MWANAMUZIKI ALIYETEMBEA TANZANIA NZIMA

 

Adeladius Makwega-MWANZA

Kati ya mwaka 1974-1980 wazazi wa Mwanakwetu Mwalimu Francis Fidelis Makwega &Mwalimu Doroth Hezron Mlemeta walikuwa waajiliwa Kurugenzi ya Mpwapwa kwa sasa ni Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa.

Walimu hao vijana; Francis akitokea Dar es Salaam naye Doroth akitokea Singida walikutana na kuoana huku wakifanya kazi katika shule kadhaa; Shule ya Msingi Tambi, Shule ya Msingi Berege na Shule ya msingi Sagara.

Wazee hao wakiwa wanasomesha Shule ya Msingi Berege Mwanakwetu anakumbuka haya,

“Eneo la Berege lilikuwa na wafugaji wengi, hata nyumbani kwetu kulikuwa na mbuzi wengi, eneo hili walikuwa wakilima sana mahindi, eneo hili pia lilikuwa na shida sana ya maji safi na salama. Kijiji hiki kilikuwa jirani na Kituo cha Gari Moshi kiitwacho Gulwe ambapo tulikuwa tunalala sana kusubiri treni kuelekea Dar es Salaam kuwasalimu Babu na Bibi. Umbali kutoka Berege hadi Mpwapwa kupitia Gulwe ilikuwa kati ya maili sita hadi kumi. Wazazi wetu walikuwa wakienda kuchukua mishahara yao. Huku wakipata mishara tu tunanunuliwa fulana zenye picha za Amita Bachani na Bruce Lee.”

Siku moja mama wa Mwanakwetu Mwalimu Doroth akawa anaimba wimbo huu,

“Ewee wema wangu,

Sikuoni tokea majuzi

Wema wanitesa kwa mapenzi sipati usingizi

Nihurumie wema.”

Mwanakwetu mdogo akawa anarudia maneno ya wimbo WEMA, mama wa Mwanakwetu akasema maneno.

“Kesho tunakwenda Mpwapwa kuchukua mishahara, tutawanunulia nguo, lakini tutawaacha hotelini, sisi tutakwenda dansini maana Mbaraka Mwinshehe atakuwepo Mpwapwa Ila ukae na mdogo wako Modestus vizuri akiamka unambembeleza.”

Kweli siku iliyofuata tulifika Mpwapwa wazee hawa wakachukua mishahara yao tukaenda hoteli tukasubiriw tusinzie na tulipolala tukafungiwa kwa nje wao wakaenda muziki ,wakarudi alfajiri na Baadaye Kurudi Kijijini Berege.


 

Mwanakwetu amekumbuka tukio hilo baada ya kuona mjadala mrefu juu mwanamuziki Mbaraka Mwinshehe kwenye mitandao ya kijamii ambaye ni marehemu, mwenye nyimbo nyingi za lugha ya Kiswahili zenye maudhui tofauti.Kwa heshima ya wazazi wa Mwanakwetu na kwa heshima ya Mbaraka Mwinshehe 

 


Mwanakwetu anakuomba msomaji wake asafiri nawe katika maisha ya Mwanamuziki huyu hadi kifo chake, akiwa na nyimbo tele huku Mwanakwetu akivutiwa na nyimbo kadhaa hasa hasa hizi; JOGOO LA SHAMBA, POLE DADA, NALILIA RAHA, ZIMAMOTO & MAPENZI YANITESA.

“Mbaraka Mwinshehe Mwaruka alizaliwa Morogoro akiwa mtoto wa pili kati ya watoto 12. Baba yake Mwinshehe Mwaruka alikuwa Mluguru msomi na karani katika mashamba ya katani, na mama yake alikuwa Mngoni. Kati ya hao kumi na wawili, ni yeye na wadogo zake Zanda na Matata ndio walikuwa wanamuziki, Zanda alikuwa mwimbaji, akiimba pia nyimbo za Kizungu katika bendi ya Morogoro Jazz na Matata alikuwa mchezaji ngoma kwenye bendi hiyo hiyo. Kutokana na maelezo ya familia, babu yake Mbaraka alikuwa na asili ya kabila la Wadoe(Wadoezi) wa Bagamoyo na alipelekwa Mzenga (Kisarawe) akawe kiongozi wa huko na wakoloni. Huko akaoa wake tisa na kupata watoto zaidi ya hamsini akiwemo baba yake Mbaraka.

