BURIANI ALLY MOHAMMED KIBAO

Adeladius Makwega-MWANZA

Septemba 9, 2024 Mwanakwetu aliamka hapa alipo na kubaini eneo lake halikuwa na umeme, hivyo alikwenda kwa jamaa mmoja fundi na alipofika hapo alikaribishwa na mlio wa mashine moja ikiunguruma, aliwasalimu vizuri na baadaye kuuliza mashine hii inaunguruma kwa kutumia nishati gani? Jamaa alijibu kwa wanatumia mafuta ya dizeli. Awali Mwanakwetu alipita kwa kijana mmoja mdogo ambaye anafanya biashara ya duka, apomuuliza juu ya uwepo wa umeme alijibiwa umeme umekatika na hata alipouwauliza ndugu zake wa Tanga majibu yalikuwa haya haya.

Kumbuka Mwanakwetu sasa alikuwa kwa fundi mashine inaunguruma akazungumza naye vizuri huku kelele za mashine hii ikipamba mazungumzo haya chamno ni juu kazi aliyopewa bwana fundi. Hapa simu ya Mwanakwetu haina chaji na Mungu Bahati ndugu mmoja akapiga simu kupita simu ya fundi na kuongea na Mwanakwetu kwa dakika chache, huku hawa jamaa wakawa wanaendelea na kazi yao, mara Mwanakwetu akaaga na kuondoka zake, akiwa anatoka tu watu kadhaa mbele yake mbele umbali kama mita 300 walikuwepo makada wa CCM wanaingia katika nyumba wanatoka, katika na jirani na Mwanakwetu walikuwepo akina mama wawili hawakuwa nadhifu lakini mweenyezi Mungu aliwalijalia kuzungumza maongezi nadhifu huku wakijibizana.

“Umewaona CCM tangu jana wanazunguka majumbani?- Eeeh naona uchaguzi umekaribia. Ndiyo lakini hawapiti nyumba zote-Wanatambua nyumba zingine CHADEMA. Wana nyumba zao, nadhani nyumba zenye wanachama wao tu. Kwa bahati nzuri kwangu wamepita nimewasikiliza vizuri-Lakini mimi sioni haja ya kupiga tena. Kwani nini? Maana unamchagua mtu anashindwa kukusaidia ! Sasa watoto wanapotea na kuuwauwa –Siyo watoto hata watu wazima,kwa mfano jana nimeoa kwenye TV , Baba Mmoja Mwarabu wa CHADEMA ameuwawa, nilijisikia vibaya  mwili wangu ulisisimka, nasikia walimbeba kwa kumteka kutoka katika basi huko Darisalaama, jamaa hao waliofanya hivyo sijui kama watawezi kuwakamata! Hivi hao wauwaji wakija huku kijiji wakaleta haya mambo yao na huu ushamba wetu si watatuuwa sote?”

Haya mazungumzo yao yanaendelea huku bodaboda zinapita na hilo likawa linafanya Mwanakwetu asisikie vizuri mazungumzo yao na safari inaendelea nao CCM wanaingia katika nyumba wanatoka wakiwa na sare zao.


Mara ikaja baiskeli ina dereva wake na imembeba mama abiria wakakutana na hawa akina mama wakawa wanawasalimia kwa Kisukuma, kwa bahati mbaya Kisukuma Mwanakwetu kinampiga chenga , hapo hapo Mwanakwetu akapita zake na kwake , alipofika kwake huku umeme ukiwa umekatika bado na majira ya saa 9.00 alibaini umeme ulikuwa tayari umesharudi na hapa hapa ndipo akaamua kuyaandika makala haya.

Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?

Shabaha ya kwanza ya Mwanakwetu katika makala haya anakipongeza Chama cha Mapinduzi kwa kupita nyumba kwa nyumba kuzungumza na wapenzi na wanachama wake. Hili Mwanakwetu analitumia kuvikumbusha vyama vingine vya siasa Tanzania vifanye hivyo mara moja maana huu ni mwaka wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

Nakuomba msomaji wangu yakumbuke maneno haya;

“Umewaona CCM tangu jana wanazunguka majumbani?- Eeeh naona uchaguzi umekaribia. Ndiyo lakini hawapiti nyumba zote-Wanatambua nyumba zingine CHADEMA. Wana nyumba zao, nadhani nyumba zenye wanachama wao tu. Kwa bahati nzuri kwangu wamepita nimewasikiliza vizuri-Lakini mimi sioni haja ya kupiga tena. Kwani nini? Maana unamchagua mtu anashindwa kukusaidia! Sasa watoto wanapotea na kuuwauwa –Siyo watoto hata watu wazima, kwa mfano jana nimeoa kwenye TV, Baba Mmoja Mwarabu wa CHADEMA ameuwawa, nilijisikia vibaya mwili wangu ulisisimka, nasikia walimbeba kwa kumteka kutoka katika basi huko Darisalaama, jamaa hao waliofanya hivyo sijui kama watawezi kuwakamata! Hivi hao wauwaji wakija huku kijiji wakaleta haya mambo yao na huu ushamba wetu si watatuuwa sote?”

Maelezo haya yananipeleka katika shabaha ya pili ya makala haya kwamba Viongozi wa CCM walioshinda katika nafasi za dola katika kuunda serikali watimize wajibu wao na tena kwa vitendo ili  wawatie moyo makada wa CCM wanaopambania chama hiki mtaani na vijiji jua kali hawana hata chupa ya maji ya kunywa. Jamani haya nimeyaona kwa macho yangu mwenyewe, kila linalofanywa jamii ione inathaminiwa hasa hili la kulinda uhai wa binadamu.


 

Shabaha ya tatu ya makala ni kwamba kama kunafanyika ukamataji wowote katika ardhi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania sasa wananchi hawana imani na wakamataji wowote ambao hawana sare na ni vizuri kila ukamataji iwe lazima Jeshi la Polisi Tanzania wenye sare zaidi ya watatu na wanaotambulika kwa namba zao, majina yao, vyeo vyao na jamii kando ya tukio hilo wawepo katika tukio hilo, hilo litasaidia  kutengaisha pumba na mchele.

Mwisho Mwanakwetu anashauri kama ipo sheria ambayo inaruhusu vyombo vya ulinzi na usalama kutokuwa na sare, sheria hiyo Bunge likae mara moja na iondolewe mara moja na Mwanakwetu anashauri Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lipitishe sheria mpya kwa vyombo vyote vya ulinzi usalama wavae sare na iwe marufuku kutekeleza majukumu yao wakiwa hawana sare na katika ulinzi wa raia na mali zake ndani ya mipaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jeshi la Polisi Tanzania ndiyo libaki na ruhusa ya kubeba silaha kwa usalama wa raia na Jeshi la Wananchi Tanzania wabebe silaha hizo katika oparesheni zao na mipakani na. wakiwa na sare

Mwisho kabisa Mwanakwetu anatoa pole kwa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo –CHADEMA, Waisilamu wote wa Mkoa wa Tanga, Watanzania wenye mapenzi mema na taifa hili na ndugu marehemu Ally Mohammed Kibao aliyeuwawa katika tukio la kusikitisha ambapo kila mstarabu na kila muungwana hawezi kuamini kama limetokea katika ardhi ya Tanzania.

 


Mwanakwetu Upo?

“Buriani Ally Mohammed Kibao.”

Pumzika Kwa Amani.

makwadeladius@gmail.com

0717649257.

 










 

 




0/Post a Comment/Comments