IBEBENI MISALABA YENU-PADRI MSIGALA

 


Adeladius Makwega-DODOMA

Wakristo wameambiwa kuwa IJUMAA KUU ni siku muhimu kuliko zote kwao maana ndipo Yesu Kristo alipoonesha unyenyekevu mkuu wa kuubeba msalaba na kukubali kufa kifo cha aibu , cha dhalili na cha unyanyasaji wa hali ya juu, kuliko matukio yoyote yaliyotokea na yatakayotokea katika ulimwengu huu.

Hayo yamesemwa na Padri Godian Msigala, Paroko wa Parokia ya Chamwino Ikulu, katika Kanisa la Bikira Maria Imakulata –Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma, katika mahubiri ya misa ya hii iliyoanza saa 9 Alasiri na kumalizika saa 12. 00 Jioni ya Machi 29, 2024.

“Jumapili ni siku ya ushindi wa Kristo, ni kweli lakini ushindi huo ni baada ya unyenyekevu mkubwa wa Kristo, kufa kifo cha unyanyasaji katika IJUMAA KUU.

Kila mmoja wetu siku hii utaona anakumbuka kwenda kusali maana anaifungamanisha na maisha na mahangaiko yake ya kila siku.”

Katika misa hii Padri Misigala alitilia maanani mambo manne ;Yesu Kristo, Petro, Mama Maria na Msalaba.

Akifafanua mambo hayo moja baada ya lingine alisema kuwa unapomtaza Yesu Kristo alikuwa ameshapigwa mijeledi 39 na mwili wote umejaa damu lakini alibaki kusimamia ukweli wake tangu mwanzo wa mateso hadi tamati.

Je mimi na wewe tunasimamia ukweli?

“Mara nyingi watu waovu, wakiona huo ukweli mwisho wa siku unamuangamiza, huwa wanabadili gia angan, hapana, Yesu hakubadilika gia angani.”

Alipomtazama Petro Paroko huyu alisema alikuwa mpenda kutumia nguvu, alikuwa jamii ya watu wa mabavu lakini nguvu zake hazikuwa na msaada wowote.

Padri Msigala aliwaomba waamini wake wasipende kutumia mabavu mara zote wawe na wingi wa hekima.

“Mtu kasogeza mpaka wa shamba lako, acha mabavu, kuwa na subira maana subira yavuta heri.”

Pia mahubiri hayo yalimtazama Mama Bikira Maria kuwa alioneshwa mtoto wake yu msalabani, akivuja damu hilo jambo linalomuumiza sana mama kwa mwanaye aliyemzaa, kumtunza na kumlea tangu utoto wake.

Yesu alimwambia Yohane, mtazame mama yako. Funzo hapa jamani tunapopitia magumu tusisite kupitisha maombi yetu kwake.

Padri Msigala alimalizia mahubiri yake kwa kuelezea juu ya Msalaba, akiomba kila mkristo kukumbuka kuubeba msalaba wake bila ya kuchoka.

“Siyo kuichagua misalaba hiyo, tusiseme huyu anatusumbua kwa ujinga wake, hapana lazima tuibebe hiyo misalaba bila ya kuchoka.”

Mahubiri hayo yalimazika na misa iliendelea kwa hatua zingine za Misa ya Ijumaa Kuu

Kwa hakika misa hiyo ilifanyika kwa amani na utulivu, huku mvua kubwa lliyoambatana na radi na ngurumo za hapa na pale ikinyesha tangu katikati ya misa hadi mwisho, nao waamini waliokuwa nje ya kanisa hilo wakiloa.



 

 

 

 

0/Post a Comment/Comments