MWANAMANJONJA HATAJWI MAPEMA.

 


Adeladius Makwega-MWANZA

Kati ya Septemba 15 hadi 24, 2021 Mwanakwetu alikuwa Mkoani Katavi katika shuhguli za Kiserikali ambapo aliyekuwa Naibu Waziri wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Bi Pauline Gekul alikuwa ziarani mkoani humo.

Eneo mojawapo ambalo Bi Gekul alitembelea iikuwa ni NSIMBO, hilo anakumbuka ambapo Kiongozi huyu alipokelewa na watu wengi na mbunge wa jimbo alikuwa mama mmoja.

Kutoka Wizara ya Habari walioambatana na Hadija Kisubi(Afisa Utamaduni Mwandamizi), Nyambi (Afisa Michezo Mkuu, dada mmoja kutoka Habari Maelezo(Afisa Habari) na Mwanakwetu(Afisa Habari Mkuu).

Naibu Waziri alikuwa na gari lake ndani yake akiwamo msaidizi mmoja na dereva.Huku gari la pili walikuwamo hawa maafisa na dereva wao alikuwa ni sanjenti mmoja wa JWTZ mzaliwa wa Iringa.

Miongoni mwa kazi zilizofanywa na Mwanakwetu ni kuripoti ziara ya Naibu Waziri kwa Vyombo vya Habari lakini pia usiku Mwanakwt aliyatayarisha makala maalum ya NGOMA YA MBUNGI.

“Mbungi ni miongoni mwa ngoma inazochezwa na makabila ya Wazaramo, Wandengereko,Wangindo na Wamatumbi, yakiwa ni makabila ndugu katika ukanda wa Pwani ya Afrika Mashariki kando ya BAHARI YA HINDI.”

 

Kwa kuwa Wazaramo, Wandengereko, Wamatumbi na Wangindo wanaoleana ni jambo la kawaida sana ngoma hii kutumiwa na makabila hayo yaliyopo katika mikoa wa Dar es Salaam , Pwani na Lindi,Mtwara na hata Morogoro. Jina lake kamili ni NTHIMINI lakini kwa wepesi inaitwa Mbungi na hupigwa na kuchezwa kwa siku nne Alhamsi, Ijumaa, Jumamosi na Jumapili kuamkia Jumatatu hapa ndpo wanafamilia na wanambungi wanainua jamvi.

 

“Ngoma hii inahusisha ngoma kubwa kadhaa na sahani maalumu ya shaba ambayo inapigwa ikitoa mlio maalumu huku ikichanganywa na nyimbo kadhaa za kuyapunga mashetani.

Ngoma hii ina sehemu kubwa mbili kabla ya ngoma kuanza ambapo wale wanaohitaji kupungwa mashetani wanatoa mialiko kwa wahusika juu ya huyu ndugu yao anayetakiwa kupungwa mashetani. Mwaliko utafika kwa wahusika alafu wanakikundi wanajulishwa kwa mdomo nyumba kwa nyumba alafu lazima mizimwi ikaombwe juu ya kazi hiyo inayokwenda kufanywa na Wanambungi.

 

Mizimwi au kinyamkera akishatoa kibali, basi zoezi la kwenda kuifanya kazi hiyo inaanza lakini inawezekana wakagundua kuna shida ndipo kafara zinatolewa na tambua kuwa Wamatumbi, Wazaramo,Wangindo na Wandengereko ni wafugaji wa kuku, bata na wanyama wadogo wadogo kama sungura tu kwa asili.

 

Hapa utaambiwa na fundi kalete kuku mweupe, kuku mweusi na kadhalika, hawa kwa asili si wafugaji wa ng’ombe, mbuzi na wanyama wengine ndiyo maana kafara zao zinaendana na hali ya jamii zao.”

 

Japokuwa kwa sasa hali imebadilika baada ya ujio wa wafugaji, wapo wanaofuga wanyama wakubwa. Lakini Mwanakwetu alitarajia kwenda huko maana kuna mtu anataka kumfungisha safari ili ya akatambua aina za kafara za makabla haya ya Pwani ya Tanzania.”

Msomaji wangu mpaka leo Mwanakwetu hajakwenda huko.


 

Wamatumbi wanayo ngoma yao nyengine ambapo hawatumii kifaa cha ngoma yoyote bali milio ya vishindo vya miguu, njuga na makofi inaitwa LINGWICHU. Hapo ni vishindo vya miguu, njuga na makofi tu na inachezwa popote pale atakapopatikana muanzishaji.

Kuna swali Mwanakwetu alijiiuza kwanini Wamatumbi kwenye sherehe za kawaida wanatumia ngoma yao ni Lingwichu inayotumia makofi, miguu na njuga wakati katika kupunga mashetani wanatumia ngoma ya Mbungi inayotumia ngoma kubwakubwa na sahani ya shaba?

