MAUWAJI YALIYOMPELEKA SADDAM HUSSEIN KITANZINI

 


 Adeladius Makwega-DODOMA

Oktoba 19, 2021 Mwanakwetu aliandika makala yenye anuani darasa la mauwaji ya dujaili kama inavyosomeka katika kichwa hapo juu siku ya leo Mwanakwetu anayarudia tena makala haya kama yalivyo.

Makala yenyewe haya ;

Miongoni mwa tukio la kukumbukwa sana duniani ni yale mauwaji ya mwaka 1982 ya Dujaili yaliyodaiwa kufanywa na Uongozi wa chama Baath cha Iraki wakati wa utawala wa Saddam Hussein, ambapo Uingereza na Marekani walitumia tukio hilo kama kiberiti cha kumtia hatiani Saddam Hussein na wenzake ambapo karibu wote viongozi wa juu wa taifa hilo hawakuweza kukwepa kitanzi cha kamba na kunyongwa. Isipokuwa kwa mtu mmoja tu marehemu Tareq Aziz Issa peke yake.

Ikiaminika kuwa katika tukio hilo la mauaji liliangamiza maisha ya Wakurdi wengi ambao walikuwa ni Waislamu wa madhehebu ya Shia waliokuwa na mahusiano na utawala wa Irani wakati huo ikikadiliwa watu zaidi ya 5000 waliuwawa.

Kijiografia Wilaya ya Dujaili ipo umbali wa zaidi ya maili 35 (53KM) kutokea Baghdad kwa wakati huo ilikuwa inakaliwa na watu zaidi ya 75,000 wengi wao wakiwa Waislamu wa madhehebu ya Shia ikiwa pia ni ngome ya kundi la Daawa.

Walikuwapo wanasimulia kuwa Ilikuwa ni siku ya Julai 8, 1982 ambayo jua kali likiwaka ilikuwa ni miezi michache tangu vita baina ya Irani na Iraki ianze kupiganwa.

Saddam Hussein akiwa na msafara wake huku akiwa na timu ya mawasiliano ya Ikulu ya Iraki ambayo yenyewe ilikuwa na jukumu la kurekodi matukio ya mheshimiwa na kutuma taarifa katika vyombo vya habari, likiwamo Shirika la Utangazaji la Iraki Saddam Hussein Rais wa iraki alipofika hapa Saddam Hussein alipokelewa kwa shangwe kubwa na watu kama ilivyo kwa viongozi wowote wa siasa. Saddam alizungumza kwa furaha katika mji huu huku akiwashukuru wakazi wa Dujaili kwa kuwatoa vijana wao kwenda kushiriki katika vita baina ya Iraki na Irani. Safari ya Saddam Hussein huko Dujaili ilikuwa ni sehemu ya propaganda ya kisiasa ilikuionesha Irani na ulimwengu kuwa hata watu wa Dujaili kutoka madhehebu ya Shia walikuwa wakimuunga mkono Saddam Hussein ambaye alikuwa alikuwa Muisilamu wa dhehebu la Sunni.


 

Saddam Hussein baada ya kuongea na umma huo alitembelea nyumba moja na alipofika huko alikaribishwa bilauri ya maji ambayo aliikataa. Hadi hapo mambo yalionekana kuwa yalikuwa hayajaingia shubiri yakiendelea vizuri na kwa amani tele. Kama ilivyo kwa viongozi wowote duniani alipomaliza ziara hiyo alianza safari ya kurudi Barghdad, ambapo ulikuwa mji wa Sunni wengi na Ikulu ya Iraki. Akiwa njiani kurudi, msafara wake ulivamiwa na kushambuliwa na watu ambao walikuwa wamejificha katika vichaka ambao walikuwa ni wanachama wa kundi la wanamgambo wa Chama cha Daawa ambacho kilikuwa cha Washia wengi ambapo wakati huo lilikuwa kundi la wanamgambo tu ambalo baadaye ikaja kuiongoza Iraki baada ya Saddam Hussein kunyongwa.

Katika shambulio hilo lilileta madhara kwa baadhi ya wasaidizi wa Saddam Hussein kuumia vibaya na wengine kufariki dunia, jambo hili lilimkera mno Saddam Hussein hivyo aliamua kurudi katika eneo la Dujaili kulipiza kisasi

Wakiwa na kikosi cha mawasiliano cha Ikulu ambacho kilikuwa kinaendelea kurekodi tukio hilo kikitimiza wajibu wake ipasavyo ambapo baadaye mkanda huo ulirushwa hewani na Runinga cha Chaneli namba 4 ya Uingereza. Katika mkanda huo anaonekana kijana mmoja aliyekamatwa akisema

 

“Mheshimiwa mimi nimefunga Ramadhani na nilikuwa narudi nyumbani muda huu, sihusiki na tukio hili.”

