Adeladius Makwega-MWANZA
Mwanakwetu alikumbuka kuwa Novemba 10, 2023 alilipia kutengenezewa
kadi ya Bima ya Afya ya NHIF, hivyo imepita miezi mitatu tangu afanye hivyo aliamua
kudamkia ofisi ya NHIF Mwanza ambayo ipo umbali wa Kilomita 120.
Alikiacha kitanda chake saa 10.00 alfajiri na kujiandaa kwa
kujimwagia maji baridi na kuvaa nguo zake haraka haraka na kutoka kwake kuelekea
stendi ya mabasi na kupanda basi moja ambayo lilionekana kuwa na abiria
wachache, akiwa ndani ya basi hilo alichagua kiti cha mbele lakini baadaye alijulishwa
kuwa kiti hicho kina abiria na walimuonesha kiti kingine na kukaa kiti cha
katikati, akilipa nauli ya shilingi 6000/- kutoka Malya hadi Nyamhongolo Mwanza.
Kwa kuwa abiria walikuwa wachache, basi hilo liliokoteza
abiria kidogo kidogo na kubaki hapo stendi Malya hadi saa 12.00 ya asubuhi,
zikitumika saa mbili kukusanya abiria kidogo kidogo.
Saa 12.05 ndipo dereva aliondoa gia na kuianza safari kuelekea
Nyamhongolo Mwanza.
Basi hilo la saizi ya kati liliokoteza abiria njiani vizuri
na kwa kuwa Mwanakwetu alidamka alfajiri mno hivyo alipitiwa na uzingizi mzito na
kulala fofofi basini.
Masikini Mwanakwetu alijipa upofu wa hatari ya kulala
safarini, hata kama linatokea lolote kwa gafla ukiwa usingizini hadi ujikusanye
utoke usingizini, hapo umeshaumia, lakini imani ya Mwanakwetu aliiweka mikononi
kwa dereva wa basi hilo ambaye alikuwa hata hamfahamu umahiri wa udereva wake.
Kwa kuwa barabara ya Kwimba Mwanza ni vumbi kwa karibu
asilimia 75 abiria anayelala ni vigumu kulala mfululizo kutokana mtikisiko na hivyo
Mwanakwetu alilala kipindi kifupi na baadaye kushituka kutokana na mambo
kadhaa; mkitikisiko wa barabara, kelele za mazungumo ya abiria ndani ya basi na
tatu ni muziki ndani ya runinga ya basi hilo.
Nakukumbusha tu msomaji wangu kuwa Mwanakwetu alikuwa amekaa
kiti cha katikati kwa kuwa kiti cha mbele aliondolewa, hivyo abiria anayesafiri
na basi akiwa katikati ya basi hilo kelele hizo tatu anazisikia vizuri kuliko
abiria ambaye yu kiti cha mbele au abiria aliye kiti cha nyuma cha basi hilo.
Kwa hakika kelele za ubovu wa barabara hii ilisababisha Mwanakwetu
kuyumbayumba katika kiti mithili ya mlevi aliyekunywa pombe mnazi lakini salama
yake alishikilia chuma cha kiti cha abaria aliye mbele yake nga-nga-nga.
Kelele ya pili ilikuwa ni muziki uliyokuwa ukichezwa katika runinga
ya basi hili, kwa hakika basi hili ni basi pekee linalofanya kazi kati ya Malya
na Mwanza lenye runinga inayofanya kazi . Ndani ya basi hili Mwanakwetu alisikia
na kuziona nyimbo nzuri na mbaya katika runinga hiyo, kubwa ni nyimbo zote
nzuri zilikuwa za mwanamuziki Christian Bella.
Wakati Mwanakwetu anashituka kutoka usingizini alikaribisha
na wimbo wa MSALITI ambapo
Mwanakwetu ulimvutia mno. Mwanakwetu alitekwa na wimbo huo kutoka hapo alipo
hadi mwaka 2014-2015 na kulikumbuka tukio moja la kweli.
Muziki huo huo wa runinga hiyo sasa ulikuwa burudani kwa Mwanakwetu
na baadaye ulichezwa wimbo wa pili wa Akli Kiba na Christian Bella NAGHARAMIA.
Hapo hapo Mwanakwetu alisikiliza na
kuutazama wimbo huo kwa ndimi zake, wimbo huo ulimsaidia sasa Mwanakwetu
kutosikia tena kelele mbli zilizobaki ambazo ni mashimo ya barabara na zile ya
mazungumzo ya abiria ndani ya basi hili.
Wimbo huu ulimvutia mno Mwanakwetu kwa
kuwa watu wote wanaonekana katika video hiyo anawafahamu kwa karibu, yaani Al-wataani Ali Kiba , mkongwe Christian Bella na hata Natasha
ambaye ni mrembo maarufu sana Afrika ya Mashariki.
