Adeladius Makwega-MWANZA
Jumatano ya majivu imefanyika Februari 14, 2024 ambapo Mwanakwetu alikuwa miongoni mwa waamini waliosali misa ya siku hiyo ambapo Padri aliyeadhimisha misa katika kanisa la Bikira Maria Malkia wa Wamisionari– Parokia ya Malya Jimbo Kuu Katoliki la Mwanza, Padri Samson Masanja alilisitiza kuwa Kwaresma hii itumike kwa kila Mkristo kufanya matendo ya huruma kwa wahitaji.
Mwanakwetu kama Mkristo ameamua katika kipindi cha Kweresma hii atajitahidi kutayarisha makala 40 ambayo yote yatakuwa na mrengo huo huo wa kuyatazama maeneo yanayohitaji huruma kwa wengine katika sekta kadha akiamini kwa wale watakaosoma, kusikiliza na kutazama makala haya wanaweza kufungua mlango wa kuitazama jamii kwa taswira nyingine kwa jicho la makala haya.
Siku ya Februari 15, 2024 Mwanakwetu aliamua kuandika makala ya tafakari kwa ndugu zake Watanzania hasahasa juu ya ubaguzi mkubwa unaofanyika katika utoaji wa elimu yetu, hasahasa kwa watoto na wanafunzi ambao wana uwezo mdogo wa kufaulu mashuleni hasa hasa kwa shule binafsi ambalo jambo hilo Mwanakwetu anaona siyo sahihi na ni ubaguzi kama ulivyo ubaguzi wa rangi.
Ubaguzi huo wa kielimu umevishwa jambakoti la dhana moja inayohitaji shule hizo kufanya vizuri katika matokeo ya taifa ya kidato cha pili, nne na kidato cha sita. Jambo hilo Mwanakwetu anaona kuwa halipo kwa vyuo vya kati na vyuo vikuu na hiyo haina maana kuwa elimu inyaotolewa vyuo hivyo haijapitiwa na ubaguzi, huko ubaguzi upo lakini ukiwa na jambakoti lingine.
Shule nyingi binafsi zinapotaka matokeo bora huwa zinapokea wanafunzi wenye uwezo tu , wakijipa upofu kuwa jamii inahitaji watu wa aina zote ili kukamilisha shughuli za maisha ya kila siku.Jamii haihitaji wasomi watu wote, hivyo kila shule inahitaji kutoa nafasi hiyo kwa wanafunzi wote ili kuibadilisha jamii jambo hilo cha kusikitisha sasa linakita mizizi hata katika shule za dini.
Msomaji wangu nakuomba kwa hisani yako yatazame matokeo haya ya shule ya sekondar mbili moja ya umma na moja binafsi katika mkoa wa Mbeya.
“Shule ya wasichana ya Mtakatifu Francis Mbeya na Shule Mchanganyiko ya
Ilomba kwa mtihani ya kidato cha pili 2021 na kidato cha nne 2023.”
Je hali ya
matokeo ilikuwaje?
“Mwaka 2021 Shule ya Sekondari Ilomba ambayo ni shule inayomilikiwa na wazazi chini ya Halmashauri ya Jiji Mbeya, wanafunzi zaidi ya 350 walifanya mtihani huo kwa kidato cha pili ambapo matokeo yalipotangazwa yalikuwa hivi I-8, II-40, III- 62 , IV- 206 , O- 29. “
Wakati kwa Shule ya Wasichana ya Mtakatifu Francis Mbeya inayomilikiwa na Kanisa katoliki Jimbo Kuu la Mbeya wanafunzi waliofanya mtihani ni 91 na wote walipata daraja la kwanza. Wanafunzi hao hao walisoma 2022 kidato cha tatu na 2023 kuingia kidato cha nne na kuhitimu .
“Kwa Shule ya Mtakatifu Francis daraja la kwanza walipata wote 91 lakini
Ilomba daraja la I-7 , II- 38, 3-51, 4-159 na 0 – 41.”
