PANYA WALIOWASAMBARATISHA WAPANGAJI

 


Adeladius Makwega-MBEYA.

Nilitoka Isimani Tarafani na Kupanda Hiace moja iliyokuwa Ikifahamika kama Mwitula kuelekea Iringa Mjini, kumbuka hiyo ilikuwa 2005 na mwaka huo ulikuwa ni mwaka wa Uchaguzi Mkuu, huku njiani tukikutana na watu wakiwa wamevalia sare za CCM ambapo kwa wakati huo tayari kampeni zilikuwa zimeshaanza.

Safari yetu iliendelea, huku tukivuka kijiji cha Mkungugu, Ndolela mara Igingilanyi na sasa tukawa tunaingia kijiji cha Nduli, hapa gari hili lilienda kwa sekunde kadhaa, upande wa kulia kwangu wa dirisha kwa mbele niliona bendera ya TLP chapa Jogoo inapepea katika nyumba moja barabarani, hii ilikuwa bendera pekee tangu nilipotokea Isimani. Wakati natazama bendera hizo mara tunakasikaa mlio paaaaaaaaaaa…, gari lilienda kwa sekunde 10-15 dereva akasimamisha na abiria tukiombwa kushuka.

 

“Nyielega! zemiyenu umutuka upatiti pachaaa! Mwikie.”

 

Alisema kondakta wa Hiace hii. Nilimuuliza jirani yangu anasema? Jirani yangu kwenye siti akaniambia gari imepata pacha, tushuke, tulishuka harahaharaka, nilikumbuka hapa si ndipo nilipoziona bendera za TLP? Nikaamua kuvuka barabara hii ya Iringa Dodoma nikaongee na wale wenye nyumba yenye bendera za TLP. Nilifika nakuwasalimia watu wakubwa wawili mke na mume, shikamoo! Wakajibu marahaba, nikawaambia naomba kujisaidia, wakaniekeza uani na mimi kwenda huko, nilipomaliza nikarudi.

 Nikaambiwa kijana karibu benchi, nikakaa. Huyu mzee akasema ,

 

“Gari hilo bado hadi watoe tairi mpaka waweke itatumia dakika kama 10.”

Aliongea mama ambaye alikuwa jirani na huyu mzee.

 

 Pumzikaga baba!, gari zenyewe zimechoka hizo na barabara yenyewe vumbi tupu, mwanzo mwisho.”

 

Mzee kando ambaye alikuwa mchangamfu sana, nyumba yake ilizungukwa na mianzi mingi ambayo ilipamba nyumba yake vizuri huku ikionekana kuwa alikuwa akijapatia kipato kwa kuvuna pombe ya ulanzi kwani palikuwa mianzi mingi .

Mzee huyu alimuuliza na wewe nani? Nilimjibu jina langu na mimi ni mwalimu. Nikaulizwa wa wapi? Nikamjibu wa Isimani Sekondari, akaniambia,

 

“Karibu mwalimu. Pale shuleni kwenu kuna mwanangu anasomo kidato cha pili anaitwa Zamoyoni.”

 

Tuliongea vitu vingi huku mzee huyu akiwa mchokozi wa mada. Mimi nikaupata upenyo wa kumuliza juu ya TLP?  Kwanini wewe siyo CCM kama hawa wenzako?Maana kote nitokako ni CCM tu.

 

“Unajua mwalimu sikiliza! CCM wana shinda moja kubwa, wanadhani nchi hii ni mali yao, kumbe nchi hii si maIi yao, bali wao wanapewa dhamana tu kwa kipindi cha miaka mitano mitano.”

Alinijibu mzee huyu kwa ujasiri. 


 

Alisisitia kuwa yeye huwa anagombea kwa nia moja ya kutoa elimu ya uraia kwa jamii si kwa kushinda, akisema kuwa anaamini iko siku elimu hiyo ya uraia itazaa matunda.

Basi dereva wa Hiace hii ya Mwitula alipiga honi pipiiii… akitujulisha kuwa tayari wameshabadilisha tairi, nikamuaga mzee huyu nikamwambia nashukuru kwa kukufahamu.

 

“Mwalimu karibu sana, ukirudi upitia nikupatie ulanzi.”

 

Nikamjibu asante sana.Tuliendelea na safari yetu na barabara ya vumbi, tukafika pahala sasa palikuwa na lami ikianzia hapo hadi Iringa Mjini, tukiwa tumetapakaa vumbi mwii mzima

.Nilipata nyumba ya kuishi maeneo ya Mtwivila-Mwangingo ambapo kulikuwa jirani mno na Makaburi ya Mtwivira/ Kihesa. Eneo hili lilikuwa na mianzi mingi ambapo nilipata nyumba kwa Mzee mmoja maarufu kama George, huyu alikuwa dereva wa mabasi ya King Cross haya yalikuwa yanafanya safari zake Iringa Dodoma kila siku..

