LINA SIWA NA MZANI

 



Adeladius Makwega-MWANZA.

Nakualika tena katika makala ya katuni siku ya leo, kumbuka haya ni makala yanayokusanya katuni mbalimbali kutoka vyanzo kadhaa wa kadhaa zenye maudhui tofauti, kwa kuzitazama, kwa kuzielezea na kwa namna zilivyochora na mwisho kupachika uchambuzi kwa jicho la Mwanakwetu.

Kuyaanza makala haya leo hii, hapa nina katuni moja inayoonesha jamaa mmoja ana mwili mkubwa mithili ya Goliati wa Biblia aliyekuwa akipambana na Daudi. Kando ya kibonzo hiki kina maneno haya. Dubwana lolote kubwa na la kutisha mbele yako si lolote wala chochote, japokuwa wewe ni mdogo, kikubwa ni Mungu wako ndiyo mkuu kuliko vyote.


 

Kwa hakika msomaji wangu katuni hii inajieleza vizuri na kubwa inataja Ukuu wa Mwenyeenzi Mungu. Katika kuitazama hili katuni Mwanakwetu amekumbuka mchango wa Gavana wa Jimbo Siaya nchini Kenya James Orengo akiwa katika Bunge la Seneti Machi 12, 2020 alisema maneno haya.

“Serikali inapokuwa madarakani mnatambua mambo yanavyokuwa, natambua tunaweza kutoa elimu kwa wenzetu wa upande wa pili kidogo, mara nyingi mapinduzi yanaweza kuwameza hata watoto wa wanamapindzi bila woga. Hata kuwameza wanamapinduzi wenyewe. Serikali hii inaweza kuwaadhibu nyinyi sana kuliko itakavyoweza kuniadhibu mimi, nawaambieni ukweli , baada ya mwaka mmoja ujao tu, mtakuja kwangu nikawatete mahakamani.

Natambua, nawaambieni, nilikuwepo hapa wakati wa Rais Kibaki akiwa upinzani, nilimtetea kwa sheria zilizotungwa hapa hapa, nilimtetea Rais Uhuru Kenyatta na Makamu wake Wiliam Ruto wakati KANU Inaanguka, wakati Kibaki anaondoka na wabunge wake na kuunda Baraza la Mawaziri, nilienda mahakamani kwa niaba yao lakini sasa wako madarakani wanasahau. Jamani ukiwa na mamlaka na yakikuingia akilini mwako, nawaambieni hauwezi kukumbuka kwamba siku moja kuna Nguvu kubwa ya kuliko zote ya Mwenyeenzi Mungu ambayo itakabiliana na wewe hapo baadaye.”

Kwa hakika maneno haya ya Gavana Orengo yananipa nafasi ya kuikamata katuni ya pili ambayo inaonesha jamaa mmoja ambaye amevalia sare za Polisi, huku akiwa amemkanyaga kwa viatu jamaa mmoja aliyepewa jina UPINZANI na huku akiwa amembeba jamaa mmoja juu ambaye amepewa jina CCM.


 Seneta wa Saiya James Orengo-KENYA.

Katuni hii kwa hakika inaelezea siasa za Tanzania na inatoa hoja kuwa polisi kama wanakipa nguvu Chama cha Mapinduzi na kuwakandamiza wapinzani. Mwanakwetu atambua kuwa CCM ni chama tawala lakini kwa mujibu wa katuni hii polisi wanawajibu wa kutoa nafasi hata kwa vyama vya upinzani kufanya kazi zao kwa haki, hilo litafanya wananchi kutambua kuwa Watanzania wakimchoma kiongozi yoyote yule na chama chochote kile kwa nafasi yoyote ile wanaweza kufanya mabadiliko haya kwa kutumia uchaguzi kupitia vyama vya siasa vilivyopo na siyo mbinu zingine mbaya zinazoweza kuleta vurugu.

Mwanakwetu anaomba Jeshi la Polisi Tanzania lifanye kazi yake vizuri kwa mujibu wa sheria na bila kumuonea mtu na wala kumpendelea yoyote yule. Hilo litasaidia hata wachoraji wa katuni wakiliona jambo hilo watachora katuni ambapo naye Mwanakwetu atazitumia katika makala haya.


 

Sasa naivuta katuni ya tatu ambao kunaonekana jamaa mmoja anasukuma toroli lake na huku kabeba mche wa mti anakwenda kuupanda,kwa kando kuna lori kubwa la mizigo limebeba magogo kadhaa ya miti ambayo yametoka kuvunwa msituni.

Mwanakwetu anapoitazama katuni hii anaona jambo kubwa la mchoraji wa katuni hii anaonesha thamani ya mti unavyopandwa huwa ni ndogo sana na unabebwa kwenye toroli tu lakini mti ukikuwa unapanda thamani yake na unabebwa na malori.Hapa binadamu anapata samani na pesa tele.

