Adeladius Makwega-MWANZA
Mwaka 2017 Mwanakwetu akiwa mtumishi wa Halmashauri ya Lushoto, aliiitwa kwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Tanga Mhandisi Zena Said, wito huo ulitolewa baada ya kumalizika kikao katika ukumbi wa Mkuu wa Mkoa wa Tanga ambaye alikuwa ndugu Martine Shigella.
Hapo kila mmoja alyeitwa aliitikia wito huo mara moja, Mwanakwetu alijongea mbele ya Katibu Tawala huyo na kwenda kupokea maelekezo ya mkubwa.
Kwa wale ambaoa hawamfahamu Mhandisi Zena Said sasa ni Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar. Msomaji wangu nakuomba kwa heshima na taadhima zote nikuume sikio jambo hili, hii ikiwa ni mbiu ya mgambo kwako msomaji wa Mwanakwetu popote ulipo.
“Injinia Zena Said ni kiongozi mahiri, makini na mwenye uwezo mkubwa wa kufanya kazi na watu wa hulka zote, anao uwezo wa kufanya kazi katika mazingira yoyote yale. Yeye ni kiongozi anayeweza kumtia moyo mfanyakazi mwenzake katika hatua ngumu anazopitia, ni mkweli na muwazi kwa walio chini yake.
Mwanakwetu anaendelea kushauri kuwa kama Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pale inapokuwa na haja ya kubadilssha Katibu Mkuu Kiongozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Injinia Zena Said ni mama sahihi kwa nafasi hiyo ili Zanzibar wanufaike na utendaji wake kazi na Tanganyika hivyo hivyo, maana kwa sasa Mwanakwetu anawaonea gere Wazanzibari.
Mwanakwetu anatambua yanaweza kuibuka maneno, oooh mbona wanawake wanakuwa wengi katika ngazi za juu, majibu yake ni haya, kwa Injinia Zena Said, yeye ni kiongozi mahiri na nafasi hiyo akipewa mambo yatakuwa mazuri.”
Hii ni ilani ya Mwanakwetu katika makala haya siku ya leo, pia unaweza kuiita ni mbiu ya mgambo.
Kumbuka msomaji wangu Mwanakwetu yu ofisini kwa Injinia Zena Said, miongoni mwa mambo aliyoelezwa na kiongozi huyo na kuyafanyikia kazi lilikuwa ni malalamiko ya wabunge wa Lushoto Rashidi Shangazi(Mlalo) na Shabani Shekilindi (Lushoto) yaliyofikishwa ofisini kwake.
Mwanakwetu alimuuliza Injnia Zena Said kuwa hata Rashidi Shangazi alifika kulalamika ? Injinia Zena Said alijibu naam.
Mwanakwetu akajiuliza moyoni hawa shemeji zangu wasambaa wana nini tena?
Nakuomba msomaji wangu kumbuka Mwanakwetu yupo ofisini kwa Injinia Zena Said, lakini naona ni vizuri nikurudishe nyuma uwafahamu wabunge waliowahi kuongoza majibu hayo mawili kwa vipindi tofauti;
“ Lushoto ni Balozi Abdi Mshangama,Hendry Shekifu na Shabani Shekilindi na Mlalo ni Charles Kagonji (mwanahabari), Hassan Ngwilizi(askari) na Rashidi Shangazi (Mlalo) ”
Katika hoja za Wabunge hao wa Lushoto alizoambiwa na Katibu Tawala, Mwanakwetu alitoa ahadi kwa kiongozi wake atafanyia kazi lakini akilini mwa Mwanakwetu alisikitika mno kwanini Rashidi Shangazi hakumwambia Mwanakwetu? Mbona wako jirani nayeye na wanazungumza mengi?
Mwanakwetu alimuaga Injini Zena Said na kutoka zake Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga na kurudi zake Lushoto.
Katika kutafiti hilo alibaini kuwa Mbunge wa Mlalo pengine alihisi kuwa Mwanakwetu alikuwa jirani sana marehemu Brigedia Hassan Ngwilizi ambaye walikuwa wakiongea mengi na Mwanakwetu, na pengineRashidi Shangazi alidhani kuwa Mwanakwetu labda alikuwa na mpango wa kumpa nguvu mwanasiasa huyu wa Tanzania na mpiganaji wa zamani wa JWTZ.
Mwanakwetu alihisi hilo akilini mwake tu labda pengine lilimpa shaka mno Rashidi Shangazi isije ikawa mwisho wake wa Ubunge ukawa 2020 hivyo kimbilio lake lilikuwa ni Injini Zena Said .
“Huyu Mkurugenzi kaletwa na Brigedia Hassan Ngwilizi kuja kuwamaliza
Shekilindi na Shangazi.”
Hayo Mwanakwetu aliyabaini na kwa kuwa Brigedia Ngwiliza aliwahi kuwa Waziri wa TAMISEMI hapo awali.
Kwa hakika msomaji wangu nakuuma sikio kuwa mahusiano baina ya Brigedia Ngwilizi na Mwanakwetu yalikuwa ya kidugu mno.
“Brigedia Ngwilizi kila marai alifika Halmashauri ya Lushoto kulipia vibali vya ujenzi na viwanja na nyumba zake , alionana na Mwanakwetu, aliweza kufika hata nyumbani kwa Mwanakwetu na Mwanakwtu kufika kwa Brigedia mara kadhaa na hata kula ugali kwa kiongozi huyu na mpiganaji wa zamani wa Tanzania katika oparesheni kadhaa nje ya taifa hili la Afrika Mashariki.”
