TUSIWALEE WATOTO KAMA KUKU KIENYEJI- ASKOFU KIANGIO

Adeladius Makwega-MWANZA&TANGA

Mhashamu Baba Askofu Thomas Kiangio wa Jimbo Katoliki la Tanga amekemea tabia ya wazazi kulea watoto kama kuku wa kienyeji, maana hali ya mmomonyoko wa maadili inatisha.

Askofu Kiangio ameyasema hayo kwa ukali na msisitizo mkubwa Agosti 4, 2024 katika Kanisa la Ekaristi Takatifu Parokia ya Lushoto Jimbo Katoliki la Tanga.

“Mtoto anabakwa, mtoto analawitiwa wazazi mnakaa kimya, toeni taarifa kwa vyombo vya ulinzi na usalama mara moja, msijali tukio hilo kafanya nani.”

Mhashamu Baba Askofu Kiangio alikemea maisha ya malezi ya familia nyingi kwa wazazi kutotimiza wajibu wao, hilo ikiwa sawa na mtu aliyegeuza kiatu cha kulia kushoto na kushoto kulia.

“Jamani msiwaache watoto wetu waishi kama kuku wa kienyeji, anatoka asubuhi anazurura popote aendapo na kurudi muda atakao, je mwanao huyu alikuwa wapi na amefanyiwa nini?”

Mhashamu Baba Askofu Kiangio alisitiza haya mbele ya waamini wanaokariba 1000 wa Parokia ya Lushoto ambayo ina mapadri wazalendo wawili na vigango vitatu huku kigango kimoja kinatarajiwa kuwa parokia.


 

Askofu Kiangio akiongoza misa hiyo ambapo nusu ya waamini waliojaza mabenchi ya kanisa hilo wakiwa vijana aliwapa kipaimara.Huku waamini wakishangazwa na moyo unyenyekevu wa Baba Askofu alipoomba msamaha kwa kuchelewa kuanza kwa Ibada ya Misa.

“Jamani mwanzoni ma misa Baba Paroko aliomba msamaha wa kuchelewa kuanza misa hii, shida siyo ya Baba Paroko bali ni mimi Askofu wenu, nilipokuwa nakuja napada milima ya Usambara Fan Belt ilikatika hivyo nikaomba msaada wa parokia mkaja kunichukua nawaombeni msamaha.”

Waamini walitoa pole kwa Mhashamu Baba Askofu Kiangio na huku akipewa zawadi kadhaa ambazo zilijazwa katika makapu tele ya ukindu.


 

Misa hiyo ilipomalizika majira ya saa 8 mchana waamini na waalikwa zaidi 1000 walikula chakula na Baba Askofu Kiangio na hukuhali ya hewa na Mji wa Lushoto na viunga vyake ni baridi kali nyumba wakaazi wa Lushoto zenye dohari wakikoka moto.




 


0/Post a Comment/Comments