Mwanakwetu anasisitiza kuwa ni vizuri jamii zetu tupanda miti kwa faida ya mbao na ili kupata hewa safi kwa binadamu na viumbe hai vyote


 

Mwanakwetu akiwa katuni hii ya mazingira amekutana na picha moja ya Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa Balozi Hoyce Temu akiwa amemkumbatia Mkurugenzi wa Shirika la Afya Dunia kanda ya Afrika mhe. Dkt Faustine Ndungulile (Mbunge wa Kigamboni) ambaye ameshinda nafasi hiyo hivi karibuni.Mwanakwetu anasema Dkt Ndungulile sasa itabidi utuachie ubunge wetu wa Kigamboni.

Mwanakwetu anapoitazama picha hii japokuwa anaona wivu kwa Dkt Ndungulile kukumbatiwa  na Balozi Temu lakini anajikaza kisaburi na kizalendo akisema hakuna haja ya kumpongeza zaidi Dkt Faustine Ndungulile kwa kushinda nafasi hiyo maana hilo kumbato la Balozi Hoyce Temu linatosha kuwapongeza kwako na Balozi Temu ametuwakilisha sote.

Ndugu yangu Dkt Ndugulile ukiwa Jimboni kwake Kigamboni nitakuja Kisarawe B tutete jambo juu ya WHO.


 

Sasa ninaikamata katuni ya mwisho kabisa ambayo inamuonesha mama mmoja kapiga suti yake maridadi na juu kapachika hijabu inayolingana na rangi ya sketi , pia mama huyu kavaa miwani ya jua. Mama huyu kabeba kikapu ambacho kina ishara ya tatu kopa(LOVE) , mizani na siwa Mama wa Watu anapiga hatua, kando ya mama huyu kuna jamaa wawili nadhani hawa ni mtu na mkewe, mwanaume anasema, Umesema ameleta Suluhu? Mwanamke anajibu Nimesema anaitwa Suluhu.

Mavazi, wajihi, maswali na majibu haya yanaonesha kuwa huyu ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan.Majibu haya ya mwanamke yenyewe yalitakiwa kuwa Ndiyo ameleta Suluhu, kujibu kuwa Nimesema anaitwa Suluhu inaleta maswali mengi. Je kina mama hawamuamini mama mwenzao? Pia kutokana na kapu alilolibeba mama huyu kuna ishara tele zenye hoja nzito

Kwanza kwa nini kapu la mama huyu limebeba ishara ya mahakama yaani ule mizani, alafu ishara ya siwa yaani lile Bunge ? Alafu viwe katika kapu la mama huyu mkononi? Wakati kwa mujibu kwa kanuni za uendeshaji Mama -Serikali, Siwa -Bunge na Mzani- Mahakama zinatakiwa kujitegemea.

Mwanakwetu anabaini mambo kadhaa, ili mwanamke yule kando na mumewe ajibu kuwa Ndiyo ameleta Suluhu yafanyike haya mara moja. Mosi kile kitendo cha Rais Samia Suluhu Hassan kumuongezea muda Jaji Mkuu Profesa Ibrahimu Hamis Juma ambalo lililamikiwa kinaonesha mahakama ipo katika kapu la deshi deshi, hivyo kwa kukwepa hilo mama yetu anawajibu wa kumteua mara moja mtu mwingine kuwa Jaji Mkuu wa Tanzania maana Tanzania ina majaji wengi wanataaluma na wabobezi wa sheria.

Pili changamoto ambayo Bunge la sasa iliipata ni pale mh. Job Ndugai alipoachia ngazi na kupatikana spika mwingine. Mwanakwetu anatambua ugumu wa mh Job Ndugai kurudi katika nafasi hiyo lakini Rais Samia kwa sasa anawajibu mkubwa wa kumteua mh Job Ndugai kuwa Waziri katika Baraza la Mawaziri na bila kusahau kuhakikisha Bunge linawaondoa Bungeni wabunge wale wa CHADEMA waliyofukuzwa uanachama na chama chao haya yafanyike kabla ya 2025.

Kwa kuyafanya mambo hayo itaondoa alama hizo mbili katika kapu la mama na mama atakuwa ameleta Suluhu .


 

Mwanakwetu upo?

Kwa katuni hizo nne, ile ya jitu kubwa, hii ya polisi kukibeba chama tawala, ile ya mche wa mti na magogo na hata hii ya nne ya mama huyu ambaye anaitwa Suluhu, ndiyo namaliza safari yangu ya makala ya katuni siku ya leo.

Kumbuka,

“Deshi… la Mama Lina Siwa na Mzani.”

Nakutakia Siku Njema.

makwadeladius@gmail.com

0717649257




 

0/Post a Comment/Comments