Mbaraka alisoma Shule ya Sekondari Mzumbe mpaka kidato cha tatu na kuacha shule kisa ikiwa ni muziki maana masomo na muziki haviwezi kwenda pamoja.Sheria za shule zilipiga marufuku mwanafunzi yoyote kuonekana katika sehemu za starehe, wewe unapokwenda katika kumbi hizo kuimba, kucheza, kupiga ngoma au kupiga gitaa, walimu wanakuja katika starehe wewe unakuwa sawa na walimu, kuhimili vishindo vya starehe na masomo hauwezi na walimu hawawezi kukuacha salama hicho ndicho kilichotokea kwa Mbaraka Mwinshehe.”

Kanuni za shule hadi kesho ziko hivyo lakini hivi sasa kuna ugoigoi katika kufuatilia kanuni hiyo na ndiyo maana sasa wapo wanamuziki ambao wanasoma huku wakifanya muziki mwisho wa siku hawafanyi vizuri masomoni.

“Mwanamuziki.Mbaraka Mwinshehe alianza kushiriki katika maonesho ya Morogoro Jazz tangu akiwa shule, wakati huo alipenda kupiga sana filimbi katika mtindo wa kwela kutoka Afrika ya Kusini ukiwa na wapulizaji maarufu kama Spokes Mashiyan, na ulipendwa sana na vijana haswa wa shule na makundi mengi ya jiving yalikuweko katika shule za sekondari. Hivyo, alishiriki akiwa mpigaji wa filimbi awali wakati wa wikiendi.”

Simulizi za maisha ya mwanamuziki huyu  zinakwenda mbali kidogo hadi mwaka 1965 wakati wanamuziki wa Morogoro Jazz wakiwa wamepumzika nje ya klabu yao, Mbaraka alipita akiwa na begi kubwa. Walipomuuliza anaenda wapi muda ule ambao anatakiwa kuwa shuleni, aliwaambia kuwa hataki tena shule anaenda Dar es Salaam kutafuta maisha, walimsihi alale pale klabuni kwanza awaze hatima yake. Kesho yake wanamuziki walishangaa kumkuta Mbaraka akifanya mazoezi ya gitaa, kwani walikuwa wakimfahamu kama mpiga filimbi, kwa kuwa walikuwa na shida ya mpiga gitaa la rhythm, walimsihi aache safari ya Dar na abaki kwenye bendi kama mpiga gitaa, akakubali. Wakati huo wapiga tarumbeta, saxaphone na gitaa la solo pekee waliokuwa wanalipwa kwa mwezi, wengine wote walipata posho kidogo kila lilipopigwa dansi.

“Siku moja, walialikwa Dar es Salaam kwa ajili ya mashindano na Kilwa Jazz. Kabla ya kuondoka, Mbaraka aligoma kwenda kwa kuwa alikuwa halipwi, wazee wa bendi wakakubali kumlipa shilingi 120 kwa mwezi, mpiga solo ambaye alikuwa akilipwa shilingi 150 akagoma kwenda Dar kwa kutetea kuwa mpiga rhythm hastahili malipo, hivyo Mbaraka akasema angepiga pia solo, bendi ikaenda Dar ikiwa na mashaka kwani Kilwa Jazz Band wakati huo ilikuwa ni tishio, na wao walikuwa wakienda bila mpiga solo.”

Mbaraka alilipiga vizuri sana solo katika mashindano hayo na bendi ikashinda. Hapo hapo akapandishiwa mshahara hadi shilingi 250 ambazo zilikuwa ni kiwango cha juu sana, na kuanzia hapo mpaka alipoacha bendi na kwenda kuanzisha bendi yake ya Super Volcano, Mbaraka akawa mpiga solo wa Morogoro Jazz Band.


 

Huku magwiji wa ala za muziki wanaamini kuwa,

“Upigaji wake wa gitaa, ni somo zuri sana kwa mpigaji anayetaka kujiendeleza katika upigaji wa gitaa la solo. Katika vipindi vyake vya kuanzia Morogoro Jazz hadi Super Volcano alipitia staili nyingi za muziki na baadhi kama Sululu, Likembe, Masika Zolezole na kadhalika. Tofauti na bendi nyingi ambazo hubadili majina ya mitindo bila kubadili muziki wenyewe, staili za Mbaraka zilionyesha mabadiliko. Nyimbo katika staili ya Likembe zilikuwa tofauti na zile za Masika Zolezole. Kipindi hicho wapenzi wa muziki waliweza kuondoka Dar es Salaam na kwenda Morogoro kufaidi wiki endi aidha wa Cuban Marimba, au Morogoro Jazz.”