Haya ni maswali ambayo Wamatumbi wanapaswa kuyajibu.

 

Kumbuka tu Msomaji wangu makala haya yanaandikwa na Mwanakwetu akiwa katika ziara ya Naibu Wazir wa Habari wakati huo Bi Pauline Gekul, Septemba 2021.

Mwanakwetu kwa mara ya kwanza aliiona ngoma ya  mbungi huko Kimanzichana-Gongoni ambako alikuwa akiishi na wazazi wake mwanzoni mwa miaka ya 1980.

.

“Ngoma hii inaulingano na ngoma ya Tokomile ambapo nayo ni ngoma ya vituko kidogo, huko ukipigwa ngomani hakuna kukimbilia polisi mambo yanaishia ngomani. Kunakuwa na ngoma kadhaa ndogo na kuna ngoma kubwa pia ipo aina ya sahani inayopigwa kwa kutumia vifaa maalumu ambapo inatoa sauti tamu.”

Haya yanathibitshwa na Bi Mariam Selemani Binti Kilemile ambaye ni Mzaramo wa Mkenge, huko Mkuranga Pwani nchini Tanzania.


 

Ngoma hii ni ya watu wazima tu na mara chache chache huchezwa hadharani.

Mwanakwetu anakumbuka hata enzi za Mbunge wa Kisarawe marehemu Profesa Kigoma wakati huo Profesa Malima katika ziara zake jimboni alikaribishwa na ngoma ya Mdundiko, Mkinda na Singenge. Huku Ngoma ya Mbungi hakuwahi kupewa nafasi hii si ngoma ya hadhara.

Wakati wa maandalizi ya Mbungi, Kabla ya ngoma hiyo kuanza huwa anatumwa mjumbe maalumu kwenda kuwajulisha juu ya ngoma yao (Mbungi) kualikwa katika shughuli fulani kama ilivyodkezwa awali . Mwaliko huo ambao hutumwa kwa kiongozi wa ngoma na mara nyingi huwa mtu mzima.

Kiongozi wa ngoma naye huwajulisha wenzake juu ya mwaliko huo na mara zote ujumbe hufikishwa kwa kila mwanangoma hiyo nyumba kwa nyumba mdomo kwa mdomo.

Safari ya kwenda kwa fundi huwadia, fundi anajukumu la kuangalia hali ya mwaliko ilivyo na itakuwaje siku ya tukio hilo, hii ni ramli ya kuangalia siku ya tukio ngoma itakuwaje? Siyo mnakwenda katika ngoma mtu anafariki ngomani, hapa inapingwa ramli.

 

“Fundi (mganga wa kienyeji) huwa na masharti kadhaa ambayo yanatakiwa kufuatwa wakiwa katika tukio hilo. Inawezekana fundi akiona kuwa ngoma hiyo itakuwa na balaa(NUKSI) basi kiongozi wa kikundi hicho au wanakikundi wote wanatakiwa kuleta kuku wa rangi anayoitaka mganga ili kuyaweka mambo sawa na kuondoa mikosi iliyoonekana kwa fundi. Masharti yatatolewa ikiwamo wakiwa katika tamasha hilo kutoshirikiana tendo la ndoa kwa wanakikundi hicho na mtu yeyote hadi ngoma itakapomalizika, au wale ambao wataonekana kuwa NUKSI kutoshiriki ngoma hiyo au baadhi ya wanakikndi kukaazwa kunywa pombe na baadhi ya vyakula.”

 

Haya yanathibitishwa na Said Hamisi Bini Magombeka ambaye baba yake alikuwa miongoni mwa wachezaji wa ngoma hii kutoka Mbagala Kizuiani.

Hapo ndipo safari inafungwa kuelekea katika onesho la ngoma ya Mbungi na mara nyingi ngoma huanza Alhamisi, inachezwa Ijumaa, Jumamosi na Jumapili ndiyo hitimisho kama ilivodokewa awali huku masharti ya fund yakiheshimika mno.

 

Msomaji wangu kumbuka makala haya yalitayarishwa huko Nsimb Katavi katika ziara ya Bi Pauline Gekul;

“Kama nilivyokujulisha awali ngoma ya mbungi inaheshimu mno masharti ya mizimu na maelekezo ya fundi, kinyume chake yule anayekiuka kwanza anafukuzwa kundini, anaweza kufikwa na mikosi kadhaa ikiwamo hata msiba.”

Alhamisi itapita salama, ijumaaa salama, jumamosi salama salimini na jumapili jioni ndipo wakati wa MANJONJA.Manjonja maana yake ni wakati wa kutoa burudani uwanjani wazi wazi ambapo vituko kadhaa vinafanyika hadharami.