Mzee huyu alikuwa muisilamu safi, ambapo kila ibada alikuwa anashiriki. Nilipomzoea nilimuuliza mbona jina lako la Kikristu na ni Muislamu ? Alinijibu tu kuwa alikuwa Mkristo kweli lakini kuna wakati alifanya kazi wa tajiri wake mmoja, alikuwa mtu mwema na mkarimu kwa hiyo alivutiwa na maisha hayo ndiyo maana sasa ni Muisilamu. Mzee huyu alikuwa na watoto wakubwa aliyozaa na mke wake wa kwanza ambaye wakati nafika hapo niliambiwa alifariki kitambo na walikuwa aidha madereva wa mabasi, makondakta au mafundi mabasi ya safari ndefu.


 

Watoto wa mzee George walikuwa Wakristu wakishiriki dominika na hawakugombana hata siku moja nikiwa pale na baba yao. Lakini Mzee George nilimkuta na mke mwingine ambaye nayeye alikuwa ni mkarimu sana, huku akifanya biashara sokoni Iringa Mjini. Alikuwa akiishi na watoto wawili mmoja wa kike na mmoja wakiume ambao walikuwa watoto wa mwisho kwa mkewe wa kwanza wa Mzee George.

Nikiwa naishi hapo huku nikisoma Chuo cha Tumaini Iringa, nilikutana na bendera nyingi za CCM kama kawaida yake, huku pia zikiwamo bendera za TLP na wakati huo huyu Mchungaji Peter Msigwa akigombea ubunge kwa tiketi ya TLP na hata nilipokuwa nikienda chuoni jirani na chuo cha Tumaini Iringa  kulikuwa na bendera moja moja za NCCR na CHADEMA.

Mzee George alifariki na tukamzika vizuri kwa mama yake mzazi huko Makanyagio. Mzee huyu alipofariki ilibainika kuwa aliwaagiza watoto wake wamtunze mama yao hadi tamati ya uhai wake huku akisema kuwa wasimfukuze mama huyu katika nyumba hiyo hasa katika chumba alichokuwa akiishi naye.

Kwa kipindi chote nilichokuwa hapo agizo hilo nilibaini kuwa walilitekeleza. Nyumba hii ilikuwa na pande mbili, kulikuwa na upande wake mwenyewe mwenye nyumba(marehemu mzee George) na upande wapangaji, tulikuwa hatukutani.

Upande wa wapangaji ulikuwa na vyumba nane viwili kwa familia moja. Kulikuwa na familia nne kimoja mimi, kimoja alikuwa kaka mmoja na mkewe wafanyabiashara wazuri sana wa vifaa vya ujenzi, kulikuwa na muuguzi mmoja na kaka mmoja mpishi katika hoteli ya Babanusa Iringa Mjini.

Nilipofika katika nyumba hiyo nilimzoea muuguzi kwa kuwa nilibaini kuwa kaka yake niliwahi kufanya kazi na kaka yake alikuwa mwalimu mwezangu huko kijijini nilipokuwa. Huyu mwaliimu mwenzangu wa Isimani alikuwa na mkewe alikuwa akifika kumsalimia wifi yake.

Ahh mwalimu Makwega unakaa hapa? Nikasema ndiyo, masomo yanaendaje? Nikasema yanaenda vizuri, aliniambia kuwa nimekuja kumsalimia wifi yangu huyu nesi, nikajibu sawa. Kwa mimi binafsi sikuwa na budi nilimzoea huyu nesi akawa kama ndugu yangu.

Nilipoondoka isimani, nilikuwa na kuku kadhaa wa kienyeji, nilipokaa katika nyumba hii kwa muda niliona kuna wafugaji wezangu kwa hiyo nilienda Isimani kuwachukua kuku wangu kama 24 na kumuomba muuguzi huyu ambaye alikuwa na banda kunisaidia kuwachanganya na kuku wake. Nilikaa kwa muda wa mwezi mmoja nikaenda Mbagala karb a uchaguzi mkuu 2005.

Wakati huo Mbagala ilikuwa sehemu ya jimbo la Kigamboni ambapo kwa nafasi ya Ubunge Jimbo la Kigamboni alishinda Mwichumu Abdul-raham Msomi huku ukizijumlisha kura za CUF na CHADEMA wakati huo zilizidi kura za ndugu yangu huyu wa CCM Mheshimiwa Mwinchumu. Huku vyama vya upinzani vikiwa na wagombea lukuki kila mmoja luwake kwa nafasi ya urais, ubunge na udiwani.Baadaye nikarudi chuoni Iringa kuendelea na masomo na ilipofika Disemba nikarudi tena Mbagala kula Krisimasi.