Mwanakwetu alishitukia tu anaimba
wimbo huo kwa sauti baada ya mzuka na mdadi wa wimbo huo kumjia bila kufahamu.
Kumbuka msomaji wangu Mwanakwetu
anasafiri na yu yupo ndani ya basi na abiria kando yake ambaye alikuwa mama
mmoja mtu mzima akasema baba naona umevutia na wimbo huo?
Alijibu, naam mama
Mama huyu akauliza, umevutiwa na
nini?
“Nimevutiwa na mkomonzio (rhythm) ya wimbo huo,nimevutiwa na sauti za
waimbaji wake na pia nimevutiwa na hata mrembo Natasha anayeonekana katika
video hii.
Kikubwa mama nimevutiwa zaidi kwa kuwa video hii imewakusanya raia kutoka
mataifa matatu maarufu ya Afrika; Ali Kiba –Tanzania, Christian Bella -Congo na
Natasha-Kenya.
Hapa kila msanii ametimiza wajibu wake vizuri. Mathalni Kiba kaimba
vizuri na mawimbi sauti yake yanavutia, Bella anaongoza vizuri sauti za wimbo
huu, naye Natasha namna anavyoonekana tu anavutia sana na kuinogesha video hii.
Hapa kila mmoja kawajibika ipasavyo.”
Mama huyu ambaye
alionekana na uelewa mkubwa wa muziki akauliza,
“Baba huu wimbo ni maarufu Congo,
Kenya na Tanzania?”
Mwanakwetu akajibu
ndiyo mama.
Wimbo huo uliendelea
kuchezwa katika runinga hiyo.
“Wewe eeeee
Unamjua huyu demu, Ohhh Nashindwa kuvumulia
Huyu demu kanipagawisha,
Kila nikutana naye moyo wangu wadundadunda
Nataka tu kujuana naye, Awe kama arafiki wangu
Hapo moyo wangu utatulia aaaah,
Bell acha ubishi, Mvumilivu hula mbivu ...”
Kumbuka tu msomaji wangu
Mwanakwetu anasafiri, akitokea Malya kwenda Mwanza na mara ukachezwa wimbo
ambao Mwanakwetu hakuvutiwa nao.
Hapo hapo Mwanakwetu
akili zake zikahamia katika kelele ya tatu ambayo ilikuwa ni mazungumzo ya abiria
hao ndani ya basi hili.
Kwanza kukawa na sauti
mbili za abiria wakizungumzia rais mzuri wa Tanzania ajaye wakisema bado hajazaliwa,
abiria mwingine akisema hata ubunge hajapata, labda baada ya miaka 25 ijayo, na
pengine bado anasoma. Abiria mwingine akasema kuwa zamani Makamu wa Rais
alikuwa anajulikana lakini sasa Makamu wa Rais hajulikani kabisa. Abiria
mwingine akasema yaani juzi mama yetu Samia kaja Mwanza lakini idadi ya watu
ilikuwa ndogo watu wachache, idadi hiyo imemtia aibu Rais Samia.
Kumbuka msomaji wangu
safari inaendelea na kwa bahati mbaya nyimbo zilizoendelea kuchezwa katika
runinga ya basi hilo hazikumvutia tena Mwanakwetu, huku sasa abiria wenzake na
Mwanakwetu wakishika usukani wa mazungumzo hayo yaliyomteka Mwanakwetu.
“Kuna siku nilipanda costa, kuna mama
mmoja alisema jamani Samia anaupiga mwingi, aaah wanawake wenzake wakapiga kelele
wakamuomba konda wamshushe mama huyu katika basi hilo kwa kumrudishia nauli
yake na kumpa pesa nyingine ya nauli kutoka kwa akina mama abiria waliokuwa wanauza
mboga mboga.”
Haya yalisema na
abiria mwanaume ndani ya basi hili.
Msomaji wangu mazungumza
yanaendelea katika basi hili ,
“Walisema bwawa bado halijajaa, sasa
wanasema bwana lina maji ila machafu, zamani walisema maji hayajai katika bwawa,
zamani walisema kuwa bwana likikamilika tutaweza kuuza umeme hadi nje ya nchi.
Kwani tuna bwana moja au yapo
mangapi?, lipo la Mtera , lipo ... Lipo na ... na lingine la wapi?
Jamani kwani mlizaliwa katika umeme? abiria
mwingine alisema”
Mwanakwetu safari
inaendelea huku Watanzania hao wakitumia haki yao ya uhuru wa kutoa maoni kwa
kuzinyumbua changamoto zao chini ya mwavuli wa Ibara ya 18 ya katiba ya Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania.
