JE DKT TAX SANTURI TUPU INAYOCHEZWA STUDIONI?

 



Adeladius Makwega-MWANZA

Nakuomba msomaji wangu siku ya leo nitumie dhana moja maarufu ya Kuweka Rekodi katika makala haya ikiwa ni lugha ya picha inayojikita katika kadhia ile ile ya Chuo KIkuu cha Dodoma.

Katika vyombo vya habarii utasikia mwanariadha fulani ameweka rekodi ya kukimbia kwa kasi umbali wa mita kadhaa kwa muda kadhaa, huku ikitajwa rekodi ya awali na aliyeiweka. Katika dhana hii nakuomba msomaji wangu nijaribu kukupa picha ya redio mbalimbali duniani  zinavyofanya kazi wakati wa kuweka rekodi ambapo rekodi wakati mwingine inaitwa Santuri / Senturi.

Nakuomba msomaji wangu nikupe picha ya redio tatu ambazo Mwanakwetu amewahi kufanyia kazi.

Mosi, Redio Country FM ya Iringa Mjini ,

“Hapa wakati huo walikuwa na studio ambapo Mtangaziji anatangaza katika chumba kimoja huku yeye pia akicheza rekodi za kipindi chake. Hapa kazi zote mbili zinafanyika katika chumba kimoja na mtu mmoja. Kwa hiyo ukiingia studioni unakutana na mtangazaji ambaye pia ndiye mchezaji wa senturi, hawa jamaa walikuwa na watangazaji maarufu sana kama Mahija Zayumba, Rose Majani na Temmy Mahondo.”

Pili , TBC /TAFA hawa ndiyo wale waliokuwa REDIO TANZANIA DAR ES SALAAM(RTD)- hawa ni wakongwe wa kuchanja mbuga za Tanganyika.

“Hawa jamaa wanastudio kadhaa zinarusha matangazo, wanayo ile ye TBC TAIFA , TBC FM , STUDIO ONE wanayo ya studio ya UKOMBOZI na studio ya Mshikamano, studio ya Mikocheni na kila kwenye kanda zao mikoani wanazo studio zenye majina kadhaa ya kizalendo. Hawa jamaa wale wazee wao wa zamani wale  wa RTD walijua kuyachagua majina, hapa Mwanakwetu anatoa heko kwa wazee wa RTD ambao wengi ni marehemu.

Namna wanavyofanya kazi huwa unapoingia studio mathalani ya TBC TAIFA ukifungua mlango, unakutana na vyumba viwili , hiki ulichukatana nacho cha kwanza anakuwapo Injinia / Fundi Mitambo. Hapa unakutana na maainjinia kama Omari Salum, Joseph Masanja na Moshi Silanda zamani walikuwepo akina Crispin Lugonga.

Hapo hapo chumba cha kwanza kunakuwa kioo kigumu sana kwa mbali utaona mtu chumba pili, hapo anakuwepo mtangazaji/ mtayarishaiji wa kipindi. Hapa Mtangazaji/ Mtayarishaji vipindi kwa chumba cha pili yeye anatangaza tu na huyu Injinia / Fundi Mitambo chumba cha kwanza yeye kazi kubwa ni kusimamia mashine za mitambo hapo studioni na mawasiliano katika minara kama matangazo yapo hewani na pia kazi nyingine ni kucheza senturi mbalimbali kama zinavyoelekezwa na mtangazaji / mtayarishaji w a vipindi.”

Tatu, DW KISWAHILI pale Bonn Ujerumani, hawa  jamaa mambo yao yako vizuri,

“Hawa jamaa wanastudio bora sana na za kisasa mno, wana studio nyingi kwa idhaa zote. Kuna studio zile za kurekodia vipindi na ile ya moja kurusha taaarifa za habari hewani. Hizi studio za kurekodia vipindi zenyewe unaingia ukiwasha mitambo ya kompyuta unarekodi, hapa kazi unafanya mwenyewe.

