Adeladius Makwega-MWANZA.
Katika mojawapo ya ukanda wa video Paulo Makonda alikuwa akijibu yale yaliyosemwa na Bi. Rose-Mary Chatanda na kujibu yale aliyodai yanasemwasemwa katika mitandao ya kijamii akionekana Paulo Makonda katika ofisi ya umma nadhani wilaya mojawapo ya mkoa huo, kando yake kunaonekaa wapo Watumishi wa Umma wakipiga makofi, na kucheka, kushangilia na kuunga mkono yale yaliyokuwa yanasemwa na kiongozi huyu.
Katika hali hiyo inavyoonekana katika ukanda huo wa video, Mwanakwetu anakuomba asafiri nawe msomaji wake katika visa VITATU nia kulenga shabaha katika kubadilisha mwenendo huo maana jamii ya Watanzania inafuatilia mwenendo wa Paul Makonda na hilo halina mashaka hata walio naye kando wanaingia katika mkumbo huo, hususani Kamati za Ulinzi na Usalama za maeneo haya tangu Wilaya hadi Mkoa.
Siku ya leo Mkongwe Mwanakwetu atajitahidi kujenga dhana katika mifano ya kina ambayo ameipa utambulisho wa herefu A, AA na AAA.
Mfano A;
“Huyu Mfalme Charles wa III wa Uingereza wa sasa mwaka 2005 alifunga safari kwenda Vatikani kumzika Papa Yohane Paulo II(Mtakatifu Yohane Paulo II) aliyefariki Aprili 2, 2005.Viongozi wengi duniani walifunga safari huko na miongoni mwa waombolezaji zaidi ya milioni 2 katika Viwanja Saint Peter Square Aprili 8, 2005 alikuwa Rais wazamani wa Zimbabwe Robert Gabriel Mugabe, safari ya mzee Mugabe kwenda mazikoni Vatikani ilikuwa imezungukwa na mizengwe hasa taifa lake kuwa na vikwazo vya kusafiri angani na vikwazo vya kiuchumi, huku ikiaminika kama atafanya hivyo atadunguliwa angani.
Mzee Mugabe alisafiri kibabe hadi kuingia katika viunga vya Vatikani kwenda kuzika na alipoulizwa alijibu kuwa lazima amzike kiongozi huyo wa kiroho mwenye heshima tele.
Kumbuka Mtoto mkubwa wa Malkia Elizabeth (Charles) aliagizwa na mama yake kushiriki maziko hayo kumuwakilisha.
Vyombo vya habari vya Uingereza vilimuonesha Mtoto wa Malkia akimpa mkono Robert Mugabe. Jambo hilo lilileta maneno mengi dhidi ya Charles mwenyewe kwa raia wake vipi haufahamu msimamo wa taifa lake dhidi ya Zimbabwe? Kumbuka hiyo ni familia yenye Uingereza yao, jamii inaihoji.
Nakuomba msomaji wangu tukitazame kisa hiki cha pili. Mfano AA;
“Jaji yu mahakamani katika kiti chake, mtuhumiwa yupo katika kizimba chake, askari, waendesha mashtaka, wazee wa baraza na wafuatiliaji wa shauri wameketi katika sehemu zao. Umri wa jaji ni mdogo kuliko umri wa mtumiwa. Jaji muungwana akamuita mtuhumiwa kwa jina lake na kumsabahi kwa neno SHIKAMOO MZEE JUMAA ! Mtuhumiwa akajibu MARAHABA MHESHIMIWA, Jaji akauliza Unaendeleaje? Mtuhumiwa alijibu anaendelea vizuri na anamshukuru Mungu.
Ndani ya ukumbi wa mahakama watu wanashangaa, wengine wanachekea kimoyomoyo.(Wangeweza kucheka kwa nguvu lakini wanaogopa kufanya contempt of the court –kuidharau mahakama)
Jaji akaendelea kusikiliza shauri hilo.”
Nakuomba msomaji wangu uwe mvumilivu kidogo nikupe mfano wa tatu na mwisho kwa leo.
