HILI NI JUKUMU LA SERIKALI

 



Adeladius  Makwega-MWANZA

Msomaji wangu nakualika tena katika makala ya katuni siku ya leo, kumbuka haya ni makala ya uchambuzi wa katuni mbalimbali kama zilivyokusanywa na Mwanakwetu kutoka vyanzo kadhaa wa kadhaa, kubwa yakizingatiwa maudhui yanayogusa jamii ya wanyonge.

Mwanakwetu anakipinga kipenga chake cha kuyaanza makala haya huku mkono wake wa kuume umeikamata katuni inayoonesha misumari mitatu , miwili iliyopinda na mmoja ukiwa umesima wima vizuri. Kwa hakika misumari miwli imeshindwa kugongelewa vizuri na ni uharibifu wa rasilimali, cha kustajabisha nyundo inaendelea na kazi kwa msumari wa tatu.

Mwanakwetu anajiuliza je msumari wa tatu matokeo yake yatakuwa hasi au chanya?

Kwa jicho la uchambuzi la Mwanakwetu anaamini kuwa unapofanya kazi yoyote ili iweze kufanyika vizuri yapo mambo kadhaa ya kuzingatiwa; ujuzi kwa anayeifanya kazi hiyo, uimara wa vifaa kazi na mazingira ya kazi husika. Hivyo ndiyo ilivyotokokea katika misumari hiyo miwili kwa hiyo sote tunawajibu wa kuyazingatia hayo ili kupata ufanisi wa kazi Mwanakwetu anaamini kama haya matatu yakitiliwa maanani basi msumari wa tatu utakuwa salama.


 

Mwanakwetu anaigubika katuni hiyo ya nyundo na anaigubua katuni ya pili iliyochorwa na Saidi Mikaeli na kupachikwa pia katika kurasa za DW KISWAHILI-hapo kunaonekana vijana mmoja wa kike na mmoja wakiume. wakiwa wamevalia kileoleo. Mvulana anasema yeye huwa anatumia mitandao kucheza kamali naye msichana anajinasibu kuweka taarifa za mahusiano yake. Mbele ya katuni hii kuna maneno yanayowashawishi kuwa simu zitumike kwa akili ili kujipatia fursa za kuongeza kipato.

Nia ya Shirika la Utangazaji wa Ujerumani kuichapisha katuni hii ni kunadi kwa wasikilizaji wake vijana wetu wachangamkie fursa za mitandao na kuachana na matumizi yasiyofaa.

Safari ya kuzisaka katuni inaendelea sasa Mwanakwetu anaichukua katuni ya tatu inayoonesha watu wawili mmoja ni maskini na mwingine ni serikali ambapo wametenganishwa na bango linalochorwa picha ya mtu.

Huyu maskini amevalia misurupwete kama vile anatakiwa kuchezeshwa kindumbwedumbwe. Huyu serikali anaonekana anamchora huyu masikini yapokuwa wajihi unafanana lakini picha inayochorwa inanesha huyu masikini mambo yake safi wakati siyo kweli- sahani halisi ina mifupa lakini sahani inayochorwa imejaa chakula na minofu tele.

Hilo linamstajabisha Mwanakwetu na kujiuliza Baba GOVERNMENT kulikoni? Unatakiwa kumchora masikini namna alivyo.


 

Mwanakwetu anaisogeza katuni ya nne. Katuni hii inaonesha jitu moja kubwa leye magwanda , mabuti  na marungu linaonekana kuzurura katika eneo lenye giza totoro. Mbele ya jamaa huyu kuna jamaa yupo kando ya shimo , jamaa huyu amepewa kibandiko ONLINE na mbele yake kaweka kitita cha fedha ili amkabidhi bwana mkubwa huyu jitu.

Kwa hakika katuni hii inatilia maana namna ONLINE Media zinavyoendeshwa kwa tabu kukiwa na kodi na vibali/leseni lukuki. Kwa hakika gharama hizo mchoraji wa katuni hii  Masod Kipanya anaona zinazinyima raha ONLINE MEDIA na kandamizi. Mchoraji wa katuni hii anatamani mazingira bora ya uendeshaji wake. Mwanakwetu anakumbusha jukumu la serikali siyo kuweka vibali, leseni na sheria na kanuni lukuki tu bali kuboresha mazingira rafiki ya kuifanya kazi hiyo mitandao hii inaweza kufanya kazi bila vibali na serikali inakusanya kodi kupitia vifaa vinavyotumika wakati wa kununuliwa na hata gharama za vocha na umeme.

Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.Ibara ya 18; 1;

 “Bila ya kuathiri sheria za nchi, kila mtu yuko huru kuwa na maoni yoyote na kutoa nje mawazo yake, na kutafuta, kupokea na kutoa habari na dhana zozote kupitia chombo chochote bila ya kujali mipaka ya nchi, na pia ana uhuru wa mawasiliano yake kutoingiliwa kati.”

Nia ya Mwanakwetu siyo kuitilia maana sana hii ibara ya 18; 1 bali inalenga shabaha kwa ibara ya 18, 2 ;

“Kila raia anayo haki ya kupewa taarifa wakati wote kuhusu matukio mbalimbali nchini na duniani kote ambayo ni muhimu kwa maisha na shughuli za wananchi, na pia juu ya masuala muhimu kwa jamii.”

Je Ibara hii ilifutwa katika katiba yetu? Hapa ndiyo kusema unapoona mtu anaendesha mitandao ya kijamii, Blog, runinga, redio magazeti, huyu ndugu katumia muda na pesa yake ya kuwanunuliwa watoto wake ugali akawekeza huko anachokifanya anaisaidia serikali kwa mujibu wa ibara hiyo 18; 2.Huu ni wajibu wa serikali. Mwanakwetu anatumia katuni hii ya Masod Kipanya kukumbusha wajibu wa serikali na kuyaweka mazingira mazuri.

Mwanakwetu upo?

Hadi hapa ndiyo natia nanga katika makala haya katuni siku ya leo. Msomaji wangu katuni zangu nne za leo ni ile ya nyundo na misumari, ile ya vijana na matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii, ya tatu ni namna serikali inavyomtazama masikini na ya mwishoni hii ya Alwatani Masod Kipanya juu ya malipo ya mitandao ya kijamii.

Kumbuka

“Maskini Achorwe Kama Alivyo- Hili ni Jukumu la Serikali.”

Nakutakia siku njema

makwadeladius@gmail.com

0717649257


 

 

0/Post a Comment/Comments