Adeladius Makkwega-TANGA
Mkuu wa Dayosisi ya Kaskazini Mashariki ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Askofu, Dkt. Msafiri Mbilu amesema kuwa Wakristo wa sasa wasiache kumuabudu, kumsifu na kumshukuru Mwenyeezi Mungu kwa kutumia lugha zao za asili, hilo ni jambo la msingi kama zinazofanya dayosisi za Pare na ile ya Kaskazini.
Haya yamesemwa na Askofu Mbilu wakati wa kuingiza mwili wa Askofu Mstaafu Joseph Mathayo Jali katika Kanisa Kuu Utondoro Lushoto mkoani Tanga Agost 20, 2024 mara baada ya kufariki Agosti 14, 2024 jijini Dar es Salaam.
“Natambua kwa sasa maeneo yetu yana watu mchanganyiko lakini tunazo asili zetu, tusizipoteze, hilo si neno, tujitahidi kuimba nyimbo za kanisa letu kwa Kisambaa na lugha zingine.
Yapo maeneo maeneo mengine katika dayosisi yetu wanafanya hivyo mathalani Ushariki wa Mlalo wanafanya ibada yote kwa Kisambaa.”
Akizungumza kwa mara kwanza katika Kanisa Kuu baada ya kifo cha Baba Askofu Jali, Askofu Dkt Msafiri Mbilu aliupigilia msumari wa matumizi ya lugha za asili kuwa waasisi wake ni akina Askofu Jali ambaye jeneza lake li mbele ya ushariki wa Kanisa Kuu.
Walihakikisha vitabu vingi vinatungwa kwa lugha hizi za asili kwa gharama ya dayosisi na hadi leo hii vinatumia
Jambo hili lilienda sambamba ruhusa ya matumizi ya ala la muziki kanisani maana zamani katika Dayosisi yetu ilikuwa dhambi kucheza gitaa kanisani.
“Nawakumbusha ruhusa hiyo ya wazee wetu, tuitumie kumsifu Mungu na sio kucheza hizo twist kanisani. Tukikiuka hilo tunairudisha wenyewe ile dhambi ya wakati ule.”
Ibada hiyo ilikusanya waombolezaji kadhaa kutoka dayosisi nzima ya Kaskazini Mashariki na waombolezaji kutoka dayosisi zingine za Tanzania na mataifa ya ughaibuni ikiwamo Ujerumani huku ikisisitizwa kuwa ibada hiyo siyo ya kuuaga mwili wa Askofu Jali bali ni semina ya maisha ya Askofu Joseph Mathayo Jali.
Post a Comment