 

“Vifaa vyenye taswira ya sehemu za siri za binadamu vinaonyeshwa huku watu wakicheza na watazamaji wakizunguka eneo hilo hasa chini ya mti mkubwa kwa mtindo wa duara. Kuna wakati MWANAMANJONJA anatembea uchi wa mnyama kabisa hapo ndiyo ile kumwaga radhi kunafanyika.”

Msomaji wang hii ni ngoma ya matambiko na ni ngoma ya kupunga mashetani Manjonjaa huwa ni vituko tu yaani kuwachekesha watazamaji tu na havina uhusiano wowote na kupunga mashetani hapo ni kuhitimsha shughuli maana aliyepungwa mashetani yamemtoka jamii inasherehekea hadharani. Siku hizi ngoma hii inakuwa adimu kutokana na sheria za sasa za nchi yetu.

Bi Mariam Seleiman Binti Kilemile anasema haya,

“Wakati ukifika miongoni mwa mwanakikundi huwa ndio anachaguliwa kuwa MWANAMANJONJA (kumwaga radhi) Katika tukio hilo la manjonja wanakikundi hicho ujitahidi kumtafuta mtu ambaye hapo kilingeni si nyumbani kwake, hilo ni sharti kubwa na hata kule kwa mganga linasititizwa kwa kina.Yule anayemwaga radhi kwa kuwa kwake ni mbali hilo linampa nafasi ya kuweza kumwaga radhi vizuri na kwa amani kubwa.”

Jina la mmwaga radhi(Mwanamanjonja) huwa linatajwa kwa mganga kule kwa sri wanapojiandaa ili kuweza kusaidia ngoma yao kufanyka vizuri.”

Jina la mwanamanjonja siku zote halijulikani hadi hiyo jumapili jioni huku watazamaji wa ngoma hii wakitambua kuwa siku ya mwisho kutakuwa na manjonja na kuna mtu atamwaga radhi tu na wanajamii wakiisikia midundo ya ngoma ya mbungi inalia siku ya kufurahi ni si ya MANJONJA na huwa jumapili jioni kuazia saa 9 hadi 12.

Swali moja ambalo Mwanakwetu aliulizwa na waliyoyasoma makala haya ni Je kwanini Ngoma ya Mbungi inaogopa kulitaja jina na MWANAMANJONJA mapema?

 

“Hilo linasaidia sana kufanikisha ngoma katika hatua zake zote wakiwa salama. Kujulikana kwake mapema ngoma inaweza kupasuka au kuungua kwa moto wakati wa kuwambwa, miongoni mwa wanangoma anaweza kuumwa au kugongwa na nyoka na mabalaa mengine kama ya ugomvi au kufumaniwa, wakiwa kazini  maana vinginevyo kazi ya kuyapunga mashetani itakwama .”

 

Jibu hilo lilitolewa na Bini Magombeka naye Mwaakwetu kuwaeleza wasomaji wake.

Kumbuka Mwanakwetu yu safarini

Maafisa hao wa Wizara hii ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania walimaliza kazi na kurudi zao Dodoma wakiongozwa na Naibu Waziri wao, Mpendwa wao, dada yao wa wakati huo Bi Pauline Gekul.

Mwanaketu anasema nini siku ya leo?

Kwa hakika Mwanakwetu kwanza kabisa amemkumbuka dada yake mpendwa mhe Pauline Gekul ambaye sasa ni mbunge wa Babati.

 

“Popote ulipo mhe Pauline pokea salaam za Mwanakwetu kwa heshima na taadhima.”

Makala haya yana  maelezo haya,

“Jina la Mwanamanjonja huwa linatajwa kwa mganga kule kwa sri wanapojiandaa ili kuweza kusaidia ngoma yao kufanyka vizuri na litajulikana siku ya manjonja tu.”

Wazaramo, Wamatumbi, Wangindo na Wandengereko kumtaja MWANAMANJONJA mapema ni kosa kubwa na usijaribu kuthubutu hilo. Kwani hilo la kumtaja mapema linaweza kusabisha yeye aliyetajwa (mwamanjonja) na kundi zima la ngoma ya Mbungi kulogwa na mahasidi wa sherehe hiyo hata kutupiwa jini au kuchukuliwa na chunusi na pengine kusababisha msiba na hata kushndwa kuifanya vizuri kazi ya kupunga mashetani.

Haya ni mambo ya wazee wetu kuwa MWANAMANJONJA hataji mapema, hilo Mwanakwetu analitoa tena kama kukumbushana tu Unapotaka ngoma yako inoge/ifane mwanamanjonja asitajwe mapema, hili ni shabaha ya mwisho ya makala haya.

Mwanakwetu Upo?

Kumbuka tu

“MWANAMANJONJA HATAJWI MAPEMA.”

Nakutakia siku njema.

makwadeladius@gmail.com

0717649257


 



 

0/Post a Comment/Comments