MAPISHI MWIKO MKUBWA

 



 Adeladius Makwega-KILIMATINDE

Siku moja Mwanakwetu alibanwa sana na njaa, kwa hiyo alitafuta mboga na kuichemsha haraka haraka mekoni, ilipoiva hakuiunga, aliichukua kama ilivyo nakuiweka kando ya jiko lake la kuni lenye mafiga matatu.

Kisha akachukua sufuria na kuiweka maji mekoni, mara baada ya dakika kadhaa, maji haya yalichemka, akauweka unga katika sufuria hiyo ili ausonge ugali.

Wakati ameshaweka unga kwenye maji yanayochemka, akageuka kuuchukua mwiko wa kupikia ugali wake, alitazama katika kichanja chake hakuuona kabisa, tafuta huku na kule mwiko hauonekani .

 

“Mwiko umekuwa na miguu?”

Mwanakwetu alijisemea moyoni,  leo anapika kwa kutumia nini? Kijiko au upawa wa chuma?

Mwanakwetu anajiuliza maswali haya huku maji yenye unga mekoni yanatokota kwa juhudi zote. Mwanakwetu akajipa majibu  juu ya kijiko na upawa wa chuma,

 

“Hivi vyote vinashika moto, unachosongea ugali huwa hakishiki moto.”

Ninafanyaje? Akili yake ilijiuliza mno, ahh gafla kwa mbele yake kwenye kona na pahala anapopikia akauona mwiko mkubwa, huku chini yake kukiwa na sufuria kubwa na makalai kadhaa ya mapishi katika shughuli.

Hapo hapo Mwanakwetu akamkumbuka mpishi mmoja wa shughuli wakati wanasoma aliyekuwa anapika siku za mahafali, huyu jamaa alipika kwa kutumia sufuria za shaba pale UPANGA Dar es Salaam mzee ALI MAPILAU.

Hapo hapo bila ya kuchelewa akauvuta mwiko huo, huku vyombo hivyo vikipiga kelele,

 

“Kwaaaaaaaaa!”

Alipoutoa tu akauosha haraka haraka na kuanza kuusonga ugali wake.

Kwa kuwa mwiko huu ulikuwa mkubwa na ugali ulikuwa wa mtu mmoja, basi mwiko huu wa kupikia sufuria la watu kama mia uliukamata ugali vizuri na kuugeuza bila tabu na hata alipokuwa anautumia kuusagasaga ugali ili kuondoa mabonge mabonge yenye unga, mwiko huu ulifanya kazi hiyo vizuri sana.

Wakati anaendelea kuusonga ugali huu, akawa anajiuliza huu mwiko wangu mdogo umekwenda wapi? Na huu mwiko mkubwa ulifikajefikaje hapa kwangu? Au Mwanakwetu nimeshakuwa msaidizi wa Ali Mapilau?

Baada ya muda, huku akiusonga ugali huo kwa juhudi zote,  alipata majibu kuwa mwiko mdogo pengine ameutupa na uchafu jalalani.

Swali lililokabaki lilikuwa vipi uwepo wa mwiko mkubwa nyumbani kwake?


 (Binti Mkomangi)

Majibu yalimjia;

“Nilipokuwa kijana, bibi mzaa baba Hedwiki Omari Binti Mkomangi aliniambaia kuwa katika nyumba yako yoyote ile, hakikisha unakuwa na mikeka kadhaa maana tunakufa muda wowote, akifa mtu mnamfunga katika mkeka haraka haraka kumpeleka mochwari.

 

Pia uwe sufuria kubwa, mifuniko upawa na miko mikubwa kadhaa, kwa maana sherehe na msiba ni lazima na hizi shughuli ili zisiwe dharura  lazima uwe na vitu hivyo.

 

 Unaweza kuamshwa asubuhi na hodi, kundi la watu wanakuja kulipa maali ya binti yako, hauwezi kuwafukuza , hapo hapo nyumba kwako muda huo huo nyumba inageuka sherehe.”

 

Hilo likasababisha Mwanakwetu anunue  vifaa hivyo.

Mwanakwetu anasonga ugali wake kwa kutumia mwiko mkubwa, akasema hapa akija mtu akanikuta ninavyousonga ugali wa mtu mmoja kwa mwiko wakupikia watu mia atasema,

 

“Katekista Makwega mbona unafanya israfu? Mwiko mkubwa chungu kikubwa.”

 

Kumbuka msomaji wangu Mwanakwetu yupo anapika ugali wake, alipomaliza akautenga na kuanza kula ugali hu polepole tonge moja baada ya lingine, bila tabu na ulikuwa ugali mtam, nakuuma sikio msomaji wangu.

Mwanakwetu siku ya leo anasema nini?

Kwa kuwa mapishi ya ugali ule yalivyokuwa matamu, Mwanakwetu akatoa agizo nyumbani kwake kuwa tangu siku hiyo ugali unaolika kwake ni wa mapishi ya mwiko mkubwa.

Ugali wa mwiko mkubwa  msomaji wangu una sifa kubwa tano;

“Kwanza lazima uive, pili huwa hauna mabonge mabonge, tatu chungu chake kinachopikiwa hakiungui, hata wale mabingwa wa kula ukoko wanajinoma kwa kupata ukoko usioungua na tano na mwisho atakayeuonja tu lazima ale tangu tonge la kwanza hadi mwisho hapo hakuna kukinai”

Je yupo anayediriki kushindana na Mwanakwetu anayepika ugali kwa kutumia mwiko mkubwa?

Ha ha ha ha ha ha ha, nicheke mie Mwanakwetu,

Jibu lake hayupo.

Labda, tena na tena, labda mwanafunzi hodari wa Mwanakwetu na aliyefuzu madarasa yote.

Hata hivyo, huyo mwanafunzi hodari (yeye) atabaki kuwa mwanafunzi wa Mwanakwetu.

Mwanakwetu upo?

Kumbuka haya ni Mapishi ya Mwiko Mkubwa.

Nakutakia siku njema.

makwadeladius@gmail.com
0717649257


 

 

 

0/Post a Comment/Comments