Ukitazama namba ya wanafunzi waliofanya mtihani kwa kidato cha pili na nne kwa miaka hiyo yaani 2021/2023 Ilomba na Mtakatifu Francis ni 330/ 308 kwa 91/ 91.
Ukiitazama pia namba ya idadi ya wanafunzi Shule ya Mtakatifu Francis imebaki palepale 91 huku Ilomba inapungua kutokana changamoto mbalimbali za jamii za Kitanzania, kama vile ujauzito, kuacha masomo, kufeli, kukosekana kwa mahitaji muhimu kwa mwanafunzi mmoja mmoja.
Kama hayo juu hayatoshi Shule ya Sekondari Ilomba ilipokea wanafunzi 300 ambayo ni mara tatu ya Shule ya Mtakafifu Francis lakini madaraja ya ufaulu wa matokeo haya Ilomba sekondari inawagawa wanafunzi hao katika ufaulu huu daraja la I, II, III, IV na 0 huku Shule ye Mtakafifu Francis Daraja lao ni I ambalo wamefanya vizuri sana.Hilo wanapaswa kupongezwa.
Shule ya Sekondari Ilomba inakundi la wanafunzi ambao wamemaliza masomo ya kidato cha nne wanaweza kuingia vyuo vya kati ambalo hilo ni kundi muhimu sana katika kuisaidia jamii katika kazi za mikono ambazo ni uzalishaji wa mali kwa kiwango cha juu na kundi linalowapokea wanajamii wengi na kazi za mikono zilifanywa na Yesu Kristo na Familia yake pia.
Ukiyatazama vizuri matokeo ya Shule ya Sekondari Ilomba,
“Yupo mwanafunzi wa kike aliyepata daraja la 1.9 Msichana huyu namba yake
ni S.1787/0064 Civic A, Hist A,Geo A,Kisw A,Engli C, LIT ENG-C PHY B,CHEM A,BIO
B na B/MATH B.”
Mwanafunzi huyu kama angepata mazingira mazuri zaidi ya kujisomea na kujifunzia angeweza kufanya vizuri zaidi katika masomo yote na angeweza kupata daraja A kwa masomo yote 10 aliyofanyia mtihani.
Binti huyu ambaye jina lake ilikuwa ngumu kulifahamu kutokana na Baraza la Mitihani la Taifa kumtambulisha kwa namba ukiyatazama matokeo yake,
“Binti huyu hakufanya vizuri sana kwa
masomo matano English C, Literature English C, Physics B, Bailogy B na Basic
Mathematic B .”
Ukiyatazama matokeo ya hayo ya Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Mtakatifu Francis wastani wa ufaulu wake ulikuwa daraja A kwa wanafunzi wote lakini kwa Shule ya Sekondari ya Ilomba wastani wake ulikuwa ni daraja D, hawa Ilomba wamevukwa madaraja matatu.
Mwanakwetu siku ya leo anasema nini?
Kwa hakika msomaji wangu umezitazama takwimu hizo kwa pamoja, huyu mwanafunzi wa Ilomba aliyepata daraja la kwanza la mwanzo kabisa ni mwanafunzi mzuri hata baada ya kumaliza elimu yake kwa kuwa amesoma katika mazingira magumu na amepata ufaulu huo , kwa mwanafunzi kama huyu anaweza kuwa msaada mkubwa kwa jamii yake na hata kufanya kazi katika mazingira yoyote yale ya taifa hili.
“Katika mtazamo wake katika maisha mwanafunzi huyu anatambua kuwa darasani kwake walikuwa wanafunzi zaidi ya 300 na wapo waliofaulu na wapo waliofeli, anatambua wapo waliofeli kwa uzembe wao na wapo waliofeli kutokana na changamo kadhaa za shule na jamii zungukwa.”
