Adeladius Makwega-MWANZA
Juni 19, 2024 Mwanakwetu alikuwa bize sana na majukumu yake maana MCSD ilipata ugeni wa Naibu Katibu Mkuu Dkt. Seleiman Serera hivyo Mwanakwetu hakuweza kuandika wala kutayarisha makala yoyote zaidi ya kuandika habari moja ya aya chache juu ya machache aliyozungumza Dkt Serera hapa Malya.
Mwanakwetu aliporudi kwake majira ya usiku alikuwa amechoka kidogo hivyo alizungumza na mke wake kwa njia ya simu alafu na akazungumza na kijana wake anayefahamika kama Albart Makwega, haya yalikuwa mambo ya kifamilia msomaji wangu-Mambo ya kitaifa yakawa kando kidogo.
Juni 19, 2024 ikaisha kwa Mwanakwetu kuuchapa usingizi. Majira ya saa 9.30(0330) ya Juni 20, 2024 aliamka, kusali kidogo alafu akaingia katika kundi la whasaap la MwAnAkWeTu 1 nakukutana na taarifa ya ratiba ya mazishi ya aliyekuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro, marehemu Tixon Nzunda, ikitaja safari yote ya mwili wa marehemu Nzunda Tangu kuagwa Kilimanjaro Juni 19, 2024 kupitia Dar es Salaam hadi Kata ya Mpemba mkoani Songwe kwa mazishi Juni 22, 2024 Mwanakwetu akiwa anaitazama ratiba hii alikumbuka mambo madogo sana mawili ambayo anatamani na wewe msomaji wake uyafahamu;
Jambo la Awali ni Hili;
“Eneo la Mpemba lipo jirani na kata mbili za Wilaya ya Mbozi-Kata ya Ihanda na Kata ya Ipunga. Momba ni wilaya iliyozaliwa kutoka Mbozi, awali Mpemba ilikuwa wilaya ya Mbozi. Kwa mipaka ya Kanisa Katoliki la Roma inayotambuliwa na Vatikani eneo kubwa la Mpemba na Tunduma yapo Jimbo Katoliki la Sumbawanga, wakati Ihanda na Ipunga zipo jimbo Kuu Katoliki la Mbeya. Awali eneo la Mpemba, Ipunga na Ihanda yalikuwa katika kata moja Kata ya Ihanda huku Kata hii iliwahi kuongozwa na diwani wa CHADEMA ambaye alikuwa Katekista wa Kanisa Katoliki lakini baadaye kakekista huyu alirudi CCM wakati wa kuunga mkono juhudi enzi za utawala wa Rais John Pombe Magufuli.
Eneo la Mpemba sasa ni ukanda mkubwa wa kibiashara,wenye makazi mengi ya watu na magodauni ya kuhifadhia bizaa akutokana na kuwa jirani na mpaka wa Tanzania na Zambia.Unapotaka ardhi ya kilimo inakuwa vigumu hivyo wakaazi wengi wa Mpemba wanalima kata ya Ipunga na Ihanda mazao kama Kahawa , mahindi na maharage . Kata ya Ipunga ambayo ipo ndani kidogo jirani na Kata ya Ihanda.”
Msomaji wangu kumbuka Mwanakwetu ameamka usingizini amesoma ratiba ya mazishi ya Tixon Nzunda kutoka Kilimanjaro–Dar Es Salaam hadi mkoani Songwe na amekumbuka jambo la kwanza juu ya eneo la Mpemba ambao ndipo maziko ya Tixon Nzunda yanafanyika lakini kibindoni
Mwana wa kwetu analo la pili;
“Mwaka 2016 Mwanakwetu akiwa Lushoto walifanya ziara ndefu vijijini, Kwanza walilala Shule ya sekondari Rangwi ambapo waliambiwa kuwa miaka ya zamani Baba wa marehemu Balozi John Kijazi(aliyekuwa katibu Mkuu Kiongozi enzi za Magufuli) aliwahi kuwa Mwalimu Mkuu katika Kijiji hicho cha Rangwi. Siku hii wakiwa ziarani walilala katika mabweni ya Shule ya Sekondari Rangwi na kulipokucha walikwenda Kata ya Viti.
Eneo hili lilikuwa na vijini vyenye wakulima wakubwa wa miti , wakulima wengi wa viazi mviringo na eneo lenye baridi kali. Mandhari yake ilipambwa na kijani na mabiwi makbwa ya vumbi za mbao kutoka viwanda vya kupasua mbao mbao, njiani tukikutana na malori mengi ya yaliyo na shehena kubwa za mbao kuelekea Kenya na mikoa mingine ya Tanzania. Eneo hili lilikuwa na watu wengi wa kabila la Wapare, Wambugu, Wasambaa wachache huku makabila mengine yalijanzwa na watumishi wa umma .
