Adeladius Makwega-MWANZA
Msomaji wangu kwa heshima na taadhima, itazame hiyo picha vizuri,
kwa hakika mheshimwa Spika wa Bunge letu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
anaonekana akiwa na ndugu mmoja ambaye amevalia suti ya rangi ya samawati.
Kwa utafiti wa Mwanakwetu umebaini kuwa picha hiyo ilipigwa
nchini Tanzania na ilipatikana katika maktaba ya Mwanakwetu lakini haifahamiki picha
hiyo ilifikaje katika maktaba hiyo.
Ukiwatazama hao ndugu vizuri, Spika wa Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania anaonekana kucheka na huyu jamaa mwenye suti ya rangi ya
samawati akicheka pia.
Baada ya Mwanakwetu kufuatilia sana ilibainika kuwa picha
hiyo ilipigwa na Mbunge wa Mlalo mhe Rashidi Shangazi ambapo mhe Spika wa Bunge
la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akiwa Naibu Spika alipotembelea Jimbo la Mlalo,
mkoani Tanga mwaka 2018.
Mwanakwetu alitamani kumfahamu aliyekuwa kando ya Spika Tulia,
alimfahamu vizuri na alipotaka kufahamu maneno yaliyosemwa na ya kumchekesha
mhe Dkt Tulia siku hiyo yalikuwa yepi?
Majibu yalkuwa haya , huyu jamaa mwenye Suti ya rangi ya
samawati alimwaga mtama huo kwa Mwanakwetu.
“Sasa mheshimiwa Dkt
Tulia, itabidi nichukue kigoda ili nilingane urefu na wewe, alafu
nikawalingishie kwetu machakani kuwa leo hii nimepiga picha na spika na ninalingana
naye urefu.”
Habari za Kuongeza Kigoda pia
zilimchekesha Mwanakwetu, ukiitazama picha hiyo vizuri hao ndugu wawili wote wanacheka,
wote weusi, wote hao ni Watanzania waliozaliwa
baada ya muungano wa Tanganyika na Zanzibar.Ukiitazama zaidi picha hii
utaona kuwa Dkt Tulia na huyu jamaa wote wamefumbata mikono na mkono wa kulia
juu na wa shoto ukitangulia.
Ukimtazama tena mhe Spika wetu kapiga gauni maridadi la kitenge,
refu hadi chini, siku hizi mheshimwa spika haya mambo ameyaweka kando, yapo likizo
kidogo, lakini katika hilo Mwanakwetu asijifanye anajua sana, watu watasema,
“Wewe Mwanakwetu, huko
machakani Kwimba-Mwanza unamuona lini na wapi Spika wetu Dkt Tulia?”
Hivi kweli kujua hilo ni kazi ngumu? Hiyo ni kazi nyepesi tu,
itabidi nimpigie simu Mbunge wa Kiteto, Mr Edward Ole Lekaita au Mbunge wa Malinyi
Mhe. Antipas Zeno Mngungusi niwaulize.
“Kaka naomba mapigo ya Dkt Tulia
mwezi huu yalikuwaje.”
Sasa waheshimiwa hao wakiuliza Mwanakwetu katika hayo mapigo
ya Spika unataka nini? Nitawajibu nini mie Mwanakwetu?
Majibu yatakuwepo tu.
“Mimi mwandishi wa habari,
nataka kumuandikia makala ya mavazi yake mh wetu, hapo mchezo umekwisha.”
Katika picha hiyo ukitazama vizuri huyu jamaa mwenye suti ya samawati
kazidiwa urefu na Dkt Tulia na ndiyo maana jamaa aliomba kigoda ili alingane na
mh Dkt Tulia. Jamaa kando ya Dkt Tulia
husuda hiyo ilimjia na aliweza kuisema kwa mhe siku hiyo.
Mwanakwetu alipoitazama picha hiyo tena
na tena ilimjia picha ya Mr II -Josephy Mbilinyi ambaye aliwahi kuwa Mbunge wa
Mbeya Mjini, ambaye Mwanakwetu anamfahamu kwa karibu tangu anaanza muziki wake
akiwa kijana mdogo, aliwahi kuishi Mbagala na akifanya kazi ya ubawabu British
Petroleum (BP) Kurasini, hizo ni habari za walikuwapo Dar es Salaam wakati huo
tu.
Mwanakwetu alikumbuka kuwa Mr II
alikuwa kijana mzuri, kosa ambalo akina Mwanakwetu walifanya kutomuozesha Mr
II, kwa hakika angekuwa sasa shemeji yao watu Mbagala , tungekuwa tunagawana
naye mirabaha
sijui mirahaba ya nyimbo zake, lakini watu wa Mbagala waliweka mitego
mingi ya Ndoa za Mkeka lakini akina Mwanakwetu walishindwa kuongeza
juhudi katika hilo, sasa hivi lazima tujilaumu.
Kumbuka msomaji wangu kama nilivyokwambia
hapo juu hizi ni habari za waliokuwapo Dar es Salaam wakati huo.
Picha hiyo hapo juu ikambeba mzega
mzega Mwanakwetu hadi mwaka 2025 Mbeya Mjini, mambo yatakuwaje wakati wa
uchaguzi mkuu?
“Mwanakwetu hakuwa na
majibu maana hao wote ni nduguze.”
Mwanakwetu siku ya leo anasema nini?
Huyu Sugu je ataweza kuutumia ule Ujanja
wa Mjini / Ujanja wa Da es Salaam alivyoweza kupenyepenya na kuibuka kinara wa
muziki wake hadi Wazaramo/ Wandengereko akina Mwanakwetu walivyomkosakosa na ndoa
za mkeka za dada zao? Je Utamsaidia kushinda ubunge?
Au mambo kwa Dkt Tulia yatakuwa kama hii
picha inayoonekana kuwa unapotaka kumfikia Dkt Tulia kwanza una kazi ya
kukitafuta kigonda cha kulingana naye, ukishamaliza kazi hivyo ndiyo uanze
harakati za kumvuka, nayo ni kazi nzito! Kama huyu baba mwenye suti ya samawati
alivyoshindwa akabakia na kicheko?.
Mwaka 2025 si mbali; mwaka, miezi,
juma, siku ,saa , dakika na sekundu zinasonga kidogo kidogo, tungoje muda
uamue.
“Mwanakwetu anatambua
MR II ni nduguye na Dkt Tulia ni dada yake. Sisi sote ni Watanzania, lazima
tuijenge nchi yetu viwavyo na iwe.”
Mwanakwetu Upo?
“2025 si mbali Je ni Ndoa za Mkeka au Sogeza Kigoda, Mwanakwetu
anasema Muamuzi ni Muda.”
Nakutakia siku Njema.
makwadeladius@gmail.com
0717649257
Post a Comment