Adeladius Makwega-MWANZA
“Kwa mfano wanajadili swali, anataka wote kundini wawe wamelielewa swali hilo kwa kina, kisha wanaanza kuyatafuta majibu pamoja, wakiyapata anahakikisha kila mmoja wao aweze kulijibu swali hilo vizuri, katika pointi kumi anahakikisha kila mmoja angalau anajua pointi hata saba ambazo hizo zitampa alama nzuri wakati wa majaribio na mitihani ya mwisho, Mzee Yahaya ana roho ya kipekee sana.”
Maelezo haya yananukuliwa na Mwanakwetu akiwa safarini kutoka Malya kwenda Mwanza, ambapo abiria watatu wapo mbele ya Mwanakwetu wanaongea kwa uhuru na kwa nguvu, hilo lilimvutia mno Mwanakwetu ambapo baadaye alibaini kuwa hao walikuwa Wakurufunzi(wanachuo) wa Chuo Cha Maendeleo ya Michezo Malya (MCSD). Mzee Yahaya ni kiongozi wa kundi lao, hata mimi huwa nakuwa na amani kama nikipangiwa kundi moja na Mzee Yahaya hapo najua Jahazi Haliwezi Kwenda Mrama. Wanafunzi hao waliovalia nguo za michezo waliendelea kuzungumza juu ya Mwenyekiti Bora wa Diskasheni Darasani Mwao,
“Kuna siku walipewa kazi yakuwasilisha darasani, Mzee Yahaya akasema,
‘Jamani eeeh tunakwenda kusimama pale mbele, hizo pointi ndiyo majibu yetu, kila mmoja akumbuke pointi zote, kama kuna neno haulifahamu maana yake ingia google mapema utapata maana yake jamani tuwe na uelewa wa pamoja, pale mbele ukiingia chake tumeingia chaka sote.’
Jamaa walifanya vizuri.”
Msomaji wangu kumbuka Mwanakwetu yu safarini na hao wanaongea wapo mbele yake na kwa alivyokaa ilikuwa ngumu wao kumtambua na kuwapa uhuru kabisa vijana hao Mwanakwetu alitoa shuka yake ya Kimasai akaiweka begani na kujifunika usoni na akawa kama amelala kumbe masikio yake yaliendelea kunukuu mazungumzo haya.
“Mzee Yahaya ni mwadilifu, ni muungwana, ni mnyenyekevu na mkarmu kwa hata kitu kidogo alichonacho. Unajua pale kipind cha mitihani wanasoma tangu saa 2-7 usiku anaweza kuona fulani anasinzia Mzee Yahaya anatoa pipi anawagawia wana kundi wote, watapumzka kidogo alafu wanaendelea na majadiliano. Unajua haya masomo yetu yanatumia akili na nguvu kwa wakati mmoja. Hivyo mtu akisema kachoka tambua kachoka vyote.”
Mjadala huo uliendelea na safari ya kutoka Malya kwenda Mwanza inaendelea pia.
“Mzee Yahaya hapendi kuchelewesha mambo yake, anapenda kufanya kazi kwa wakati.”
Kijana wa kiume safarini ambaye aliongea mara chache chache akasema unajua kwenye haya mambo ya kusoma wengine tunahitaji kuchangamshwa ili mambo yaende na sote tufike salama Mzee Yahaya ni mahiri, binti aliyeketi mkono wa shoto akasema
“Mimi ninadhani hata ufaulu wake utakuwa mzuri, binafsi namuombea heri yule baba.”
Mjadala unaendelea, safari inanoga huku Mwanakwetu akitamani kumfahamu huyo Mzee Yahani ni nani? Huku akilini mwake ikimjia taswira iliyojengwa na Lady Jay Dee katika wimbo Yahaya,
Yahaya unaishi wapi,
Jina lako halisi nani?
Yahaya eeeehhh ,
Yahaya Yahaya Yahaya…
Taswira ya wimbo Yahaya wa Lady JD ikiwa tofauti na ya Yahaya wa Malya (MCSD) lakini hadi hapo hamfahamu ni nani? Safari hiyo inaendelea huku Mkongwe Mwanakwetu akinukuu neno kwa neno la Yahaya wa MCSD.
“Wakati ule tulikuwa likizo, kundi lao wanawasiliana katika mitandao ya kijamii, Mzee Yahaya akawaambia,
’Jamani eeeh matokeo yametoka, kila mmoja aangalie kama amefaulu au kama unarudia somo, asisite kurudi mapema kufanya mitihani ya marekebisho.’
Kweli kila mmoja alifanya hivyo baadaye kila mmoja aliombwa kwa hiari yake kuonesha ufaulu wake, waliofanya hivyo na kutiana moyo.”
