BABA ANA MKE MMOJA HANA MCHEPUKO



Adeladius Makwega MWANZA

Jumapili ni siku ni kuabudu kwa wale Wakristo na mie siku hii ilinibidi nijogee kusali hiyo dominika angalau nikafute dhambi zangu. Kwani ni muda mrefu nilikuwa sijajongea malangoni mwa Bwana.

 

Sheria ya Kanisa zinatutaka walei wote,

 

“Kuhudhuria dominika na sikukuu zilizoamriliwa.”

 

Hapo Mwanakwetu ni mgeni katika jiji la Dodoma na mkaazi mgeni wa eneo la Kijiji cha Chamwino Ikulu. hiyo ikiwa septemba kuelekea Oktoba 2021. Akajiuluza je kanisa Katoliki lipo wapi?

 

Mwanakwetu alibaini kuwa watu wa Kijiji cha Chamwino Ikulu wana Kanisa Katoliki zuri na Msikiti mzuri ulio karibu sana na Ikulu yetu. Nyumba hizi za ibada ni kwa shukurani ya marehemu John Magufuli ambaye leo hii hatunaye tena.

 

“Chamwino Ikulu kuna makanisa mengi na misikiti kadhaa, Magufuli keshafariki, hisani yake kwetu kwa kutujengea sasa haipo tena, sasa ni zamu ya sie tuliohai kuijenga misikiti na makanisa yaliyobaki, yalingane na hadhi ya Ikulu yetu. Tena katusaidia maana ramani ya Kanisa zuri na Msikiti mzuri katuachia.”

 

Mwanakwetu alipoyasikia hayo akasema ,

 

“Raha ya milele uumpe eee Bwana, Mwanga wa milele umuangazie, apumizke kwa amani, Amina.”

 

Mwanakwetu alipouliza Kanisa Katoliki lilipo aliekezwa upande lilipo kanisa hilo na kwa kuwa nyumba yake ilikuwa ya kimasikini iliyokuwa na vyumba vitano ikiezekwa chumba kimoja tu, ipo njiani, aliwasikia vijana wakiimba nyimbo za Kikatoliki wakielekea kanisa na huku awali alisikia mapigo ya kengele za kanisa hilo, alichomoka kitandani kwake saa 11.40 ya alfajiri hiyo ya dominka na kufunga gidamu za viatu vyake, akafunga zipu ya jaketi lake jeusi na kutoka katika ua wa miti wa nyumba yake hii, kuanza safari ya miguu kuelekea kanisani.

 

Alipokuwa njiani huku akiongozana na wanafunzi ambao kwa kuwatazama alibaini kuwa wanasoma shule ye Sekondari ya Chamwino Ikulu ambayo ni shule ya umma na bweni kwa wanafunzi wa kidato cha tano na sita.

 

Huku kundi hilo la wanafunzi wasichana na wavulana wachache wakiimba nyimbo hizo za Kanisa Kikatoliki.

 

Mwanakwetu kumbuka anakwenda kwa mara ya kwanza eneo hilo Kanisani kusali , akasema moyoni ,

“Leo sitaweza kupotea Kanisa, niambatane na hawa mabinti wanafunzi ambao kiumri wanalingana kabisa na binti zangu.”

 

Palikuwa na kikundi kikubwa cha wanafunzi hao ambapo walongozana nao kwa mwendo kama dakika 15 hadi Kanisa Katoliki la Bikira Maria Imakulata- Parokia ya Chamwino Ikulu-Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma.

 

Mbele ya Mwanakwetu  kulikuwa na kundi la wanafunzi kati 11-15 na nyuma yake kulikuwa na kundi lengine la wanafunzi kama tisa Mwanakwetu yu katikati akiwa umbali wa mita kadhaa.

 

Kwa kuwa siku hiyo kulikuwa upepo unaovuma vizuri, wanafunzi hawa wa kike walikuwa na mazungumzo mazuri juu ya maisha na wazazi wao huko kwao.

 

Binti mmoja akawa anasema,

 

“Mimi baba yangu ana mke mmoja, hana mchepuko”

 

Binti wa pili akajibu ,

 

“Hahahahah! Wapi? Inawezekana baba yako ndiyo anaye mke mmoja, lakini ana michepuko kibao. Nyumbani kamuweka mama yako anatawa, wewe unaona ati mama yako yupo mwenyewe. Ngoja afe utaona mtakavyoletewa ndugu kibao.