Mwanakwetu anakwambia ukweli msomaji wake kuwa urafiki wake Brigedia Ngwiklizi haukuwa urafiki wa mchezo bali urafiki wa kidugu ambapo Mwanakwetu alijifunza mengi hasa hasa ulinzi binafsi katika hali ya hatari.
Kumbuka msomaji wangu Mwanakwetu yu safarini akitokea Tanga kurudi Lushoto, akakumbuka namna siku moja alivyozungumza na Brigedia Ngwilizi juu ya ufanyaji kazi wa TAMISEMI yao baina yake na Waziri wake Mdogo Mizengo Pinda.
“Hii TAMISEMI yenu tulifanyakazi kweli kweli na kazi mojawapo ilikuwa ni ujenzi wa Shule za Kata nchi nzima, sambamba na hilo Wizara Elimu kuhamisha shule zote za sekondari kwenda TAMISEMI.
Hapo Waziri wetu Mkuu alikuwa huyu Edward Lowassa ambaye sasa wanamuita fisadi.”
Brigedia Ngwilizi alisema kuwa wapo watu waliziita shule hizo ni majengo ya kuku, matundu ya ndege lakini kwa hakika zimesaidia sana watoto wengi wa masikini kupata elimu, japokuwa zina changamoto tele sasa nyinyi miliopo TAMISEMI mzitatue changamoto hizo maana ramani ya vita mnayo.
Mwanakwetu alikumbuka kuwa siku hiyo alimuuliza kiongozi huyu swali hili,
Je mwaka 2008 baada ya kujiuzulu kwa Edward Lowassa Bungeni na je baada ya uteuzi wa Mizengo Pinda kuwa Waziri Mkuu jambo hilo halikukushangaza sana?
“Unajua mimi nilifurahi kuona kuwa Mzengo Pinda ni mtu niliyefanya naye kazi sasa ameaminiwa na kushika nafasi hiyo .”
Brigedia Ngwilizi alisema kuwa uteuzi wa Edward Lowassa kuwa Waziri Mkuu baada ya Jakaya Kikwete kushinda Urais mwaka 2005 ulikuwa na taswira ile ya utawala wa mwalimu Julius Nyerere ambapo mawaziri wenye nguvu za kisiasa walishika nafasi hiyo kama vile Edward Moringe Sokoine , Cleopa David Msuya, John Malecela na Salim Ahmed Salim na hiyo ikawa sivyo kama alivyofanya Benjamin Mkapa kwa uteuzi wa Fredrick Sumaye mwaka 1995 ambaye awali alikuwa Waziri Mdogo.
Msomaji wangu kumbuka hayo Mwanakwetu alikuwa anakumbuka safarini, Mwanakwetu alifika Lushoto na kumtafuta Mbunge wa Mlalo na kumueleza kuwa yeye yupo hapo kufanya kazi tu na ameelezwa kwa kina juu ya malalamiko yao na Katibu Tawala Mkoa Tanga wakati huo Injinia Zena Said,
“Mimi sijafika hapo Lushoto kwa ajili ya mtu yoyote, bali kufanya kazi na niliowakuta hapo, hivyo naomba tufanye kazi ya Watanzania.”
Maisha yaliendelea kama kawaida huku akiendelea kuwasiliana na Brigedia Hassan Ngwilizi.
Je siku ya leo Mwanakwetu anasema nini?
Kwa hakika kuchaguliwa Edward Lowassa kuwa Waziri Mkuu mwaka 2005 ilikuwa ni kuuwaweka mafahari wawili katika zizi moja, lakini kwa uhakika kabisa ndugu Edward Lowassa alipokuwa Waziri Mkuu alitoa ramani ya vita vizuri kwa kufanya kazi zilizotukuka ambayo ilitoa muelekeo wa serikali ya awamu ya nne.
Mwanakwetu ameyakumbuka matukio hayo tangu ofisini kwa Injinia Zena Said hadi mazungumzo yake na Brigedia Hassan Ngwilizi kutokana na msiba wa Edward Lowassa ambaye amefariki dunia Februari 10, 2024 huku taifa la Tanzania likiomboleza msiba huo kwa siku tano.
Historia ya maisha ya Edward Lowassa inatoka mbali kwa walio wengi hafahamu hilo ,
“Mara baada ya kufariki kwa Edward
Moringe Sokoine, Novemba 2,1985 CCM iliwachagua wabunge kadhaa kutoka Umoja wa
Vijana kuwa Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, majina ya
vijana hao ni Anne Makinda, Pascal Mabiti, Sukwa Said Sukwa, Khatib Hassan Khatib,
Edward Lowassa na Venance Ngulla.
Wengi wa watazamaji wa masuala ya siasa za Tanzania na hata Mwanakwetu wanaona kuwa maamuzi hayo yalikuwa na lengo kwa CCM kumpata mrithi wa Edward Moringe Sokoine na mwakilishi bora wa jamii ya wafugaji.
Katika siasa za ukanda wake na kweli CCM waliweza kulifanikisha hilo, lakini hilo pia lilitaka kuwapokonya tonge la utawala wa taifa hili mara baada ya Lowassa kwenda upinzani mwaka 2015.”
Mwanakwetu kwa heshima zote anatoa pole kwa Bi Regina Lowassa kwa kumpoteza mumewe, anatoa pole kwa watoto wa kiongozi huyu, anatoa pole kwa ndugu jamaa na marafiki wote wa familia hii na anatoa pole pia kwa wote wanaoheshimu kazi zilizofanywa na kiongozi huyu alipokuwa hai.
“Bwana ametoa, Bwana Ametwaa na Jina la Bwana lihimidiwe-Amina.”
Mwanakwetu Upo?
Nakutakia siku njema.
0717649257
Post a Comment