Mjadala huo unaendelea na sasa basi hilo likafika Mabuki na kuingia barabara ya lami kuelekea Mwanza.Vijana hao wanaongea wakisema katika maisha yetu tunapokuwa katika jamii tusikae kihasahasara, tunatakiwa kukaa kwa umakini mkubwa si unaona leo hii tunamzungumzia Mzee Yahaya kesho tutazungumziwa sisi. Kijana kando yao akauliza hivi hilo kundi lao lina wanafunzi wangapi? Binti ambaye alikuwa mzungumzaji mkubwa alijibu,
“Pale yupo Said Kasana, Jovin Jemsi,Haji Mawanga, Simoni Mlenge, Ally Yusuph, Faraja Msigwa, Dorothea Peter, Rehema Mshani, Evodia Komba, Ezra Lupoli, Latuna Saluni na Yahaya Said (Mzee Yahaya Mwenyewe).”
Mwanawetu alipoyasikia majina haya akawa anayanuku vizuri katika shajara yake, huku Mwanakwetu akiwafahamu vizuri Faraja Msigwa na Ezra Lupoli ambao ni viongozi katika Serikali ya Wanachuo.
Kwa bahati mbaya kondakta alifika alipo Mwanakwetu na kumuamsha huku akidai pesa yake ya nauli. Hapo hapo Mwanakwetu alilipa shilingi 7000/- na vijana hawa mbele ya Mwanakwetu walikonyezana kwa kutanbua kuwa Mwanakwetu yupo nao. safarini na hawakuendelea tena na simulizi za Mzee Yahaya wa MCSD. Basi likafika Mwanza naye Mwanakwetu kushuka na kwenda kununua aichokifuata huko na baadaye siku hiyo hiyo Kurudi Malya huku Mwanakwetu alijiuliza mengi juu ya Mzee Yahaya wa MCSD ni nani?Baadaye alitambua haya;
“Yahaya Said ni Mwanachuo wa Stasahahda ya Michezo Malya (MCSD) mwaka pili atahitmu 2024. Huku akiwa ni kiongozi wa Umoja wa Vijana wa Kisilamu hapo chuoni yeye alikuwa ni AMIRI tangu mwaka 2023 hadi mapema 2024. Umoja wao wa vijana wa Kiisilamu kwa kipindi chote cha mwaka 2023-2024 umekuwa na sifa ya pekee ya kufanikisha shughuli zao zote kwa mujibu wa ratiba kwa uwezo wao mdogo, huku wakitafuta fedha kutoka vyanzo mbalimbali vikiwamo marafiki, huku sherehe zao za dini hapo chuoni wakipika vyakula na kula wanachuo wote bila kujali dhehebu. hilo likiwa tofauti na vikundi vingine vya dini.”
Mwanakwetu alipofuatilia zaid alibaini kuwa Mzee Yahaya ni mzaliwa wa Nzega, Mkoani Tabora alipata elimu ya Ualimu Chuo cha Ualimu Ndala huko huko Tabora na sasa ni Mwalimu katika Halmashauri ya Ifakara mkoani Morogoro.
Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?
Kwa hakika Yahaya Said Abdallah mwenendo wake unaonesha ni kiongozi mzuri tangu katika dini hadi katika jumuiya aliyopo, akitilia maanani motisha kwa wenzake rejea utoaji wa pipi, anaaminiwa na wenzake hadi wanamsimulia maisha yake safarini. Ukilitazama kundi lake la wanachuo 12 yeye akiwa mwenyekiti anao viongozi wawili kutoka serikali ya wanachuo, humo ukiangalia madhehebu ya dini utabaini kuwa Waisilamu ni Ally Yusuph, Said Kasana, Yahaya Said(Mzee Yahaya Mwenyewe), na Haji Mawana (Wote hao Waisilamu wa dhehebu la SUNNI BIN JAMAA) , Ezra Lupoli ambaye ndiye Katibu wa kundi hilo, yeye ni MPENTEKOSTI, kuna Evodia Komba, Rehema Mshani, Simon Mlenge, Jovin Jemsi na Latuna Saluni hawa ni Kutoka Kanisa la Kiinjili la Kiluthei Tanzania (KKKT) huku Faraja Msigwa ni MSABATO. Ukitazma vizuri Mzee Yahaya anaaminiwa vizuri na wenzake huku akipenda matokeo chanya ya kundi lake zima bila kumuacha nyuma yoyote miongoni mwao.
Mwanakwetu anashauri hasa kwa sasa ni vizuri taifa letu kuwatazama vijana wetu ambao wanafanya vizuri katika uongozi wa umoja wa makundi ya dini wapewe nafasi. waje kutusaidia kutuongoza maana hawa wana mioyo ya uwoga na kuheshimu maadili ya dini zao. Mwanakwetu pia anamuomba Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro amtazame huyu mwalimu Yahaya Said Abdallah kutoka katika halmashauri yake ya Ifakara anaweza kuwavushaa katika hatua moja kwenda nyingine ya mambo ya umma.
Mwanakwetu atafunga safari hadi Dar es Salam kumtafuta Binti Machozi, Komando Lady JD ili amuimbe huyu Mzee Yahaya wa MCSD.
Mwanakwetu upo?
Kumbuka,
“Jahazi Haliwezi Kwenda Mrama.”
Nakutakia siku njema.
0717649257
Post a Comment