Hii studio kubwa ya kurusha matangazo hewani yenyewe unapoingia unakaribisha na chumba kikubwa sana na chumba kimoja kidogo. Chumba kikubwa anakuwepo injinia mmoja, DW Kiswahili wanaye injinia mmoja mrembo sana , dada mmoja wa Kijerumani anaitwa Nina Markgraf, mrenbo mno, Mwanakwetu hajawai kumuona dada mzungu mrembo kama huyo tena  maishani mwake yaani Nina Markgraf.

Injinia Nina Markgraf alikuwa anajua Kiswahili kidogo lakini walikuwepo wengi hawajui Kiswahili kabisa lakini waliweza kufanya kazi vizuri na DW KISWAHILI.

Chumba cha pli kilikuwa na kioo kikubwa na unamuona Mtangazaji, huku akishirikiana vizuri na Injinia Nina Markgraf, huku akicheza vizuri santuri zote bila hata ya kukosea.”

Mwanakwetu anatambua Waswahili wanapenda nongwa sana

“Ohh ukimuona mtu anasifia mvua ujue imenyea, mbona Mwanakwetu anamsifia sana Nina Markgraf”

Jamani huyu dada ni mrembo sana wapigieni simu ndugu zenu Wakitazania hasa hasa kaka zenu walipoo huko watawapa majibu hayo juu ya Nina Markgraf.

Mara nyingi katika redio vipindi/ taarifa zinapokwenda hewani huwa kunakuwa na makosa yanayofanyika studioni au pengine rekodi iliyopangwa inaweza kugoma kucheza, Mtangazaji anaweza kusema tunaanza na taarifa huko Kongo kinachocheza kikawa kutoka KUBA (CUBA).Hapa pale redioni mnatambua mmekosea na  wasikilizaji wenu watatambua mmekosea, hamna budi kuomba radhi.

“Samahani msikilizaji wangu, tulikuwa tunataka kwenda Kongo lakini taarifa hiyo haiko tayari na sasa twende KUBA.”

Hii ni kazi ya watu, wewe umekosea na unatambua hilo na jamii inatambua hilo lazima kuomba msamaha hapo hapo, hakuna kungoja. Muda mwingine unaweza kuweka rekodi ikacheza alafu ikawa haina kitu, hapo mwendo ni ule unaomba msamaha unaitoa rekodi tupu unaweka rekodi yenye kitu.

Msomaji wangu nadhani tupo pamoja tangu kule Iringa kwa Temmy Mahondo ,TBC Dar es Salam kwa injnia Omari Salum na DW KISWAHIL BONN kwa mrembo Injinia Nina Markgraf.

“Hoja ya msingi siyo kuweka rekodi tu bali weka rekodi yenye kitu.”

Hizo redio tatu Country FM Iringa, TBC TAIFA Dar es Salaam  na DW KISWAHILI BONN zote zinatangaza kwa Kiswahili na redio mbili zinatumia mainjinia lakini redio moja mtangazaji anafanya kila kitu.

Hawa DW KISWAHILI mara nyingi mainjinia wao huwa ni Wajerumani na wanacheza rekodi katika Idhaa ya Kiswahili bila ya kufahamu Kiswahili na hawezi kukosea hata mara moja, maana mifumo yao ipo vizuri na mtu yoyote akielekezwa anaweza kuifanya kazi hiyo vizuri hata katika studio za Kichina, Kihausa, Kiingereza na hata Lugha zingine za hapo hapo DW.

Mwanakwetu siku ya leo anasema nini?

Mwanakwetu bado yupo katika kadhia ya Chuo Kikuu cha Dodoma, unaweza kumchukua mtu ambaye amezoea kufanya kazi katika eneo lenye mifumo bora, hawezi kufanya kazi vizuri katika eneo ambalo halina mifumo mizuri, linalohitaji ufuatiliaji wa kina. Mifumo huwa inahitaji mambo yaende kama yalivyo na kama yalivyopangwa lakini katika Tanzania yetu hali haiko hivyo inahitaji ufuatiliaji wa kila hatua kwa hatua na ndiyo maana akina Karl Peters walifuatilia mambo yao mguu kwa mguu.

Unamchukua mjuzi ukiwa dhana ya kuja kuweka rekodi na mwenyewe anajua mimi naweka rekodi, jiulize hiyo rekodi iliyokwe inanini nini, siyo rekodi tupu?