Mwingine alikuwa akisema kuwa yupo katika kundi fulani la wanamgambo. Saddam Hussein alionekana akitoa maagizo wawekeni kando muwahoji zaidi ndugu hawa.Mara baada ya watu kukusanywa tena alionekana Saddam Hussein akiongea kwa ukali mno

 

“Liwe kundi dogo au kundi kubwa lenye mizinga kadhaa, kamwe sintofumbia macho, nitahakikisha nawasaka na kuwamaliza wote.”

Huku watu waliokusanywa katika tukio hilo wakionesha kutokuhusika katika tukio hilo. Naye Saddam Hussein akisisitiza kuwa atahakiisha anawasaka waahalifu wote ili waweze kujitenga na watu wazuri wa Dujaili.Ikiaminika kuwa baada ya tukio hilo Washia zaidi 148 walioteswa na walifariki wakiwamo wanaume kadhaa.


 

Kesi hiyo ikiwa mahakamani kabla ya Saddam Hussein kunyongwa shahidi mmoja alieleza namna alivyotendewa vibaya katika tukio hilo, huku binti mmoja ambaye wakati wa tukio hilo akidai kuwa alibakwa na wanaume zaidi ya 5

Pia kesi hiyo mahakamani hapa ilicheza santuri iliyokuwa na sauti ya Saddam Hussein akitoa maelekezo kwa viongozi wa mkoa mmoja akisema kuwa wahakikishe wanaharibu makazi na mashamba ya watu hawa wote huku vyeti ya vifo zaidi ya 127 vikithibitishwa vifo vya tukio hilo.Ikiaminika kuwa hata katika barua ambazo alitumiwa Saddam Hussein akiwa Rais wa taifa hilo zaidi ya watu 45 waliokuwa wakituhumiwa na tukio hilo la Dujaili walikufa wakiwa gerezani.

Akiwa mahakamani Saddam Hussein aliungama wazi juu ya kutokea kwa mauwaji ya Dujaili akieleza kuwa yeye kama mkuu wa nchi kitendo cha msafara wake kurushiwa risasi(Kushambuliwa) kilikuwa ni uhaini kwa wale waliofanya hivyo.

Aliongeza kuwa kuwa si sahihi kwa yeye kushitakiwa kwa matendo aliyoyafanya akiwa Rais wa Iraki.

“Mimi ndiye nilifanya tukio hilo sasa kwanini mnawauliza wengine juu ya jambo hili na mimi ndiye nilifanya maamuzi na kusema kuwa watuhumiwa wote wapelekwe katika mahakama ya mapinduzi na hakuna aliyekuwa na uwezo wa kupinga kama mimi niliamua hivyo.”

 

Msomaji wangu kwa kifupi hiki ni kisa cha mauwaji dujaili kilichosabbaisa Saddam Hussein na wenzake kadhaa wanyongwe.


 

Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?

Leo hii msomaji wangu naomba tujifunze mambo mawili tu’

Mosi, baadhi ya watu wanadhani kuwa sheria au katiba inaweza kumzuia mtu asipelekwe mahakamani kama imemtaja kumlinda.Mwanakwetu! Iraki hilo lilishindikana na Saddam Hussein alipelekwa mahakamani, akahukumiwa kunyongwa na baadaye kunyongwa.

Pili, katika tukio hilo kesi ikiwa mahakamani ushahidi uliotumika ni ule ule uliokuwa umekusanywa na wanahabari wa Ikulu ya Bargdad na wasaidizi wa Saddam Hussein mwenyewe kama taarifa za kawaida tu wakiwa kazini mathalani barua kwa rais na nyaraka kiserikali lakini ukatumika kumuangamiza Saddam Hussein, tuwe makini ndiyo maana walatini wanasema Volenti non fit injuria.

Mwanakwetu upo?

Kumbuka,

“Darasa la Mauwaji ya Dujaili ambayo ni mauwaji yaliyompeleka Saddam Hussein kitanzini.”

Msomaji wangu ,hasa wale viongozi wenye mamlaka tilieni maanani sana hii makala-Nawatakia Siku Njema.

 

makwadeladius@gmail.com

0717649257.





 

 

0/Post a Comment/Comments