Adeladius Makwega-MWANZA
Msomaji wangu natambua uu mzima, hapo ulipo, ukiendelea na majukumu yako ya kila siku, kama ulivyojaliwa na Mungu. Kwa upande wa Mwanakwetu ni mzima huku akimshukuru Mungu kwa uzima huo.
Kwa hakika msomaji wangu tambua kuwa kama binadamu changamoto ni sehemu ya maisha yetu, ukiona wewe una changamoto tambua bado upo hai, ukiona hauna changamoto tambua kuwa siku zako za kuishi zimekwisha.
Msomaji wangu nakuomba nikichukue hapo ulipo siku ya leo nikurudishe nyuma kidogo Disemba 31, 2023, siku hii Mwanakwetu aliitumia kikamilifu kutembelea maktaba yake ambayo imesheheni vitu vingi vizuri vya zamani vyenye simulizi tele.
Mwanakwetu alifungua masanduku kadhaa ya chuma, ambayo alikuwa hajayafungua tangu Mei 2019 yalipofungwa wakati anaondoka Vwawa–Mbozi mkoani Songwe.
Sanduku moja ya chuma ambalo kufuli yake ilikuwa ngumu kufunguka, Mwanakweru aliomba msaada kwa binti yake mwenye nguvu na kusaidia kuivunja. Zoezi hilo lilipokamilika alilifungua sanduku lake na kukutana na mapazi kadhaa ambayo yalikuwa yakitumika katika madirisha ya nyumba hiyo aliyokuwa akiishi ambayo ilikuwa madirisha makubwa.
Sanduku hilo ni kubwa ambalo kwa uzito linaweza kubeba mzigo unakaribia nusu tani, ndani yake yalikuwa mapazia makubwa 20 ya rangi ya kijivu. Mwanakwetu akayatoa mapazi hayo vizuri na kubaini kuwa chini ya sanduku hilo kuna flemu kumi za picha mbalimbali ambazo zilikuwa zinawekwa sebuleni hapo Vwawa Mbozi . Kwa hiyo yule aliyeyaanua mapazia madirishani alianua na picha ukutani na kuziweka katika sanduku moja pamoja, ambalo Disemba 31, 2023 Mwanakwetu analifungua kwa mara ya kwanza, miaka minne baadaye.
Mapazia hayo yaliotengezewa yalikuwa salama kabisa na sasa alizifikia flemu zenye picha, hapo Mwanakwetu alibaini safari ya kutoka Vwawa hadi Lushoto ya Lori lililobeba mizigo ilikuwa ngumu hivyo flemu kadhaa ziliharibika na vioo vilivyunjika kabisa na picha kuharibika , uharibifu huo ukitafautiana.
Miongoni mwao katika picha iliyopata itilafu ilikuwa hiyo hapo juu hapo, Mwanakwetu aliwatambua baba mmoja mwenye nywele nyingi yu na watu wengine wanne. Watu hapo ni Hamisi Holela (Mdigo) kushoto, Adeladius Makwega(Mpogolo), Farida Hamisi(Msukuma) mwenye hijabu na Angela Mndugu(Mpare) mwenye blauzi ya samawati.
Mwanakwetu alikumbuka kuwa picha hiyo ilipigwa chumba cha Habari cha TBC Taifa Barabara Nyerere Jumatatu ya Julai 13, 2015 na aliyepiga picha hiyo ni Batlet John Milanzi(Mmakonde).
Hao wote hadi mpiga picha walikuwa watangazaji wa TBC Taifa na TBC International wakati huo, isipokuwa huyu mwenye nywele nyingi ambaye alikuwa mgeni wao.
Huyu ras kwa bahati mbaya jina lake Mwanakwetu hakulinukuu katika shajara yake ya siku hiyo.
Kwa maelezo yake katika mahojiano aliyofanya na Hamisi Holela katika kipindi cha siku hiyo cha Habari& Muziki alisema haya,
“Nilianza kuzifunga nywele hizi tangu mwaka 1982.”
Alifika hapo TBC Taifa akiambatana na Ras Innocent Nganyagwa.
Kumbuka msomaji wangu Mwanakwetu yupo katika sanduku lake anaitazama picha hiyo ambayo alipokuwa Vwawa ilikuwa na flemu ya mpingo na kioo ambavyo vilivunjika vipande vipande na hilo likasababisha picha kuwa na itilafu pembeni alipo Angela Mndugu na Mwanakwetu.
