Adeladius Makwega-MWANZA
Msomaji wangu nakualika tena katika makala ya katuni siku ya leo, kumbuka haya ni makala mengine ya uchambuzi kupitia katuni kadhaa ambazo zimekusanywa na Mwanakwetu ndani ya vyanzo kede kede.
Siku leo Mwanakwetu ameshika katuni nne 1, 2, 3, na 4. Leo anapiga mbiu ya mgambo ya kuanza makala haya kwa katuni inamuonesha jamaa mmoja yupo pamoja na mkewe, jamaa amevalia shati jeupe huku akitoka kazini na bahasha mkono, kando yupo mkewe na ametinga gauni nyekundu huyu mama ni shabiki wa Simba. Jamaa kwa moyo wa dhati anamshirikisha mkewe kuwa amefukuzwa kazi. Mama mwenye gauni jekundu alivyo haramia anajibu kuwa sasa huu ndiyo wakati sahihi wa kuachana, mama mwenye gauni nyekundu kapata kibali naye aiyefukuzwa kazi kapatwa na bumbuwazi. Mchoraji wa katuni hii anatilia maanani juu ya maisha ya ndoa na changamoto zake, kikubwa maisha ya ndoa yanawajibu wa kuwa ya shida na raha na pengine kifo ndiyo kiwatenganishe.
Sasa ninaikamata katuni ya pili ambayo inaonesha mandhari ya kijijini huku nyumba za udongo tano zikiambatana na kwa juu ya nyumba hizo kunaonekana nyanya za umeme mkubwa unapita kwa kasi. Katika nyumba kubwa ya udongo kuna maneno haya, mwanagu huku kwetu umeme umepita. Mwanakwetu anapoitazama katuni hii anatambua kuwa wakati katuni hii inachorwa umeme ulikuwa unapita njia tu vijijini vingi vya Tanzania lakini hali hiyo sasa ipo hivi;
“Taarifa za serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Bungeni Dodoma Machi 2024 zinadokeza kuwa hadi kufikia Machi 2024 jumla ya vijiji 11,837 sawa na asilimia 96.37 ya vijiji vyote 12,318 vya Tanzania Bara vilikuwa vimeunganishiwa huduma ya umeme. Aidha taarifa hiyo ilikwenda mbali zaidi kwa kuonesha katika kuimarisha utoaji wa huduma kwa Wananchi vijijini, jumla ya taasisi 63,509 zinazotoa huduma kwa jamii ikiwemo ya elimu, biashara, pampu za maji, vituo vya afya na nyumba za ibada zilikuwa zimeunganishiwa umeme, ikilinganishwa na taasisi 43,925 za Aprili, 2023.”
Hilo halina ubishi serikali ya Rais Samia inapaswa kuipeperusha doti ya khanga ya mama wa watu huyu angani kama ishara ya mafanikio lakini lakini lakini lakini hili litanoga zaidi kama mkatiko wa umeme ukiwa msamiati mfu nchini Tanzania.
Mwanakwetu anakumbuka hili
“Jumamosi ya Agosti 17, 2024 saa 9-11 nilikuwa Shinyanga Mjini umeme ulikatika na kurudi jioni yake uliporudi jirani yangu wa Mwanza akapiga simu, ‘Jirani umeme umerudi hivi sasa lakini naona kwa wenzagu unawake, kwangu hauwaki, vip kwako umeme unawake?” Nilijibu kuwa mimi sipo Mwanza bali nipo Shiyanga Mjini lakini hata hapa ulikatika saa 9 nikashindwa hata kuchapa makala zangu.”
Agosti 27, 2024 umeme ulikatika tena hapa Malya kwa muda mfupi.Kwa hiyo shida ya sasa ya umeme wa Tanzania unakatikakatika. Habari za mkatiko wa umeme siyo jambo zuri ni hatari kwa usalama wa binadamu na mali zao.
Kwa hakika Waziri anayeshugulika umeme wa Tanzania Dkt Dotto Biteko ambaye ndiye Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania , mtaani watu wanasema Dkt Biteko amekuwa mzungumzaji mzuri, mwenye maneno matamu matamu matamu… lakini bado umeme wakatika mchana kweupe.
“Aachane na kuwa infuliancial speaker avalie kibebwe mkatiko wa umeme.”
Mwanakwetu kwa makala haya anamkumbusha Dkt Biteko kuwa yeye yu kando ya mlingoti kuipaisha juu doti ya khanga ya Rais Samia Suluhu Hassan lakini Dkt Biteko unalikwamisha hilo kutokana na huu mkatiko wa umeme, nakuomba lifanyie kazi haraka ili Mwanakwetu akamilishe kazi yake ya kuipaisha juu doti ya Khanga ya Rais Samia.
Sasa ninaikamata katuni yangu ya tatu ambapo kunaonekana jamaa wawili mmoja kasimama na begi mkononi na mwingine kakaa. Huyu aliyekaa kavaa nguo za rangi ya kijani. Kando yao kuna maneno haya Kwa hiyo una uhakika ushindi ni asilimia 100? Jamaa mwenye kijani anajibu Sio vizuri kusema ushindi asilimia 100, wewe sema ushindi wa kishindo. Mchoraji wa katuni hii Masoud Kipanya anaelezea hali ya kuelekea uchaguzi mambo yanavyokuwa mitaani hasa wanasiasa wanavyocheza na maneno.
Sasa naikamata katuni ya nne ambapo anaonekana mama mmoja kavalia hijabu vizuri akizingukwa na watoto wake mkono wa shoto na mkono wa kulia upande mmoja wa mama huyu kuna watoto wenye nguo za kijani wanasema mama hao wengine wafukuze. Mama kakasirika akamcheki huyu mtoto mwenye kijani kwa jicho pembe alafu chupuchupu ampige kibao. Mama huyu alivyokaa na wanawe mithili ya yule ndege Hondohondo mlezi wa wana.
Mwanakwetu anapoitazama katuni hii analinganisha na mahusiano ya Rais Samia na vyama vya upinzani na kubwa ni kuendelea kwa rais wetu kuwa na moyo huu vyama pinzani na chama wote ni Watanzania.Kero kubwa inayolalamikiwa mitaani kwa sasa ni utekaji na watu wasiojulikana tu, mama hilo lifanyie kazi nakuuma sikio.
Mwanakwetu Upo?
Basi msomaji wangu kwa katuni ile ya mwanamke aliyemuacha mumewe kwa kufukuzwa kazi , pia katuni hii ya Hondo Hondo Mlezi wa wana , kwa katuni ile ya ushindi wa kishindo na Katuni ile ya umeme vijiji na mkatiko wako, Ndiyo inakamilisha makala ya katuni siku ya leo.
Kumbuka
“Khanga ya Rais Samia.”
Nakutakia siku Njema.
0717649257
Post a Comment