Wale wanaopata nafasi ya kuongoza taasisi za elimu na hasa serikali wajitahidi mno kuweka mazingira ya watoto wa Kitanzania ili waweze kusoma, wazazi tujitahidi kutatua changamoto za watoto wetu wanapokuwa shuleni mathalani kuchangia chakula cha mchana na kuwapa vitendea kazi vyote hasa zana za kusomea na kujifunzia.
Mwanakwetu anaamini kuwa mchango wa shule za umma ni mkubwa katika kutoa fursa sawa ya elimu kwa watoto Wakitanznia na kila mtoto angalau anayo nafasi yakusoma ya kwenda shuleni na kusoma japokuwa uwekezaji katika shule za umma bado duni, hazina vifaa bora, vya kujifunzia, zana bora, maabara bora na hata walimu bora kwa masomo mbalimbali na hasa ya sayansi.
Ukiangalia matokeo ya mwanafunzi wetu wa mfano huyu S.1787/0064 amepata B katika masomo ya sayansi yaani Fizikia, Bailojia na Hisabati na pia B katika masomo ya Lugha ya Kiingereza.
Kwa kuwa Mwanakwetu anayaandika makala haya wakati wa Kwaresma anamuomba Baba Askofu Mkuu Gervas Nyaisonga wa Jimbo Kuu Katoliki la Mbeya kwa heshima na taadhima kwa kuwa ndiye mmiliki wa Shule ya Sekondrai ya Mtakatifu Fransis ambayo inafanya vizuri Kitaifa atambue haya,
“Shule ya Sekondari Ilomba inahitimisha wanafunzi wengi , Shule hii ipo jirani na Shule ya Wasichana ya Mtakatifu Francis ambapo ufaulu wa Shule ya Wasichana ya Mtakatifu Francis na Ilomba ni sawa Mbingu na ardhi, katika kundi la wanafunzi 300 wapo wanaokuja kuwa wauguzi, wafanyabiashara, makarani, madereva, askari polisi, askari jeshi , magereza, walimu na wajasirimali wa eneo hilo.
Baba Askofu Nyaisonga kwa hisani yako unaweza kuagiza angalau walimu wa shule ya Wasichana ya Mtakatifu Francis kuwasaidia kuwasomesha mara moja moja wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Ilomba.
Jambo hio halina gharama kubwa kikubwa ni kuwapatia posho kidogo tu walimu hao wakaenda huko kuhokoa jahazi la taaluma.”
Mwanakwetu anaamini kuwa Baba Askofu Mkuu Nyaisonga anapotaka kupata dereva wa kumuendesha kuna uwezekano mkubwa dereca wake akawa aliwahi kusoma Ilomba sekondari, Baba Askofu akitaka mlinzi kuna uwezekano akawa amesoma Ilomba sekondari na hata Baba Askofu akitaka kupata Padri tarajiwa kun auwezekano akawa pia amesoma Ilomba sekondari.
Kwa kuwa leo hii ni wakati wa Kwaresma, Mwanakwetu anatumia makala haya kuwakumbusha hasa wamiliki wa shule za kanisa kutambua kuwa Yesu Kristo alikuwa Selemala tu na wakati huo tabaka la wasomi na tabaka la watawala ni miongoni mwa tabaka lililomkandamiza.
Kanisa lisisahau kuwekeza katika kubadilisha mitazamo ya ngazi za juu lakini lisiilipe kisogo kundi kubwa ambalo linakosa elimu bora na kufanya vibaya katika mitihani ya kitaifa hapa Tanzania, hapa kanisa na serikali wanaweza kuongeza nguvu zaidi katika uwekezaji katika vyuo vya kati hasahasa mafunzo ya ufundi.
Huko itakuwa ni kuwapa matumaini na mafunzo hayo yatolewe kwa gharama nafuu ili kulipa matumaini kundi hilo, vinginevyo kundi likikosa matumaini ni hatari zaidi.
Mwanakwteu Upo
Kumbuka Tusiwape Kisogo Wanaofeli Mitihani ya Taifa.
Nakutakia Siku Njema
0717649257
Post a Comment