Kabla ya kuondoka kwenda Dar es Salaam nilibaini kuwa nyumba hii ilikuwa na shida moja ya kuwepo kwa panya ambao walikuwa wanaharibu sana vitu. Hapa kila mmoja alikuwa anapambana kivyake, ukiingia chumbani kwako ukimkuta panya unamuua, kama unaweza kuweka mtego, unamtega lakini njia hizo hazikuwa na tija. Mimi niliamua kuchukua chakula kidogo na kutafuta sumu ya panya na kuwatega chumbani kwangu na kuondoka zangu Dar es Salaam.

Siku niliporudi kweli nilikutana na panya wengi wakiwa wamekufa niliwakusanya kutoka kila kona nyanyua viti na vitanda huku nikifanya usafi maana harufu ilikuwa ya kutosha. Niliwakusanya na kuwachimbia shimo na kuwafukia.


 

Sote kwenye nyumba hii kila mmoja anapambana na panya kivyake akifa anamtupa ajuavyo. Sasa hakuna anayetambua kama mwenzake kaweka sumu au katumia mtego wa panya na kwa bahati mbaya panya hawa walikuwa na uwezo wa kuingia kila chumba nyumb ahii haikuwa na dali nyumba hii ilikuwa ya makabwea

Sumu inawezekana nimetenga mimi panya akafia kwa muuguzi au kwa mfanyabiashara. Kumbuka msomaji wangu kuwa mimi nina kuku nimeziweka kwenye banda la muuguzi kuku hawa kule tunapotupa uchafu ndiyo malisho yao.

 Kuna siku tuliamka asubuhi na kukuta kuku 48 wamekufa.Kuku karibu 48 walikuwa wenye thamani ya kama 336,000/ kama wangeuzwa kwa 7000/ walikufa ambapo mshahara wa Afisa Elimu Msaidizi daraja wa tatu Mwanakwetu ulikuwa ni 108,000/.

Sasa muuguzi akawa anasema kuwa hawa kuku itakuwa wametolewa kafara na huyu mfanyabiashara na ndiyo maana duka lake linajaa vifaa si bure, haiwezekani kufa pamoja kuku wote, kwa kuwa ugonjwa ulishapita, na hata kama ugonjwa wangekufa mmoja mmoja. Ugomvi ukawa mkubwa watu hawasalimiani. Kwa kuwa hasara tuliopata ni mimi na muuguzi, mimi nikawa bize na chuo, huku nyumbani narudi usiku, kumbe watu hawana amani. Niliongea na niliyekuwa nimemzoea yaani muuguzi, nikamwambia dada mimi nadhani kuku wetu watakuwa wamekula sumu tu. Mimi nilitenga sumu chumbani kwangu na niliporudi nilifanya usafi.

Muuguzi alisema mwalimu hilo hapana hapa pana mkono wa mtu mbona mimi kila mara natega sumu mbona kuku hawafi? Sikuwa na jibu.Balaa lilizidi na mimi kumaliza Chuo na kurudi Dar es Salaam, huku kila mmoja akiikimbia nyumba hii.


 

Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?

Shabaha kubwa ya makala haya  MwanakwetU leo amekmbuka maiha yake ya  miaka 20 iiyopita hapo Iringa Mjini kubwa katika makala haya namna  panya ambao walikuwa wakiharibu vitu vya thamani ndani ya nyumba hii ya Mzee George. Sasa kitendo hicho  kilisababisha kuku wetu 48 kufa na sie kupata hasara. Huku amani ikitoweka katika nyumba hii. Yote hii ilitokana ni kisa cha kila mmoja kupambana na panya hawa kivyake, huyu kaweka sumu, huyu kaweka mtego huyu kamuua kwa kumbahatisha kimeleta shida na migogoro ndani ya hii nyumba hadi wengine wakiikimbia na kutafuta nyumba zingine kwa kushikana uchawi.Tungefanikiwa kuwamaliza panya wale kama tungekaa pamoja na tungekuwa na shabaha moja kwa hakika panya wale wangekufa lakini walitusambaratisha sisi Wapangaji.

Mwanakwetu Upo?

Kumbuka

“Panya waliowasambaratisha Wapangaji-Jamani Tuwe na Shabaha Moja.”

Nakutakia siku njema.

 

makwadeladius@gmail.com

0717649257


 

 

0/Post a Comment/Comments