Hata Angela Binti Mndugu haonekani vizuri, mama huyu wa Kipare ambaye ni mwanafunzi wa Mwanakwetu tangu sekondari 2003-2004 Sinza Tower Secondary Sinza na hata mwanafunzi wa Mwanakwetu hapo TBC Taifa.
Nakuomba msomaji wangu nikuume sikio,
“Angela Mndugu ni mrembo sana, hata Wajerumani walimpenda zaidi wakati Watanzania
wanasuasua, wakamchukua na kuondoka naye, sasa yu Ujerumani akitangaza Idhaa DW
ya Kiswahili “
Kumbuka Msomajji wangu Mwanakwetu yu kando ya sanduku lake anaitazama picha hiyo iliyopata itilafu na akiiweka vizuri na huku akiyakumbuka hayo yote anayosimulia.
Mwanakwetu akasema moyoni,
“Mara nyingi mtumishi anapohama vitu vinaharibika na huu ndiyo ushahidi
ninauona katika sanduku hapa.”
Katika picha hiyo wanaonekana watangazaji wanne lakini yupo wa tano ambaye ndiyo aliyepiga hiyo kama nilivyodokeza awali anaitwa Batlet John Milanzi huyu ni Mmakonde Ntwara, ambaye nayeye alikuwa mtangazaji mzuri sana na sasa anafanyakazi na Redio ya Kiswahili ya Japan.
Katika kipindi walichokuwa wakitangaza wakati huo kwanza aliondoka Angela Mndugu nadhani 2015 kwenda DW Kiswahili, alafu aliondoka Mwanakwetu 2016, baadaye akaondoka Batlet Milanzi Japan, hapo sasa TBC wamebaki Farida Hamis na Hamisi Holela.
Hawa ndugu wawili; Farida Hamsi na Hamisi Holela ukiwatazama utadhani ni ndugu, wengine wanadhani ni mke na mume lakini siyo hivyo. Hamisi Holela ni shekhe mkubwa kweli na mshika dini sana wa dini Kiisilamu na ibada zote hazimpiti, nakwambia msomaji wangu kuwa hazimpiti kwa kusali na matendo, hilo Mwanakwetu anaweza kuila yamini hadharani kwa huyu kijana wake(Hamisi Holela)
Hawa mapacha Mwanakwetu akakumbuka wengine waliwaita baba na mtoto, walikuwa ni watangazaji wazuri sana na hata katika redio za kimataifa, kubwa kwa wanaowasimamia wajaribu kuwatengenezea mazingira mazuri kwa kuwapa fursa za kuonesha umahiri wao, ili watutumikie sisi Watanzania wa machakani.
Mwanakwetu alitoka katika chumba hicho chenye giza na kukaa katika eneo lenye mwanga na kuzipiga picha hizo vizuri pamoja na flemu zake.
Mwanakwetu siku ya leo anasema nini?
Ukiitazama picha hiyo vizuri unamuona huyo ras ana nywele ndefu, hizo nywele ndefu hazikuja tu bali alitoa fursa za nywele hizo kuzitunza na zikakua na hadi Julai 2015 alikuwa ndiye Mtanzania mwenye rasta ndefu kuliko wote.
Ukiangalia picha hiyo Mwanakwetu anaupala (nywele ndogo sana) kama Mwanakwetu nayeye angetoa fursa ya nywele zake kukua pengine zingekuwa sawa na za ras huyo.
Ili tuweze kufikia malengo na shabaha zetu lazima tutoe fursa kwa wote bila kujali chochote kile, hilo linamjenga yule anayepata fursa nayeye kutoa fursa kwa wengine bila ya ubaguzi wowote. Unapobagua wewe na na yule anayebaguliwa atamtafuta mnyonge wake atambagua, hapo ubaguzi unaendelea, ukiacha ubaguzi unaikata ile kamba ya ubaguzi.
“Acha ubaguzi ili na wewe , mwanao na uzao wako usibaguliwe.”
Ukitaka kumfahamu mwalimu au mhadhri watafute wanafunzi wake kwa kipindi tafauti, kwa siri watakwambia habari zote za mwalimu wao alivyo katika kila jambo .
Mwanakwetu anakupa siri msomaji wake, ukitaka kumfahamu Mwanakwetu mwenyewe watafute Faridi Hamsi, Batlet Milanzi, Angela Mndugu na Hamisi Holela watakwambia ukweli na bila woga na bila kuuma maneno dhidi ya mwalimu wao Mwanakwetu.
Mwanakwetu Upo?
Kumbuka tu huo utakuwa Ukweli Bila ya Kuuma Maneno
Nakutakia Siku Njema.
0717649257
Post a Comment