Mfano AAA;
“Vijana waliyokuwa na umri kati ya miaka 18-25 walishiriki katika tukio la udhalilishaji wa binti -ubakiaji wa kundi na waliofanya tukio hilo walikuwa katika ngoma za usiku ubakaji huo ukafanyika. Baadaye vijana hao wakakamatwa na kufunguliwa shitaka na kila mmoja mbele ya sheria mahakamani.
Katika mwenendo wa shauri lilieleza ushiriki wa kila kijana katika tukio hilo, wapo walikuwepo katika tukio lakini (Ashakumu si Matusi) hawakumuingia binti huyo. Hawa ambao hawakufanya hivyo walijitetea kutokuhusika kwao katika tukio hilo japokuwa waliungama wazi mbele ya mahakama. kuwepo eneo la tukio.
Mahakama ilielezwa kuwa walipiga makofi, walicheka, walishangilia wakati tukio hilo linafanyika.Mahakama iliamua nini?
Bila ya kusita mahakama iliwatia hatiani vijana wote kwa tukio hilo la ubakaji wa binti huyo.”
Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?
Katika mfano hiyo mitatu A, AA na AAA yapo mengi ya kutilia maanani. Mfalme Charle III mwaka 2005 alitambua umri wa Robert Gabriel Mugabe hivyo alipaswa kumuheshimu kwa umri wake tu japokuwa vitendo vya Mugabe vilikuwa mwiba kwa serikali ya Uingereza wakati huo(Rejea MFANO A). Hapo paul Makonda ajitahidi kusikia anayoambiwa na Rose Mary Chatanda, aache kushupaza shingo yake.
Mfano huu unaoana na mfano wa Jaji aliyemsalimu mtuhumiwa mahakamani kwa salaam ya SHIKAMOO, japokuwa hilo ni jambo adimu sana katika mahakama zetu. Hata kama ni mkosaji unapaswa kumpa haki yake, unapaswa kumpa heshima yake, wewe hauna ugomvi naye bali ni majukumu tu ndiyo yanayokukutanisha naye.(Rejea MFANO AA).Usipojenga tabia ya kuwaheshimu watu, watu hao hao watakuvunjia heshima na wewe, hilo Paulo Makonda ajue na hilo ni pande zote mkubwa kwa mdogo na mdogo kwa mkubwa.
Mwisho ni ufahamu wa ofisi ya umma nalo ni jambo la msingi ambayo mtu anaitumikia, kila mhusika ni jambo la msingi kujua hilo maana wenye ofisi sio watumishi hao bali watumisi hao wapo hapo kufanikisha mambo ya wananchi tu(wenye ofisi)
Paulo Makonda anawajibu wa kuwa makini mno kama anataka kubaki katika nafasi hiyo aliyonayo sasa, hivi karibuni ameendelea kuyachanganya madawa, Mkuu wa Mkoa siyo mwajiri wa watumishi mkoani, Mkuu wa Mkoa makini hawezi kumchagua msaidizi wake katika mkutano wa hadhara, anatakiwa kuwa kimya hata kama amevutiwa na Utendaji wa Mtumishi alafu awasiliane na Katibu Tawala wake kwa siri na idara ya Utawala na Rasilimalia Watu ikalifanyia kazi jambo hilo taratibu kuangalia sifa za mtumishi, uzoefu wake na huko anapotoka anakwenda nani?
Mwanakwetu anajiuliza kama Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha kama ametekeleza hilo na mtendaji huyo kama sasa ndiye msaidizi wa Paulo Makonda katika masuala ya Migogoro basi Katibu Tawala huyo ni mtu dhaifu hatufai katika nafasi hiyo.
Kitendo cha kutekeleza hilo ni sawa na kile kitendo cha kupiga makofi, kuchekelea, kushangilia kila anaolifanya Paulo Makonda na hilo halikubaliki na hilo ni sawa na kisa udhalilishajia wa binti kwa wale vijana waliojitetea kuwa wao hawakutenda kosa japokuwa walikuwepo siku ya tukio(Rejea MFANO AAA.)
Wanaomzunguka Makonda Arusha wawe makini tangu Kamati za Ulinzi na Usalama Wilaya hadi Mkoa.
Mwanakwetu Upo?
Kumbuka
“Wanaomzunguka Paul Makonda Arusha Wawe Makini.”
Nakutaka siku njema.
0717649257
Post a Comment