BURIANI THADEI OLE MUSHI

 



Adeladius Makwega-MWANZA

Katibu Mkuu mmoja wa Wizara mojawapo nchini alimuita mtumishi wake wa umma ili kuongea naye, kwa bahati nzuri kando ya kikao hicho alishiriki kiongozi anayesimamia masuala ya kiutumishi.

“Ndugu yetu nimekuita bila shaka unafahamu nafasi yangu na huyu kando ndiye anayesimamia masuala ya kiutumishi. Wewe ni mwandishi mzuri lakini namna unavyoandika kana kwamba kama siyo mtumishi wa umma.

Jambo hilo linatukwaza na ndiyo maana tumekuita na taratibu za kiutumsihi zinakataza hilo, kwa hiyo tunakuandikia barua kwa kukiuka hilo ujieleze.”

Katibu Mkuu akatoa nafasi ya Mkuu wa Utawala na Rasilimaliwatu nayeye akasema jambo katika hilo hilo huku akinukuu vipengele vya kanuni za utumishi wa umma.

KIongozi huyu alinukuu kanuni ya utumishi wa umma C.15(1) ya 2009,

“No correspondence which has passed between Ministries, Independent Departments, Regions, Local Government Authorities or between the public and Ministries/ Independent Departments/ Executive Agencies/ Regions/Local Government Authorities may be communicated to the Press or any member of the public without the approval of the Chief Executive Officer concerned.”

Hivyo ndivyo ilivyonukuliwa na kiongozi wa rasilimali watu ana kuungwa mkono na Katibu Mkuu.Kikao hicho kilimalizika kidugu nayeye mtumishi kukubaliana na aliyoambiwa na maisha yakaendelea kama kawaida. Baada ya kikao hicho mtumishi husika alirejea kanuni iliyotajwa na alibaini kuwa kanuni hiyo ya utumshi wa umma ilinukuliwa kwa kifupi na kipengele muhimu kuachwa ambapo ilitakiwa kusomwa hivi,

“No correspondence which has passed between Ministries, Independent Departments, Regions, Local Government Authorities or between the public and Ministries/ Independent Departments/ Executive Agencies/ Regions/Local Government Authorities may be communicated to the Press or any member of the public without the approval of the Chief Executive Officer concerned;

but information of general nature which may be material assistance in discussing local questions need not be withheld, provided that such information is not of confidential nature or likely to infringe the privacy of others.”

Ndiyo kusema kwa kifupi siyo taarifa zote zinatakiwa kuombwa kibali kwa wakubwa kwa mtumishi wa umma anapozitumia katika mijadala kwa umma. Ndugu huyu alikwenda mbali zaidi na kufahamu kuwa hata katika Ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977 Sura ya 2 Marejeo ya 2008,  nanukuu;

“18 (1) Bila ya kuathiri sheria za nchi, kila mtu yuko huru kuwa na maoni yoyote na kutoa nje mawazo yake na kutafuta, kupokea na kutoa habari na dhana zozote kupitia chombo chochote bila ya kujali mipaka ya nchi, na pia ana uhuru wa mawasiliano yake kutoingiliwa kati.”

Kwa hakika maelezo ya ibara hiyo yako wazi na hayana mjadala .



Kwa vigezo vya kanuni ya utumishi wa umma C 15 (1) ya 2009 na Ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hapo mtumishi huyu alisema hakuna kigugumizi, haki yako ukiifahamu itumie ipasavyo, usipoitumia shauri ni lako wewe mwenyewe na itapendeza kama haki hiyo utaitumia kwa maslahi ya wengi.

Kwan ini siku ya leo Mwanakwetu anayandika makala haya?

Kubwa ni kutokana na msiba wa Thadei Ole Mushi aliyefariki Dunia ambapo kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa mazishi yake ni Jumatano Februari 7, 2024 huko Kilimanjaro akiwa ni miongoni mwa vijana wadogo wachache wa Kitanzania walioweza kutumia kalamu zao kwa manufaa ya jamii ya wanyonge wa Tanzania.

Mara baada ya msiba wa Thadei Ole Mushi, hakuna shaka mitaani nchini Tanzania yanazungumzwa mengi na mojawapo ni kuwa Thadei Ole Mushi alikuwa mwalimu wa kawaida akiijenga Tanzania katika kada hiyo.



Mwanakwetu anachoweza kusema kwa leo ni kuwa Thadei Ole Mushi alikuwa Mtanzania aliyeitumia vizuri ibara ya 18 ya katiba ya Jamhuri wa Tanzania katika kutoa maoni yake yenye shabaha ya kumkomboa Mtanzania mnyonge.

“Swali la kujiuliza kwa kila mmoja wetu, wakati mwili wa Mtanzania huyu kutoka mkoa Kilimnajaro unaporudishwa mavumbini, Je kila mmoja wetu popote alipo anaitumia ipasavyo haki hiyo ya ibara ya 18?

Swala la pili je mimi na wewe tunazitumia vipi taaluma zetu tulizosomea kwa manufaa ya wengi?”

