KIJANA MZURI SHIDA HAJAOKOKA

 



Adeladius Makwega-MWANZA

Siku hii ilianza kama kawaida ya siku zingine, baadaye Mwanakwetu alipokea simu kutoka mkoani Songwe mama mmoja aliyejitambulisha kama kiongozi wa CHAMATA, mama muungwana sana akitaja jina lakini ambalo halikusikika vizuri masikioni mwa Mwanakwetu.

Mama huyu aliuliza maswali mengi kwa Mwanakwetu mojawapo kama ni Mwanachama wa CHAMATA na je anayo nafasi yoyote? Mwanakwetu alijibu hapana.Mama huyu alimualika kuwa mwanachama Mwanakwetu alisema anashukuru lakini ni vigumu kwake kwa sasa kuwa mwanachama wa chama hicho cha kijamii.

Mama huyu aliuliza pia juu ya stori za Mwanakwetu ni za kubuni au za kweli?

Mwanakwetu alijibu kuwa ni makala ya mambo ya kweli kabisa. Mwanakwetu hapa pia  alivutiwa mama huyu maana alikuwa na maswali mengi. Msomaji wangu tambua kuwa simu kama hizo ni nyingi kwa Mwanakwetu lakini zinahiaji uangalifu mno wa majibu maana binadamu siyo wema.

“Kama unahitaji kujua kitu kwa Mwanakwetu jitahidi uwe na mtu anayefahamiana na Mwanakwetu kwa miaka mingi na isipungue 10 nyuma vinginevyo utatwanga maji kwenye kinu.”

Msomaji wangu kumbuka Mwanakwetu anaongea na simu na huyu mama, hapo hapo Mwanakwetu akamuuliza jina lake maana awali hakulisikia vizuri, alijibu anaitwa Monica Chipungahelo. 

Lilipotajwa jina hilo akili ya Mwanakwetu iliyakumbuka majina mawili; Mary Chipungahelo (MARY CHIPS) na Josephine Chipungahelo. Hapo hapo Mwanakwetu akamuuliza huyu dada kama anamfahamu Mary Chipungahelo? Monica Chipungahelo alijibu kuwa huyu ni miongoni mwa shangazi zake.

Mwanakwetu akadakia na kusema,

“Huyu mama alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, ni miongni mwa wanawake wachache makini waliokuwa Wakuu wa Mikoa enzi hizo na nadhani ni miongoni mwa viongozi wachache walioweza kuuongoza vizuri Mkoa wa Dar es Salaam. Mama huyu alikuwa na anapambania heshima ya Serikali za Mitaa mbele ya Mawaziri waliotoka Serikali Kuu. Mathalani mgogoro wake ya marehemu Augustine Mrema akiwa waziri wa Mambo ya Ndani.”

Msomaji wangu kumbuka Mwanakwetu anaongea na Monica Chipungahelo ambaye amempigia simu na mazungumzo haya yanapamba moto baada ya Mwanakwetu kujua kuwa Monica Chipungahelo ana nasaba na MARYCHIPS aliyekuwa Mkuu wa  Mkoa wa Dar es Salaam enzi za Rais Ali Hassan Mwinyi.


 

Mwanakwetu akamuuliz  mama huyu kama anamfahamu Josephine Chipungahelo? Mama huyu alijibu kuwa ni dada yake wanazaliwa tumbo moja lakini sasa amefariki dunia .

Mwanakwetu akajibu kuwa hilo analitambua na chanzo cha kifo chake ni uzazi. Bi Monica Chipungahelo alifurahi zaidi.

“Yule dada yako nilifahamiana naye vzuri sana pale Isimani Sekondari yeye na mimi tukiwa walimu vijana mwaka 2004-2005 yeye na walimu wenzake ndiyo walinippkea.”

Hapo Monica Chupungahelo na Mwanakwetu mazungumzo yametiwa hamira na kuumuka vizuri mithili ya maandazi ya Bakhresa.

“Dada yako alinipiga tukio moja kali tukiwa kazini na akanirushia ndege wangu mchana kweupe.”

Monica Chipungahelo akasema nipe stori kaka yangu ilikuwaje?

“Kwanza huko alipolala kaburini alale pema peponi.Nilifika Isimani Sekondari Disemba 4, 2004 huku shule hii ikipata walimu wapya watatu; Adeladius Makwega (Kiingereza & Kiswahili), Boniface Katura –SIR BONI (Basic Mathematics& Geography) na mwalimu mwingine binti mrembo chotara wa Kihaya&Kinyakyusa (Historia & Jografia).

Huyu mwalimu chotara wa Kihaya & Kinyakyusa alipewa nyumba ambayo ilikuwa kota ya familia mbili yeye na mwalimu Josephine Chipungahelo(Dada Yako).

Mara ya kwanza mwalimu chotara anaripoti kazini aliongozana na mama yake mzazi, wafanyazi shuleni wakawa wanamtania ‘kweli mwalimu unaletwa na mama yako kuanza kazi?’ Huo ukawa utani kila mara, Mwalimu huyu chotara alikuwa mlokole dhehebu moja na Josephine Chipungahelo(Dada Yako).

Kumbuka pia wanakaa kota moja.”

Ofisini Mwanakwetu ninakaa na mwalimu chotara jirani, wakati fulani Mbunge wa Isimani mhe.William Lukuvi ambaye aikuwa mwema sana na mkarimu mno  kwa watumishi wake akatuletea meza na viti vizuri walimu wote, kwa hakika sijawahi kukalia meza na viti vizuri kama hivyo tena, nadhani ulikuwa msaada kutoka Serikali ya Japan.