 

Mimi baba yangu ana mke mmoja lakini najua lazima atakuwa na michepuko mingi na hata nikiambiwa wewe ni ndugu yangu siwezi kukataa.”

 

Msomaji mabishano yanaendelea hivyo hivyo huku safari ya kanisani inaendelea. Naye Mwanakwetu akiwa katikati ya kundi hilo akipata hisani yao kufahamu kanisa lilipo bila kundi ya kundi hilo la wanafunzi kufahamu.

 



Mada hiyo ilimvutia sana Mwanakwetu, japokuwa alikuwa amevaa masikioni mwake kiongeza sauti kutoka katika simu, akisikiliza wimbo wa Lets Gets it on wa Marving Gaye ilimbidi auzime ili aweze kuwasikiliza wanafunzi hao waliokuwa katika mazungumzo mazito ambayo hakutarajia kama yatazungumzwa na mabinti dhidi ya baba zao wa kuwazaa.

 

Mwanakwetu akasema moyoni,

 

“Kumbe ndivyo mabinti zetu wanavyotuzungumzia?”

 

Mazungumzo ya mabinti hayo yaliendelea,

 

“Mimi nawaambieni, kwa ukweli wa Mungu wanaume hawana maana kabisa, sie nyumbani kwetu kuna jirani, wana binti wa kazi,  yule binti ni rafiki yangu sana, kwani ni msusi mzuri na hata kama nina dawa za nywele, mitindo kama bob, bati, mkeka na moja kwa moja anaweza kuichana, huwa naenda kila mara wakati wa likizo anichane na kunisuka.

 

Sasa alinisimulia kitu juu ya baba wa nyumba ile, ambaye anaishi na mkewe, ambaye ni muuguzi.”

 

Kumbuka tu msomaji tupo njiani kuelekea kanisani, sasa Mwanakwetu alikuwa jirani nao hawa wanafunzi na sasa walikuwa kando ya ukuta wa Ikulu ya Chamwino , ilibidi Mwanakwetu avae kiongeza sauti masikioni mwake lakini hakuucheza wimbo wake wa Lets get it onili kuyasikiliza mazungumzo yao, huku akitikisa kichwa kuwadanganya kama anasikiliza muzki huo.



 

Mjadala ukaendelea.

 

“Binti huyu wa kazi, kwa kuwa baba huyu anamtaka sana kimapenzi lakini anaogopa kuleta balaa katika nyumba hiyo na kila mara mama mwenye nyumba akienda zamu za usiku hospitalini, basi shughuli ndiyo hiyo, mara kagonga hodi, mara niletee hiki , mara kile.

 

Baba huyo hajatulia, sasa wakati akiendelea kumtaka kimapenzi. Binti huyu wa kazi huwa anasikiliza hata mazungumzo ya simu ya baba huyu mwenye nyumba yanaonesha kuwa ni kishadamtembezi(kishadamtembezi maana yake nini? -Binti mmoja aliuliza) Maana yake hajatulia , ni muhuni.

 

Binti wa kazi akasema kuwa kutokana na usumbufu huo mambo ya kuamua yalikuwa mawili tu;je ampe au aache kazi?”

 

Binti huyu mwanafunzi akasema kuwa yeye mwanafunzi aliulizwa atoe ushauri, akasema kuwa tena anaulizwa mambo magumu kama haya ushauri nini tena hapo?Akasema yeye alicheka tu alafu akamwambia nitakupa jibu.

 

Binti huyu aliendelea kusimulia,

 

“Likizo iliyopita nilipoenda nyumbani nikamuuliza ehe vipi mambo  yaliishaje na yule baba? Binti wa kazi alicheka sana, akaniambia ni habari ndefu. Nikamuuliuza mlishamalizana ? Maana malalamiko siyapati tena!Nataka uniambie ili nikupe ushauri.”

 

Binti huyu akasema wakati anakaribia kurudi shule binti wa kazi alimwambia kuwa kuna siri atamsimulia lakini asimwambie mtu, akajibu sawa.