Kwa hakika kila mmoja anayo majibu yake, nakuomba msomaji wangu hayo majibu kaa nayo moyoni alafu ujitathimini, kama tutapiwa kwa alama kati ya 1-100 % kila mmoja atapata maksi zake , Mwanakwetu anaamini kuwa Thadei Ole Mushi alipata daraja A katika hilo.

Wako wanaodai kuwa Thadei Ole Mushi alikuwa Mwana CCM, hilo ni kweli swali ni Je viongozi wa CCM wote walikuwa wanaridhika na mwenendo huo wa mwanachama wao?

Majibu yanaweza kuwa pengine ni sawa na yaleyale ya mtumishi yule aliyeitwa na Katibu Mkuu wake ofisini hadi kufikia kunukuliwa kwa kanuni ya utumishi wa umma C.15(1) ya 2009, kwa kifupi na mtumishi yule alikwenda mbali zaidi hadi kufikia ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mwanakwetu anaamini kuwa Thadei Ole Mushi alitimiza vizuri katika ahadi ya nane ya Mwama CCM.

“Nitasema kweli daima, Fitina kwangu mwiko; Nitasema kweli daima fitina kwangu mwiko.”

Katika hilo ipo mifano mingi ya mambo yaliyosemwa na Thadei Ole Mushi na kufanyiwa kazi baadaye, kilichokuwa kinapishana ni muda tu baada ya jambo hilo kuandikwa na muda wa kulitekeleza, kama ikiwa  siku, juma, mwezi au mwaka.

Ukichambua mambo ambayo yalibeba maudhui ya maandiko ya Thadei Ole Mushi , maadiko yake hayakuwa ya kibaguzi ya kuangukia mrengo mmoja, kwa hakika  aliweza kusemea hata upinzani, aliwasonta vidole viongozi kadhaa serikalini na hata kukosea maamuzi ya CCM na hata maamuzi ya serikali.Kuwa mwana CCM haikuwa kibali chake cha kuyaona maovu na kuyafumbia macho.

Mwanakwetu anaamini kuwa Thadei Ole Mushi yeye kama Mkristo alitimiza kikamilifu amri kuu ya MAPENDO.

Mwanakwetu kwa siku ya leo ananukuu kutoka Bibili Takafifu, kitabu cha  Waebrania 12, 14 ,

“Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote na utakatifu, ambao bila ya kuwa nao hakuna mtu atakayamwona Bwana.”

Mwanakwetu anaamini kuwa yako mambo mengi ya kujifunza katika msiba wa Thadei Ole Mushi;

Kwanza walioguswa na kifo chake,

Ni Watanzania kutoka vyama mbalimbali vya siasa, iwe upinzani na hata CCM na viongozi mbalimbali katika serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Kaka, rafiki na ndugu yangu Thadei Ole Mushi, Mungu Baba yetu , akupe pumziko la milele mbinguni. Kizazi chetu kimempoteza mwalimu, mchambuzi na mwanajamii kijana aliyetumia maarifa na kalamu yake kutoa maoni na hisia zake katika nyanja nyingi.”.

Hayo ni ya Mkuu wa Mkoa wa Njombe mhe . Mtaka Antony.

“Poleni sana sana.

Nimesikitishwa sana na msiba huu. Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi.

Tumempoteza kijana mahiri katika kuwasilisha jumbe mbalimbali kwa jamii kupitia makala zake pendwa.

Lala Salama Ole Thadei Mushi.”

Hayo juu ni ya Balozi Hoyce Temu, Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa .



Jambo la pili la kujifunza kutokana na msiba huo,

“Kwa wanahabari wote tunatakiwa kutumia vizuri kalamu zao. Thadei Ole Mushi alifanya kazi nzuri ya kihabari, japokuwa hakuwa mwanahabari, hivyo wanahabari tusipotimiza wajibu wetu ndani ya jamii wanaweza kuibuka akina Thadei Ole Mushi wengi na wakasaidia jamii kuliko hata vyombo vya habari. Huku wanahabari hao wakiwa miongoni mwa wafuatiliaji wa taarifa zake.

Wanahabari wa Tanzania tusifungwe na ajira, tusifungwe na itikadi, tusifungwe na maslahi binafsi, tujali maslahi ya walio wengi ambao hawana sauti.

Hapa duniani tunakaa kipindi kifupi sana, ndugu yetu Thadei Ole Mushi ameecha mke, ameacha watoto, ameecha kila kitu huku akirudi alipotoka na hiyo ni ya sisi sote, hiyo ni safari yetu. Kila mmoja atapimwa kile alichokisomea na namna alivyoitumikia jamii yake”

Mwanakwetu anaiweka chini kalamu yake katika makala haya ya buriani akitoa pole kwa familia ya Thadei Ole Mushi tangu mkewe , watoto wake, wazazi, ndugu jamaa na marafiki.

“Raha ya milele uumpe ee Bwana na Mwanga wa Milele umuangazie apumzike kwa amani amina.”

Mwanakwetu upo

Buriani Thadei Ole Mushi.

makwadeladius@gmail.com

0717649257




 

 

 

 

 

 

0/Post a Comment/Comments