HUNA MAMA HUNA



Adeladius Makwega-TANGA

Januari 10, 2024 Mwanakwetu alitumia muda wake mwingi kutembelea maktaba ya familia yake ambayo ina mkusanyiko wa nyaraka nyingi  ambazo kwa hakika zimehifadhiwa vizuri, ndani yake zipo barua mbalimbali zilizowahi kuandikwa na wanafamilia, zipo picha, kadi za kiliniki, vyeti vya kuzaliwa, mitihani , ripoti za shule, barua za posa,vyeti vya ndoa, vyeti vya ubatizo, madaftari na shajara kadhaa tangu mwaka 1938.

Kwa hakika unapoingia katika nyaraka hizo mara nyingi anayeingia huko hutekwa na mtu ambaye yu jirani naye kidamu, ambalo hilo halina ubishi, hata Mwanakwetu lilimkumba.

Mwanakwetu alivutiwa na taarifa za watu wawili , mmoja yu hai mwingine ni marehemu, jamaa hao wawili ni Mwalimu Francis Makwega na Mwalimu Doroth Hezron Mlemeta, ambapo aliyehifadhi alimtambulisha kama Mwalimu Doroth Makwega, hao ndugu wawili ni wazazi wa Mwanakwetu yaani baba na mama.

Mwanakwetu alitazama picha nyingi za mama yake na mwisho alivutiwa na mwandiko wa mama mzazi yake alivyokuwa akiumba herufi.

Kwa kuwa huyu mama alishafariki, Mwanakwetu alihitaji kuwalingishia watoto wake namna mama yake alivyokuwa akiandika.

Je mama huyu alikuwa na mwandiko mzuri kuliko wajukuu zake?

Kweli Mwanakwetu alikutana na shajara ya mwisho mwisho wakati wa uhai wa huyu mama ambayo ilikuwa ya rangi bluu, ililiwa na panya kidogo, lakini panya hao hawakuweza kuitafuna yote maana ilikuwa na gamba gumu.

Usalama wa shajara hiyo ulikuja baada ya kupatikana muda mfupi baada ya mwalimu huyu kufariki dunia miaka 22 iliyopita na hapo ndipo shajara hiyo ikabaki kuwa salama na kuhifadhiwa , hadi sasa Mwanakwetu anaifungua na kuisoma.

Hapo Mwanakwetu akakutana na kipande cha shairi lililopewa jina HUNA likiwa na bei tatu kama unavyoliona na mama huyu kaandika kwa mkono wake mwenyewe, Mwanakwetu akasoma alafu akacheka sana, hasahasa neno AMBI ikimanaanisha kitu cha urembo wapakacho akina mama, kama piko kuongeza urembo, hivi sasa ni maarufu mno , bi harusi hawezi kuolewa hadi apake AMBI.

Mwanakwetu akaendelea kuipekua shajara hii ya mama yake akakutana na kurasa moja imeandikwa kwa wino mwekundu.



Hapo kunaonekana masuala ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2000 Ikieleza idadi ya vituo va kupiga kura-Jimbo la Ilala vilikuwa 265 na Jimbo la Ukonga Vituo 719 jumla kuu kwa majimbo mawili ya wilaya ya Ilala ilikuwa na vituo 982 , mwisho akaandika watu 4000, hiyo  idadi 4000 haikufafanuliwa kama ilikuwa ni idadi ya wasimamizi au nini?

Mwanakwetu akaendelea kupekua shajara hiyo akakutana na karatasi nyingine ikiwa na maandishi ya Masharti ya Usimamizi wa Uchaguzi.

Katika kurasa hizo tatu tangu hii ya Masharti ya Usimamizi wa uchaguzi ,Idadi ya Vituo vya Kupiga Kura na shairi la Huna , hayo mambo matatu yalimpa tafakari kubwa Mwanakwetu karibu usiku mzima, akijiuliza ilikuwaje mama yake aliandika haya mambo katika shajara yake ambayo leo hii miaka karibu 24?



Kwa hakika Mwanakwetu hakupata majibu

Mwanakwetu alikula chakula cha usiku huo na kulala vizuri, kulipokucha tu alifungua simu yake ya kiganjani gafla alikutana na video katika ukurasa wa Bibi Helen Kijo Bisimba ukiwa na akina wakilalamikia madhaifu ya viongozi wetu.

“Hata mkisema tukapige kura ,mnadhani tuna hamu tena ya kupiga kura? Wakisema tupige kura hatuna hamu kweli. Naamka saa kumi na mbili nasema napigia kura watoto, wajukuu wangu waje wanisaidie, sasa sioni hata hiyo faida ya kuamka asubuhi, sasa ninaamka kwenda kufanya nini?”

Mwanakwetu alipowatazama akina mama hao aliwalinganisha sawa sawa na mama yake mzazi kama angekuwa hai.Hapo hapo Mwanakwetu akakumbuka yale mambo matatu katika shajara ya mama yake, ubeti wa shairi,vituo vya kupiga kura na masharti ya usimamizi.

Mwanakwetu akasema,

“Mama yangu alikuwa anashiriki uchaguzi kama Msimamizi wa Uchaguzi .”

Mwanakwetu akasema moyoni,

“Akina mama sasa wamekata tama, Rais wa sasa wa Tanzania ambaye ni mwanamke anatakiwa afahamu kuwa Watanzania wamekata tamaa sana na hawana hata hamu ya kupiga kura.Jukumu la Rais wa sasa wa Tanzania anatakiwa kutambua kuwa anayo kazi ya kurejesha miiyo ya watu waliokata tamaa kama akina mama hawa.Rais Samia anatakiwa kuweka viungo katika mioyo ya Watanzania ili wawe na hamu ya kupiga kura . Kubwa CCM waache kuishi kimazoea kama walivyoishi zamani, maana kama walizoea kupika chakula chuku chuku alafu kikaliwa basi sasa wakifanya hivyo watapata tabu.”

 

Mwanakwetu akaendelea kusema moyoni,

“Kwa kuwa Rais wa sasa wa Tanzania ni mwanamke na ni mama anatakiwa kila anachopika kisiende jamvini kuliwa bila ya kuwekewa viungo, kwa kuwa rais wa sasa ni Mzanzibari, siri ya wanawake wa Zanzibari ni kupika kwa kutumia viungo vingi hilo hapaswi kuachana nalo hata mara moja.”

Mwanakwetu akataja maana ya kupika chakula chukuchuku,

“Ni kuishi kwa CCM kama ilivyokuwa ikiishi zamani, dhana mojawapo ya kupika chukuchuku sasa CCM inasema fomu ya Mgombea wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ndani ya CCM itakuwa moja. Huku ni kupika chakula chukuchuku na kukiacha kiliwe. CCM iweke viungo vingine kwa ruhusu watu tofauti waingie kilingeni, hilo pekee litaongeza ladha na hamu ya Watanzania kupiga kura.”

Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?

“Rais Samia awaambie hao wanaotaka mgombea mmoja fomu moja, kuwa yeye ni Mzanzibari chakula chake lazima kiwe na viungo ili kinoge.”

CCM ya samia isipofanya hivyo itakuwa inapika chakula chukuchuku na chakula hicho kitakuwa hakinong.



Hapo Rais Samia atakuwa hana cha kulingia na mwisho wake utakuwa mbaya kama lilivyo shairi kutoka shajara ya mama yake Mwanakwetu.

Mwanakwetu upo?

Kumbuka Huna Mama Huna na Usikubali Chukuchuku.

Nakutakia siku Njema.

makwadeladius@gmail.com

0717649257




0/Post a Comment/Comments