Kijiji cha Viti kilikuwa na Shule ya Msingi Viti na Shule ya Sekondari Viti.Tulipofika Shule ya Msingi Viti Kaimu Afisa Elimu Msingi Mwalimu Mgonja alituongoza hadi shuleni hapo tuliwakuta walimu na wanafunzi wapo mstalini wakiimba Mungu Ibariki Tanzania beti za mwisho… ilipokwishwa tukapokelewa na kuwasalimu wanafunzi na walimu na kufanya nao kikao, wakauliza maswali juu ya haki na stahiki zao yakajibiwa tukawapongeza mno na kuondoka zetu kuelekea shule ya sekondari Viti.Shule ya Sekondari Viti hali ilikuwa mbaya, mazingira machafu , vyoo vimebomoka, mashimo kadhaa ya choo yametitia, vyoo havifanyiwi usafi, huku wanafunzi wakitumia hivyo hivyo, walimu walikuwepo wachache na Mkuu wa shule hakuwepo.
Tukazungumza na wanafunzi na baadaye na walimu huku wakitoa mapendekezo yao.Kweli tumeshindwa hata kuomba miti kwa hawa matajiri wenye msitu alafu tufunike vyoo, vyoo vipo wazi wakifa hawa wanetu tunamlilia nani? Aliyekuwa Kaimu Afisa Elimu Sekondari Mwalimu Yahaya akasema ‘Mkuu wa Shule anashida, kinachotusumbua mteuzi wao ni Katibu Tawala Mkoa kwa mapendekezo ya Afisa Elimu Mkoa, unapowagusa wakuu wa shule sekondari hilo linaleta maneno makubwa.’ Mwanakwetu akasema acheni uwoga mwoondoeni aletwe mtu mwingine, alafu Katibu Tawala aelezwe kwa ushahidi, maana Uongozi Hamira Andazi lisiloumuka linaoneka. Watumishi wanacheka ziara ikaendelea vijiji vingine.
Jioni katika tathimini ya ziara tukaelezwa amepelekwa kukaimu Ukuu wa shule mwalimu kutoka Ngulwi sekondari anayefahamika kama… Mwana Berege.
Mwalimu Yahaya kaimu Afisa elimu Sekondari akasema jambo hili linasumbua sana ukiwagusa wakuu wa shule wanasumbua sana kwa RAS hata huyu aliyekuwepo ana cheo UVCCM. Mwanakwetu akajibu hata kama yupo UVCCM anawajibu wa kufanya kazi maradufu maana wao ndiyo wenye Ilani na pia kama afisa elimu mkoa kama anampenda sana anazo shule nyingi anaweza kumpeleka huko.Tukio hili liliripotiwa na vyombo vya habari huku Mwalimu Mwana Berege aliendelea na kazi vizuri na shule ya sekondari Viti ilibadilika kabisa
Jambo hili alielezwa Katibu Tawala Mkoa wa Tanga wakati huo Injinia Zena Said(Sasa katibu Mkuu Kiongozi Zanzibar) alilielewa vizuri sana naye msaidizi wa Mkuu wa mkoa wa Tanga ndugu Mkapanda na yey aliomba maelezo na kujibiwa.Baada ya mwaka mmoja Kaimu Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Viti Mwalimu Mwana Berege alichaguliwa Kuwa Afisa Elimu Sekondari wilaya moja nchini Tanzania kwa barua iiyosainiwa na Naibu Katibu Mkuu TAMISEMI anayesimamia Elimu wakati huo Tixon Nzunda.”
Mwanakwetu Upo?
Msomaji wangu kumbuka Mwanakwetu anaitazama tu ratiba ya mazishi ya Tixon Nzunda ambaye mwili sasa unalala kaburini ambaye akiwa hai mkono wake ulitenda haki kwa kuwateua walimu wengi kuwa maafisa elimu bila upendeleo. Mwanakwetu hapo hapo alikiicha kitanda chake na kusogelea kompyuta yake na kuanza kuyaandika makala haya.
Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?
Kwa hakika shabaha ya makala haya ni moja tu kumuadhimisha marehemu Tixon Nzunda ambaye alikuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro ambapo ajali imegharimu uhai wake. Mwanakwetu amejaribu tu kuyakumbuka mambo ambayo aliyashuhudia kwa macho yake akiwa kama Mtanzania mwingine katika harakati ya maisha.
Kubwa mwili wa Tixon Nzunda unaolala kaburini katika ardhi ya Mpemba ukiwa na uhai uliweza kutoa vyeo kwa haki ambapo awali nafasi hizo zilidaiwa kutolewa kwa upendeleo na rushwa, kwa hali ilivyo sasa hapo TAMISEMI, Mwanakwetu hafahamu lakini Nzunda ameacha alama ya unyayo uliotenda haki. Je wewe uliopo sasa unatenda haki au dhuluma? Kwa hakika unapokuwa kiongozi pahala popote unatakiwa kufanya kazi kama hamira ili kuumua maandazi yaliyopo kama alivyoweza kufanya Kaimu Mkuu wa Shule ya sekondari Viti wakat huo Mwalimu Mwana Berege ambaye alipandishwa cheo na kuwa Afisa Elimu sekondari na Tixon Nzunda wakati wa uhai wake.
Kumbuka
“Uongozi Hamira Andazi Lisioumuka Linaonekana-Buriani TIXON NZUNDA.”
0717649257
Post a Comment