 

“Siku yakuvunjwa kikombe ilifika, binti wa kazi akaniambia siku moja akiwa amekaa akitazama michezo ya kuigiza katika runinga ya hapo nyumbani muda wa saa 4 usiku.

Baba huyu akamwambia,

‘Mwanangu mbona haulali, nenda kalale sasa hivi ni usiku, pia kumbuka watoto wanaenda shuleni mapema usije ukachelewa kuamka na ukaja kugombana na mke wangu na si unamjua yeye namna alivyo? ‘

 

Binti wa kazi akasema ni kweli niliona ni hoja nzuri, nikaenda zangu kulala, basi ilipofika saa kumi na moja ya asubuhi binti wa kazi aliamka kuanza majukumu yake.

 

Kwanza akaenda kuuchukua ufunguo uliowekwa juu ya friji na mara alipoamka akashangaa anasikia mlango wa chumba cha yule baba nao unafunguliwa. Nyumba hii ikiwa giza , basi yule binti wa kazi alisema akatulia kimya aone kitakachotokea, yule baba akaja hadi jirani ya friji na kupapasa, kukiwa giza na akakutana na mkono wa binadamu umeshika funguo.

 

Ehh akashituka, ‘kumbe hapa kuna mtu’ (ndiyo baba) ‘Ehh mwanagu umeshaamka kumbe’ (ndiyo baba) ‘Oh pole sana mwangu, basi naomba funguo.’

 

 Basi binti yule wa kazi akampa funguo yule baba akafungua mlango na kutoka nje. Wakati anatoka nje akaona kuna mtu mwingine akiambatana naye, alikuwa mwanamke ambaye sura yake aliifahamu, akiishi nyumba jirani, akamsindikiza na kisha akarudi zake ndani. Baba yule akamwambia binti wa kazi,

Mwanangu hili uliloliona usimwambie mtu.’

 

Binti wa kazi akamwambia hakuna neno baba, sawa baba  na sintomwambia mtu.

 

Kweli sasa ikawa desturi ya baba yule kumuigiza mama yule jirani katika nyumba hiyo kila mkewe akisafiri au akiwa zamu za usiku. Mama huyu jirani alikuwa akija na kulala bila ya wasiwasi wowote na hata binti wa kazi alijenga urafiki mkubwa na mama huyu.

 

Baada ya tukio hilo baba huyu aliacha tabia ya kumtaka binti huyu wa kazi kimapenzi na hilo lilimuokoa binti huyu kuingia katika mahusiano ya kimapenzi na baba huyu. Binti wa kazi alikuwa akijiuliza duu wanaume ni watu hatari kweli unamuingiza mwanamke mwingine katika kitanda unacholalala na mkeo?

 

Maisha ya binti wa kazi yalikuwa mazuri na baba wa nyumba hii alimpenda sana na hata alipokuwa akigombezwa na mkewe alitetewa mno hadi mama wa nyumba hii alidhani kuwa mumewe ana mahusiano na binti wa kazi, wakati hilo halikuwa na ukweli wowote.”

 

Kumbuka msomaji wangu tupo njiani tunaenda kusali, sasa tulikuwa tunakaribia kuingia katika eneo la kanisa hilo Katoliki, namie sikuweza tena kuyasikia mengine waliokuwa wakiyazungumza.



 Hapo kila mmoja hali ya misa ilimjia, mabinti hawa waliingia kanisani na kukaa katika mabenchi ya kwaya ya kanisa hilo na kuimba katika misa yote ya siku hiyo na hata wakati tunarudi nyumbani sikuweza kuwaona tena wale wanafunzi. Hata kama ningewaona kuwauliza kilichoendelea katika kisa hicho kisingeleta picha nzuri kwao kwangu, kwa umri wangu mimi kama mzazi.

 

Mwanakwetu alirudi nyumbani kwake jumapili hiyo huku akiendelea kumsikiliza Marving Gaye na Lets Get it on.

 

Mwanakwetu Upo?

 

Nakutaki siku Njema.

 

makwadeladius@gmail.com

0717649257

 

NB

Simulizi iliandikwa Oktoba Mosi, 2021 Kijijini Chamwino Ikulu



0/Post a Comment/Comments