 

Tukiwa ofisini nilimuuliza mwalimu chotara mama yako alikuleta kweli au wanadanganya?Mwalimu huyu alijbu,

‘Nia ya kuja ni kuyaona mazingira ya kazi ninayokuja kufanyia kazi .”

Msomaji wangu tambua kuwa Mwalimu Josephine Chipungahelo hajaolewa na huku mwalimu chotara hajaolewa wakati huo, hapo Mwanakwetu akawa jirani sana na mwalimu chotara. Mhe Lukuvi akija shuleni anamtania Mwanakwetu.

“Wewe mwalimu wa Kiswahili, wewe mwalimu Swahili sana unajua nimepata tabu kuhakikisha shule hii inapata mwalimu wa Somo la Kiswahili , sasa mwalimu usiondoke, nisaidie kuwasomesha ndugu zangu.

Kama unataka kuoa oa dada zangu nitamwambia Mama Sekadinda akutafutie mchumba mzuri. Au kama hauwataki dada zangu kisa hawajui kupika kwa kutumia nazi oa mwalimu mwenzako huyo jirani (Chotara) Walimu ofisini wanacheka.”

Msomaji wangu Wiliam Lukuvi anapokuwa nje ya Baraza la Mawaziri binafsi huwa sielewi, jamani jamani Lukuvi ni kiongozi wa kweli, tumtumie jamani

Kumbuka Mwanakwetu anaongea katika smu na Monica Chipungahelo.

“Kila Jumapili Josephine Chipungahelo na mwalimu chotara wanakwenda kusali katika kanisa lao, naye Adeladius Makwega& Boniface Katura wanakwenda Parokia ya Isimani kwa Padri Anjelo(Italian Priest) kusali dominika.”

Mwanakwetu kijana akiwa muwindaji akitafuta mwenza maana sasa ana kazi na mshahara wake  ni 108,600/-akiwa Afisa Elimu Msaidizi Daraja Tatu. Hapo hapo akamkazia macho na kumpenda chotara wa Kihaya na Kinyakyusa.

 Mwalimu Chotara akayapokea maombi ya Mwanakwetu kwa mikono miwili akaomba apewe muda huku jambo hilo kila upande uliingize katika maombi. Wakati suala hilo lipo katika maombi akashirikishwa Josephine Chipungahelo (dada yake Monica). Kuwa Mwalimu Makwega ananipenda anataka kunioa je nimkubalie? Mjadala wao ulikuwa mrefu na mwisho wa siku nikajulishwa haya.

“Josephine Chipungahelo kasema maneno haya,

‘Makwega ni kijana mzuri, hana makundi makundi,hana magengemagenge, ni mtu mkweli, hapendi hapa kazini tuonewe na hata mkuu wa shule na Mratibu Elimu Kata wanajua hilo. Hanywi pombe lakini shida ya Makwega ni Mkatoliki, Makwega hajaokoka. Mkatoliki na Mlokole ni vitu viwili tofauti.

Kaa zungumza naye mjue mnafanyaje ? Sisi hatutaki kumpoteza kondoo wetu, hata wazazi wako hawawezi kukubali.Kazi kwako mwenyewe’ kama unaokoka mimi nipo tayari uamuzi wako.”

Msomaji wangu Mwanakwetu akafuatwa na mwalimu chotara na kuelezwa hayo kama yalivyo.Kwa hakika Mkatoliki na Mlokole ni viatu vya kushoto na kulia.Hapa ukabaki urafiki wa kutembeleana, kuchukulia mishahara mwisho wa mwezi na kukopeshana pesa. Baadaye Mwanakwetu alikwenda masomoni na mwalimu chotara alihama akidai kuwa mwalimu Makwega uwepo wake ulisaidia wasionewe.

“Mimi nilioa na huyu mwalimu chotara aliolewa na profesa mmoja, mpaka kesho tunawasiliana si yeye tu bali hata wazazi wake ambao ni wachungaji wa kanisa mojawapo huku wakiniweka katika maombi hatua zozote ninazopitia.”

Kumbuka haya maelezo yote anaambiwa Monica Chipungahelo kwenye simu , huku Monica akisema kweli Mwanakwetu unazo simulizi nyingi.

“Kweli ninazo simulizi nyingi.”

Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?

Shabaha kubwa ya makala haya ni kuonesha kuwa imani ya dini zinaweza kututenganisha. Swali ni je shabaha ya Mwenyeenzi Mungu ni kuwatenganisha wanadamu?

Shabaha ya pili ya makala haya ni hii, katika makala haya kuna maelezo haya,

“…mwalimu chotara alihama akidai kuwa mwalimu Makwega uwepo wake ulisaidia wasionewe…”

Hapa wanafunzi wa Isimani walimkosa Mwalimu wa Jografia na Historia ambapo Wiliam Lukuvi alihangaika kwa Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kumpata mwalimu huyu lakini mtu mmoja hamtendei haki mwalimu huyu alafu anahama, mwingine anaweza hata akaacha kazi kisa ni uzembe wa kiongozi mmoja, hili halikubaliki viongozi wabadilike.

Mwanakwetu upo?

Kumbuka

“Mwanakwetu Kijana Mzuri Shida Hajaokoka.”

Nakutakia siku njema

makwadeladius@gmail.com

0717649257





 

0/Post a Comment/Comments