“... sukari inapanda bei tu, Jamani
Kisesa na kona ya Kayenzi sogea, haya Kisesa Kona ya Kayenze nakuomba usogee
huko nyuma, wale wa Kisesa kona ya Kayenze huko nyuma, (tupoo ) haya sogea mama
bonge...”
Safari inaendelea na
basi hili kufika Nyamhongoro na hapo abiria wote kushuka nayeye Mwanakwetu
kushuka zake vizuri na alijaribu kuongea na mama mmoja ambaye alikuwa akiongea
ndani ya basi hilo na kumuuliza mbona mnalalamika sana?
(MAONO YA ABIRIA WENZAKE MWANAKWETU KAMA YALIVYOREKODIWA)
Mama huyu alijibu haya.
“Unajua hata katika ndoa, namna
unavyoanza ndiyo utakavyomaliza, kumbuka ukianza vizuri, utamaliza vizuri na
ukianza vibaya utamailiza vibaya, yangu hayo baba.”
Mwanakwetu alipomaliza
kuongea na mama huyu alipanda daladala kuelekea NHIF Buzurugwa na kupatia kadi
ya mwenza wake na kurudi alipotoka.
Je siku ya leo
Mwanakwetu anasema nini?
Mwanakwetu aliyafuatilia
kwa karibu mazungumzo hayo ya safarini yake juu ya abiria wenzake.
Mwanakwetu amejifunza
kitu japokuwa abiria hao walikuwa wakitoa maoni hayo, kwa hakika watu wengi walikuwa
kimya, hakuna aliyeweza kuinua mdomo wake na kusema tofauti labda yule tu
aliyesema haya,
“Kwani
nyinyi mmezaliwa katika umeme?”
Zamani katika vyombo
vya usafiri panapokuwepo na hoja za kisiasa kulikuwa na hoja pande mbili
zinazoshindana waziwazi. Hilo Mwanakwetu anasema kwa ushahidi maana alianza kupanda
mabasi ya jumuiya kama vile UDA& daladala akiwa mdogo Shule ya Msingi akitokea
Mbagala kuelekea Mnazi Mmoja katikati ya jiji la Dar es Salaam.
Swali ni kwanini pande
mbili zinazoshindani hazipo kwa hivi sasa? Pia katika basi hili alilopanda
Mwanakwetu sauti zilizosikika sana ni za akina mama wakilalamika na pia
zilikuwa ni sauti za juu ,wanaume katika basi hilo walikuwa wengi na walisema na
kama waliongea kuunga mkono tu hoja au kuwatajia vituo vya basi, mijadala yote
ilianzishwa na wanawake au wanaume kutoa mifano kidogo.Hayo ni maswali ambayo
Mwanakwetu anayatafutia majibu yake.
Mwanakwetu anatambua
kuwa Rais Samia Suluhu Hassan ndiyo kiongozi wa taifa letu, vyovyote
anavyongoza hilo ni jambo letu Watanzania sote. Inawezekana yupo ambaye
ameshagushwa na Rais Samia katika utendaji kazi na kuyaona maendeleo, kwa hiyo
anapomsifia hilo siyo kosa anayeeleza mazuri aliyoyaona yeye kwa nafasi yake
hatupaswi kumtenga na kumshusha katika basi. Mwanakwetu anaamini kuwa yapo
mengi mazuri ya Rais Samia hata huo uhuru wa kuyadilia haya na amani ya taifa
letu.Kila anayetoa maoni yake tumpe nafasi hiyo, tunapaswa kuvumiliana.
Kumbuka msomaji wangu
katika safari hiyo Mwanakwetu aliona video kadhaa za nyimbo mbalimbali lakini
yeye alivutiwa na nyimbo za Christian Bella na pengine wapo abiria ambao
hawakutiwa na nyimbo hizo, bali walivutiwa na nyimbo zingine. Huo ndiyo ubinadamu
ulivyo, tuvumiliane tu hadi tutafika salama mwisho wasafari yetu kama ile ya
Mwanakwetu ya kutoka Malya kwenda Nyamuhongolo Mwanza.
Kikubwa katika safari
hiyo Mwanakwetu aliupenda wimbo wa NAGHARAMIA ambao Ali Kiba , Christaan Bella
na Natasha kila mmoja alitimiza wajibu na kuifanya video hiyo kumtoa usingizini
muungwana Mwanakwetu, hivyo hivyo kwa wasaidizi wa mhe Rais Samia wanapaswa kufanya
kazi wa jitihada zote kufika malengo ya taifa letu. Kila mmoja akitimiza wajibu
wake hapo ndipo video yetu itakuwa nzuri na Tanzania yetu itapendeza na kila
mmoja kujivunia matunda ya taifa hili.
Mwanakwetu Upo
Kumbuka sana msomaji wangu,
“Namna Unavyoanza Ndivyo
Utakavyomaliza.”
Nakutakia siku Njema
0717649257
Post a Comment