Januari 12, 1979 ulimwengu wa muziki Tanzania ulitikisika kwa simanzi baada ya kusikika kifo cha mwanamuziki huyo, mpiga gitaa, muimbaji, mtunzi na kiongozi wa bendi wa miaka mingi na ambaye bendi yake ilikuwa imepiga karibu kila wilaya zote za Tanzania. Taarifa ziliingia jioni ya siku ile kupitia redio ya Tanzania Dar es Salaam kuwa nguli huyu alifia hospitali katika jiji la Mombasa nchini Kenya muda wa saa 1:55 jioni kufuatia ajali ya gari.

“Nilipofika karibu na Kanisa la Kongoya niliona gari aina ya Peugot 404 nyeupe ikitoka upande wa Bush Bar kwa spidi kali, ikaenda na kuligonga lori moja lililokuwa likitokea upande mwingine.”

Haya ni maelezo ya Zebedee Japhet Kinoka maarufu kama Super Zex Mtanzania pekee aliyeshuhudia ajali ya Mbaraka Mwinshehe Januari 12, 1979 akiwa  anatoka maeneo ya Kisauni kumtembelea Mtanzania mwenzake aliyekuwa na hoteli huko, ambaye pia walitoka kijiji Kimoja cha Maramba Muheza mkoani Tanga.


 

Ilikuwa mchana kiasi kama saa 7 hivi.

“Watu tukakimbilia kuangalia ajali na mara nikamtambua Mbaraka na kuwambia watu kuwa huyo ni mwanamuziki Mtanzania anaitwa Mbaraka Mwinshehe. Watu wananishanga. Katika gari lile kulikuweko watu watatu Mbaraka alikuwa amekaa mbele pamoja na dereva na kitu cha nyuma alikuwepo abiria mwingine yeye alifariki palepale. Hapo tunafanyaje? Tukaanza kukata mabati ya 404 iliyoharibika vibaya kwa dafrao ili kuwaondoa walio hai ambao ni Mbaraka na dereva.”

Msimuliaji aliongeza kuwa Mbaraka alikuwa amebanwa miguu yake tukapambana na kuwatoa na kuwakimbizwa hospitali.Dereva wa 404 alifahamika baadaye kama Omari Abdi Mtanzania na mwenyeji wa Moshi Kiimanjaro yeye na Mbaraka walifariki hospitali .

“Mwishoni ndipo tukautoa ule mwili wa abiria aliyefariki kiti cha nyuma.”

Maelezo ya Zebedee Japhet Kinoka yanaendelea,

“Nilikimbilia Kengeleni Bar ambapo Jamhuri Jazz Band (Bendi ya Watanzania) ilikuwa ikipiga muziki nakuwambia kuwa mwenzao kaumia sana, na wao wakatoka mbio, wakiwemo akina Harrisson Siwale. Hadi hospitali ya Makadara. Hapo hapo nikatumwa kuwafuata wanamuziki wa bendi ya Super Volcano ambao wakati huo walikuwa wakipiga Zambia Bar. Kumbuka mwanamuziki maarufu huwa anaingia wa mwisho ukumbini, wanamuziki walipofika hospitali wakaambiwa watoe damu na wakaanza kukwepa kutoa damu kwa visingizio mbalimbali. Muda si mrefu Mbaraka Mwinshehe akafariki dunia.”

Mbaraka alifarik Januari 12,1979 akiwa na umri wa miaka 34 tu. Kwa kuwa mpaka wa Kenya na Tanzania ulikuwa umefungwa wakati huo kutokana na mgogoro kati ya serikali za nchi hizi mbili, mwili wa Mbaraka ulisafirishwa mpaka mpakani na kupokelewa na ndugu marafiki na Maafisa wa Wizara ya Utamaduni wakati huo.

Baadaye kusafirishwa hadi Mzenga Kisarawe na kuzikwa.


 

Mwanakwetu Upo?

Kumbuka

“Mbaraka Mwinshehe ni Mwanamuziki aliyetembelea wilaya zote za Tanzania.”

makwadeladius@ gmail.com

071764957.


 


0/Post a Comment/Comments