Unaposikia kutoka kwa wasikiiizaji kuwa rekodi hiyo uliyoweka ni tupu, jitahidi kutafuta rekodi iliyo kitu ichezwe.



Nakuomba msomaji wangu utazame mfano huu na hili ni la Profesa Lughano Kusiluka na msomaji wangu utaamua mwenyewe kama rekodi hii tupu au rekodi ina kitu?

“Kuna wakati Chuo Kikuu Dodoma kilitangaza nafasi za masomo katika kozi ya moja nishari fulani, kawa bahati mwombaji alijitokeza alikuwa mmoja kutoka taifa moja jirani, akafika na kuanza masomo haya. Masomo yalipoanza ikabainika ni hasara kuendelea kozi hiyo ikiwa na mwanafunzi mmoja. Huyu kijana akaombwa wamuhamishie chuo kingine. Kijana akagoma akijibu hapo nilipo ndipo mfadhili anapopafahamu, huko mimi siendi.

Mazungumzo ya kumshawishi mwanachuo huyo ahamishwe yaliendelea, akagoma lakini akawajulisha wanaomlipia ada na wao wakagoma.

Mjadala huu unaojadiliwa na mwanachuo mgeni, hiyo inatoa picha mbya ya taifa letu mbele ya wageni tunaonekna wababaishaji. Basi likipokea nauli ya habari hata mmoja lazima liendelee na safari. Kijana huyu anaendelea na masomo.

 Kama nyinyi wenyewe mmefanya udahili; iwe TCU au iwe UDOM mnaona mwombaji ni mmoja mnawashawishi watoto wa Kitanzania hata 10 wasome bure wanane kutoka bara na wawili kutoka Zanzibar mchezo unakwisha na yale madhaifu yetu yanafichwa.”

Profeaa Lughano Kusiluka kama Makamu Mkuu wa chuo, wewe ni balozi wetu chuoni hapo kwa wanachuo na wahadhri kutoka mataifa mengine, usipokuwa balozi mzuri basi wewe ni santuri inacheza studioni lakini tupu.

Tuje kwa Dkt Stergomena Lawrence Tax, Juni 7, 2022 akifungua semina huko Dar es Salaam kuhusu A Agenda ya Wanawake , Amani na Usalama(Women, Peace and Security Agenda) kama Dkt Tax hakumbuki atazame shajara yake. Nadhani wakati huo Dkt Tax alikuwa ndiye Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa wa taifa letu, akiwa ukumbini alinukuliwa akiyasema maneno haya,

“ ... majukumu la wanawake wakati wa migogoro na katika kuleta amani yanatafautiana. Hilo pia ni suala gumu, hivyo basi Tanzania inahitaji ushirikiswaji wa wanawake katika masuala ya amani na usalama...”

Haya yanasema na huyu msomi ambaye sasa ndiye MKuu wa Chuo KIkuu cha Dodoma , malalamiko ya wanachuo katika taasisi yako  mengi ni ya wanawake,.



Huo ni mgogoro akina mama wanateseka je  Dkt Tax umeshawahi kuchukua hatua zozoze? Hata kuzungumza nao? Kumbuka maneno yako haya.

“...hivyo basi Tanzania inahitaji ushirikiswaji wa wanawake katika masuala ya amani na usalama...”

Mwanakwetu anasema kama Dkt Tax alishaongea na wanachuo wenye malalamiko hayo bila kujali jinsi zao hapo utakuwa umefanya jambo zuri  na hongera sana lakini kama haujafanya hivyo wewe ni sawa tu na santuri tupu inacheza studioni.

Mwanakwetu anaomba kwa leo aishie hapo, akisisitiza kuwa Profesa Lughano Kusiluka aondolewa kwa manufaa ya umma nayeye Dkt Stergemena Tax afungashe virago vyake UDOM na kwa hisani tu akabakiziwe hayo majukumu yake ya kisiasa hadi 2025.

Mwanakwetu Upo?

Santuri Tupu Inayocheza Studioni

Nakutakia Siku Siku Njema

makwadeladius@gmail.com

0717649257




0/Post a Comment/Comments