nilikuwa na miaka 34 nikamwambia mzee... maana alinieleza anachotaka kuifanyia Zanzibar yaani unasisimka akieleza, nikamwambia ukweli nimesisimka na maelezo yako lakini siyo utamaduni wetu, ni kweli nimesisimka lakini siyo utamaduni wetu, tukikupa temu moja tunakuacha unamalizia ya pili kwenye nafasi ya urais. Sasa nimesema mapema ili tusije tukaelewana vibaya baadaye eee... CCCM- CCM-CCM-CCM...”

Mwanakwetu yupo katika ukurasa wa Instagramm wa Balozi Temu na picha yake hiyo juu ilimkumbusha maelezo hayo juu ya Balozi Dkt Emmanuel Nchimbi Katibu Mkuu mpya wa CCM Taifa.




Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?

“Katika hilo la tusije kuelewana vibaya Katibu Mkuu wangu Balozi Dkt Emmanuel Nchimbi nimekuelewa vizuri na hatutaki kugombana na wewe.”

Mwisho Mwanakwetu anasema kuwa Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi tunakuita Katibu Mkuu - Mwenyekiti kwa kuwa wewe uliwahi kuwa mwenyekiti wetu wa UVCCM, kwa hiyo hatuwezi kukupokonya nyota yako ile ya Uenyekiti wa UVCCM wa wakati ule , japokuwa sasa una mvi , nyota ile itabakia pale pale ilipo.



Mwanakwetu Upo

Kumbuka tu mwanaccm asiye na msimamo ni ndumila kuwili

Nakutakia siku Njema.

makwadeladius@gmail.com

0717649257





0/Post a Comment/Comments