WATU WANAJISHIKA VICHWA

 


Adeladius Makwega-DUMILA

Msomaji wangu nakuomba siku ya leo twende pamoja na mimi kwa kuwatazama Watanzania wawili ambao wana majina yanayofana lakini wakiwa na umri tofauti kizazi tofauti ambao kwa hakika hawajawahi kukutana zaidi ya mdogo kusimuliwa habari za mkubwa, huku mmoja akiwa hai na mkubwa akiwa mfu, amelala usingizi wa milele.

Mwaka wa  2010 baada ya Uchaguzi Mkuu kukamilika na kuelekea 2011, ndugu Jakaya kikwete ndiyo ameshinda uchaguzi mkuu wa kipindi chake cha pili, akianza kuunda serikali yake

Mwanakwetu alikuwa katika Mkahawa wa RTD ambapo ulikuwa ukiendesha na Chama Cha wafanyakazi cha RTD.

Hapo Mkahawani kulikuwa na watu sita ;

“Wahudumu wawili wanawake wazaliwa wa Soni Lushoto Tanga, msimamizi wa mkahawa huo na mhasibu wa RTD SACCOS aliyefahamika kama Swedi huyu alikuwa nadhani Mmanyema wa Kariakoo, alikuwepo Mtangazaji wa (PRT) TBC FM wakati huo Hassan Mbazigwa huyu akiwa Muha& Mmanyema wa Kariakoo , alikuwapo Mtangazaji Mkuu& Mtayarisahaji Vipindi Mkuu wa RTD marehemu Abisai Steven huyu nadhani alikuwa Mchaga& Mmeru na mwisho aliyekuwepa huyu huyu anayekusimulia-Adeladius Makwega.”

Katika mkahawa huu palikuwa na spika inayorusha hewani matangazo ya RTD-TBC TAIFA na muda huo ilikama kama saa 10.00 ngoma za RTD za marehemu Morris Nyunyusa zikalia na taarifa ya habari kuanza kusomwa kutokea TBC Mikocheni.

“Rais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania Jakaya Mrisho Kikwete amemteua ndugu… kuwa Mkurugenzi Mkuu wa TBC, kabla ya uteuzi huo alikuwa…”

Mwanakwetu yupo katika meza moja na marehemu Abisai Steven na nadhania kabla ya kufika hapo mkahawani Abisai Steven alikuwa anawasimamia kina Mwanakwetu katika mojawapa ya kipindi kilichokuwa kinarushwa moja kwa moja hewani.

Mzee huyu akajishika kichwa kwa viganj vyake viwili , Akakaa kimya kwa muda alafu akasema maneno haya,

“Nawaambieni Ngojeni Muone.”

Mwanakwetu aliongea kwa kirefu na Abisai Steven hasa hasa hiyo ngojeni muone ya uteuzi uliofanywa na Rais Jakaya Kikwete dhidi ya TBC.

Masikini wa Watu Rais Jakaya Kikwete hajui watu wanafikiria nini juu ya uteuzi wake, mzee wa Msoga keshamaliza kazi, file la TBC lishapelekwa masijara huku pengine baadhi ya waungwani pengine wakimpngeza aliyeteuliwa na aliyefanya uteuzi huo.

Kwa hakika marehemu Abisai Steven alikuwa mtangazaji mwenye akili sana na mwenye maneno machache katika mazingira yasiyo rafiki, yakisindkizwa na sauti yake ya mikwaruzo ya kiutu uzima.

Akiwa TBC Abisai Steven alipenda sana kumtania mtangazaji mmoja ambaye aliwahi kufanya na RFA awali na hadi sasa yupo TBC TAIFA anaitwa Stella Setumbi. Kwa ambao hawamfahamu Bi Setumbi ni mke wa Mtangaji Roy Maganga ambaye nayeye alikuwa RFA zamani wakahamia TBC enzi ya TIDO MHADO nadhani Roy Maganga anafanya biashara zake lakini mtangazaji mzuri.

Mwanakwetu anamfahamu Stella Setumbi miaka mingi, kupitia kwa mdogo wake anayefahamika kama Carolyne Setumbi, hawa ni Wakwere wa Msoga maana Carolyne Setumbi na Mwanakwetu wamesoma Shahada ya Sanaa ya Habari pamoja kule Tumaini iringa.

