Adeladius Makwega-MWANZA
Wakristo wameambiwa kuwa wakati wa Kwaresma ni wa kutubu na
kuamini injili na kama ilivyoelezwa wakati wa Jumatano ya Majivu na pia dominika
hii jambo hilo linaendelea kutiliwa mkazo na kupewa msukumo wa juu zaidi.
Hayo yamesemwa katika Jumapili ya Kwanza ya Kwaresma,
Februari 18, 2024 katika Kanisa la Bikira Maria-Malkia wa Wamisionari , Parokia
ya Malya- Jimbo Kuu Katoliki la Mwanza na Padri Samson Masanja ambaye pia ndiye
Paroko wa Parokia hii.
Padri Masanja alisema kuwa uovu unamkasilisha Mwenyeenzi
Mungu na dhambi inamchukiza Mwenyezi Mungu na kama mwanadamu akifanya dhambi
anaweza kukutwa na gharika la wakati wetu .
“Ndiyo maana tunaona ghariba linalotokea wakati huo kutokana
naukaidi wa watu na watu kutokuwa tayari kumrudia Mwenyezi Mungu na kuhongoka.”
Inawezekana yatatokea magonjwa, yakatokea mapigano na vita na
kimbunga, tukumbuke upendo wa Mungu ni wa Kibaba, hivyo tuyafuate yale aliyotuagiza.
Mungu mara zote anasema halitoweza kutoka Gharika Kuu tena, huo ni upendo
mkubwa na agano la Mwenyeenzi Mungu kwetu na agano lake ni la haki.
Padri Masanja alisema kuwa katika somo la pili Paulo Mtume anasema
kuwa Kristo mwenyewe amekuja ili kuifuta dhambi na ili sisi sote tuwe wenye
haki
“Kristo ambaye hakuwa na dhambi, alikubali kuivaa dhambi, ili
sisi tulio wadhambi tuwe na haki, akawa tayari kuteshwa, akawa tayari kufa
lakini akaibuka kuwa mshindi.”
Padri Masanja aliongeza kuwa huu ni wakati wa Kwaresma,
“Huu ni wakati wa kutafakari, ni wakati wa hija, ni wakati wa
kurudi kwa Mwenyeenzi Mungu, mimi na wewe tuwekeze katika kipindi hiki na tujitathimini
kwa yale tunayoyafanya kwa ukaidi na tusiyompendeza Mungu , ili turudi, ili
tuyapokea malipo yake kama anavyoeleza Yohane Mbatizaji kuwa wakati umetimia na
mpango wa Mungu u jirani, tubuni na kuamini injili .”
Misa hii pia iliambatana na nia na maombi kadhaa,
“Eee Mungu, uwepo wako unajitokeza kwa dalili ya wema, upole
na upendo. Utujalie kuwakilimie wenzetu upole, wema na upendo. Eee Bwana-Twakuomba utusikie.”
Wakati wa matangazo ya misa hiyo, waamini walikumbushwa kuwa
kila wakati wa Ibada ya Njia ya Msalaba inapomalizika, zoezi la kuyasafisha
maeneo ya makaburi linafanyika, ikumbukwe kuwa hakuna Mkristo asiye na marehemu
popote aishipo.
“Hauna ndugu yako katika eneo la kaburi, tambua umefiwa
jirani au umefiwa na mwanajumuiya, hivyo fika kwa ajili ya kumsafishia huyu ndugu,
jirani au mwanajumuiya mwenzako. naombeni tuzingatie hilo . Marehemu wote wanatuhusu,
fanyeni usafi wa makaburi kwa wakati .
Tuzingatie ibada za Njia ya Msalaba zipo sita wakate huu wa
Kwaresma hivyo siku za usafi wa makaburi ni sita , lakini siku ni tano maana
ibada ya Njia ya Msalaba ya Mwisho ina mambo mengi. Eneo letu la makaburi ni
kubwa tukifika waamini 13, siyo rahisi kulimaliza maana majani ni mengi, miti
imekomaa, tufikeni kwa wakati na tuje na mapanga, majembe na mafyekeo.”
Hayo yalinadiwa katika misa hiyo na msomaji wa matangazo. Kwa
utaratibu wa mazoea ya Wakristo wengi ,wakati karibu ya Pasaka huwa ni muda wa
kusafisha makaburi ya wafu.
Kwa hakika hadi misa hiyo inamalizika saa moja ya asubuhi
hali ya hewa ya eneo la Malya na viunga vyake ni joto, jua na mawingu kidogo , huku
ikiaminika kuwa mwezi Februari mvua inapungua kidogo na itarudi kwa kasi mwezi Machi
na hivi sasa inatoa nafasi wakulima kuvuna mazao yao yalikomaa ili watayarishe
mashamba tena ili wapande kwa mara nyingine.
Post a Comment