Adeladius Makwega-Utondoro-TANGA.
Maelfu ya waombolezaji Lushoto mkoani Tanga Agosti 21, 2024 wameshiriki mazishi ya aliyekuwa Askofu Mstaafu wa Dayosisi ya Kaskazini Mashariki ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Joseph Mathayo Jali, aliyefariki Agosti 14, 2024 Jijini Dar es Salaam.
Huku mazishi hayo yakiwakutanisha pamoja viongozi kadhaa wa madhehebu ya Kristo ikiwamo Kanisa la Anglikana na Kanisa Katoliki.
Ibada ya mazishi ilianza saa 2.00 asubuhi huku waombolezaji kadhaa hawakujali baridi kali iliyowashambulia miili yao lakini ikipozwa na masweta, makoti na migololi iliyofunika viwiliwili vyao.
Akiongoza ibada hii kwa sauti nzito iliyosindikizwa na maaskofu kadhaa, wachungaji kadha na kwaya kadhaa wa kadhaa kutoka dayosisi mbalimbali. Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Askofu Dkt Alex Malasusa ambaye pia ndiye Mkuu Dayosisi ya Mashariki na Pwani aliwaomba waombolezaji wote watambue;
“Kifo cha Askofu Jali ni mtaji kwa kanisa kutokana na mwenendo wake mwema wa maisha ya Kikristo na msiba huu utumike kuwaunganisha wanasharika mbalimbali katika Dayosisi ya Kaskazini Mashariki na Kanisa zima la Kiinjili la Kilutheri Tanzania ”
Akitoa neno katika msiba huo Askofu wa Dayosisi ya Kigoma Jackson Mushendwa amesema kuwa wasifu wa Askofu Jali unajieleza vizuri kuwa mzee huyu hakuwa mchoyo kwa wanadamu wenzake bila kujali tafauti mbalimbali katika jamii zetu.
“Kwa sasa dunia inapata shida kutokana na uchoyo na ubinafsi, takwimu zinaonesha matajiri ni asilimia 20 na ndiyo wanaomiliki asilimia 80 ya utajiri wa dunia, huku masikini ambao ni asilimia 80 wanapambania asilimia 20 ya rasilimali za dunia. Hapo ndipo shida inaanza. Jamani hapa tujifunze katika maisha ya Askofu Jali, alipewa zawadi yake ya siku yake ya kuzaliwa shilingi milioni na ushehe akaibeba na kuitoa kanisani.”
Kwa upande wake mwakilishi wa serikali Niabu Waziri wa Maliasiri na Utalii Dastan Kitandula na Mbunge wa Mkinga akimwakilisha Waziri Mkuu alisema ,
“Serikali inatambua na kuheshimu mchango wa Askofu Jali katika maendeleo ya mkoa wa Tanga na taifa na tutaendelea kumuenzi kutokana na ushauri wake kadhaa aliyotoa katika mambo mbalimbali.”
Katika mazishi hayo tukio ambalo liliwavutia waombolezaj wengi ni barua iliyoandikwa na Katibu Mkuu Mstaafu wa CCM Mzee Yusufu Rajabu Makamba kwa Askofu Malasusa na nakala yake kumpa Askofu Dkt Msafili Mbilu ikisema
“Askofu Jali alikuwa mtu mwema sana, binafsi na kwa familia yangu tunaendelea kumlilia.”
Barua hiyo ilisomwa huku waombolezaji wakishangilia huo moyo wa Mzee Makamba ambaye ni mgonjwa aliyeamka kitandani kutoka na msiba wa Mzee Jali na kuchukua peni na kumuandikia Askofu Malasusa barua ya Buriani ya Askofu Jali, baadhi ya wambolezaji walisikika wakisema Mzee Makamba amezeeka lakini bado anaijua vizuri ile ile siasa ya Tanzania.
Post a Comment