Msomaji wangu nikuume sikio kuwa marehemu Abisai Steven alikuwa anapenda kuucheza wimbo unaofahamika kama Sifa za Stella nadhani uliimbwa na bendi ya Umoja wa Vijana-wa CCM -VIJANA JAZZ enzi ya akina William Lukuvi na marehemu John Gudinita.

Mwanakwetu kila aliposikia wimbo huo alimuuliza marehemu Abisai Steven,

“Bosi hapo unautafuta Ugomvi na Roy Maganga, unacheza nyimbo za kusifia wake za watu? Au unataka na sisi tucheze nyimbo za kumsifia bibi nyumbani? Hilo bosi halikubaliki na kwa  kufaya hivyo unakaribisha ndundi studio, studio ni sehemu ya amani ukiingia shida zako zote unaziacha nje.”

Watu wanacheka , wakisema Makwega waulize watu wa masijala ya RTD tujue jina la mke wa mzee Abisai Steven alafu tuzicheze kila siku nyimbo zenye jina hilo.

Msomaji wangu watu wanacheka, maisha yanasonga, hapo utawala wa nawaambieni ngojeni muone unaendelea

Mwaka 2016 Mwanakwetu alifika Lushoto hapo alikuta na kijana mmoja ambaye alikuwa Mfamasia wa Wilaya. Mwanakwetu akawa anaona jina katika makaratasi ya serikali Abisai Steven, Abisai Steven, hapo hapo akikumbuka zamu kukeshe usiku RTD.

Wakati huo yule Abisai Steven wa RTD alishafariki nadhani mwaka 2011,Mwanakwetu akamuita huyu kijana ofisii akamuulize je yukoje na marehemu Abisai Steven wa RTD?

“Baba yangu alimpenda mtangazaji huyu(Abisai Steven), hivyo nikapewa hilo jina nilipozaliwa tu, sijawahi kumuona lakini watu wengi huwa wananiuliuza hilo swali.”

Mwanakwetu akawa jirani na huyu kijana na ofisi yake ya Mfamasia wa Wilaya, Mwanakwetu alianza kufuatilia ufanyaji kazi wa mfamasia Abisai Steven. Ofisini kwake alikuwa na watumishi wawili Mmeru mmoja na Mkwere mmoja na mwenyewe watatu.

 Miongoni mwa watumishi waliokuwa wakifanya kazi kwa amani na kidugu ilikuwa ni ofisi ya mfamasia wa wilaya hii. Huyu mfamasia alikuwa ni kijana mdogo aliyeridhika na maisha. Mfamasia wa Wilaya ana safari nyingi kwa hakika hawa wasaidizi wake walikuwa wakisafiri safari nyingi kuliko hata mfamasia mwenyewe.

“Mkuu bosi ameniambia niende mimi hata hii safari ya nje.”

Watu Halmashauri wanashangaa maana kuna mabosi wengine kila safari kigulu na njia hadi wanaitwa VISHADA WATEMBEZI.

Hivi sasa Abisai Steven ndiye mfamasia wa Mkoa wa Manyara, Mwanakwetu anaamini kuwa Ofisi ya Mfamasia wa Mkoa wa Manyara wanafanya kazi kwa amani.

Mwanakwetu hajawasiliana na Abisai Steven tangu mwaka 2018 lakini kama yupo Tomaso na anabishana haya yanayosimuliwa afuatilie,

“Nawaambieni Ngojeni Muone.”

Siku ya leo Mwanakwetu anasema nini?

Katika utumishi wowote jamani tujitahidi mno kukaa na wenzetu vizuri, kinachopatikana tujitahidi kugawana, iwe pesa, iwe posho na hata visafari kinyume chake kila safari unakwenda wewe? Wapo watu wanachukia moyoni na mara nyingi hawasemi lakini moyoni wanakuombea ajali na hata unapopewa cheo wanajishika kichwa, wakimaani kuwa shida zitaongezeka.

Katika maisha usifanya watu wengine wajishike kichwa dhidi yako, hilo siyo jambo jema, dunia iwe sehemu ya furaha amani, utani vicheko kama ilivyokuwa kwa Abisai Steven mtangazaji na akina Mwanakwetu wakati ule.

Mwanakwetu Upo?

Watu Wanajishika Vichwa.

Nakutakia Siku Njema.

makwadeladius@gmail.com

0717649257


 

 

0/Post a Comment/Comments