Adeladius Makwega-MWANZA
Msomaji wangu siku ya leo sikupanga kuandika makala haya, lakini ndugu yangu mmoja Roho wa Bwana ikamuongoza, kwanza alinakili kwa kupiga picha ukurasa wangu wa facebook, ukionesha picha ya hukumu ya Mtakatifu Thomas More, alafu ikionesha picha ya yangu, jina langu, idadi ya rafiki zangu 5000 na kuonesha aya ya Bibilia Wokolosai 3, 23-24.
Jamaa akamuomba Mwanakwetu aseme neno juu ya uwepo wa aya hii katika ukurasa wake wa facebook. Hapo hapo Mwanakwetu akacheka sana alafu akamsimulia huyu jamaa kisa hiki.
“Mwaka 2009-2010 na 2011 nikiwa mtumishi wa Shirika a Utangazaji Tanzania, wakubwa walinipa kipindi cha dakika 15 kiitwacho Uhalifu Haulipi, haya yalikuwa makala ambapo kwa juma moja yalichezwa mara mbili; mara ya kwanza kikiwa kipindi kipya na mara pili marudio, pia wapangaji wa vipindi pale TBC Taifa wakati huo walikuwa akina mama wawili Shida Masanmba na Jean Lusaserwa walikuwa na mamlaka na kukipanga zaidi. Kwa hiyo kwa wiki kilikuwa kinaweza kuchezwa hata mara mbili, mara tatu na hadi sita. Kumbuka hii redio inarusha matangazo saa 24 kwa siku moja na kwa juma saa 168 kwa mwezi karibu saa 744 na kwa mwaka saa 8760. Hizo ni saa hewani, hapa inahitaji uwezo mkubwa wa watayarishaji wa vipindi siyo unaingia studioni na kuongea ongea tu.Katika tuzo za MCT kwa mwaka 2011 Uhalifu Haulipi kikashinda na kuwa makala bora ya redio kwa vipindi vya mwaka 2010 katika kategoli ya Utawala Bora.
Kwa hakika ni jambo gumu redio ya umma kushinda tuzo hiyo ya Utawala Bora maana watayashaji wengi wanaogopa kusema kweli wakikwepa mbawa nzao kunyonyolewa na watawala lakini hilo linafanyika vizuri katika vyombo binafsi , kwa hiyo kwa mwaka 2011 kwa vipindi vya 2010 Uhalifu Haulipi kikashinda tuzo ya MCT , mtayarishaji & mtangazaji ni Mwanakwetu, akapata tuzo hiyo, zawadi kadhaa na cheti.Tuzo zilitolewa Mlimani City na sherehe hii ilimalizika usiku manene.Kabla ya kupokea tuzo hii hadi anapokea tuzo hii yaani 2010-2011 Mwanakwetu anayakumbuka matukio makubwa matatu kutoka kwa watu watatu anaowapenda na kuwaheshimu mno waliyokuwap pale Shirika a Utangazaji Tanzania wakati huo.”
Kumbuka msomaji wangu Mwanakwetu anaongea katika simu na huyu ndugu aliyemuulizia juu ya uwepo wa mambo kadhaa ikiwamo ile aya ya Biblia Wakolosai 3, 23-24 katika ukuta wa mtandao ya kijamii wa Adeladius Makwega.
Mwanakwetu alipotoka jengo la Matangazo ya TBC Taifa lililojenga Japani Jengo la Vipindi vya Shule hapa akakutana na gari dogo dereva akiwa Amina Mollel. Huyu huyu Amina Mollel wakati huo ni Mtangazaji na msomaji mzuri wa taarifa ya habari za runinga. Amina Mollel amesoma na Mwanakwetu Chuo Kikuu ile Shahada ya Sanaa ya Habari tangu 2005-2008 na walikuwa wote viongozi wa tawi la CCM Chuo Kikuu.
Amina akamsalimia na Mwanakwetu,
“Kaka Kwema? Wifi yangu hajambo? Leo kakuchagulia suti nzuri, mambo ya visanduku haya, angalia kaka usije ukapata mrembo mwingine hapa redioni, alafu ukamsahau wifi yangu, hilo sitaki. Eeeeh kaka tuache utani vipi 2010 ndiyo hii unagombea Ubunge kura za maoni CCM jimbo gani?”
Mwanakwetu akajibu swali hilo na kuagana na ndugu yake huyu ambaye alikuwa anakwenda ofisi za utawala za shirika hilo la umma. Kwa wale ambao hawamfahamu huyu huyu Amina Mollel alikuja kuwa mbunge katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, baadaye akawa Mjumbe wa Bodi ya Shirika la Utangazaji Tanzania. Amina alipoelekea utawala Mwanakwetu akafanya kazi zake na kurudi kwake.
Siku moja baada ya tuzo kutolewa pale Mlimani City marehemu Sued Mwinyi alikutana na Mwanakwetu na kusalimiana’Ahlan Wa Sahlan.’ Sued Mwinyi ambaye alikuwa anafahamu Lugha kadhaa ikiwamo Kifaransa, Kijerumani na Kiarabu akajibu.’Ahlan Bik.’Bwana mdogo njoo tugawane zawadi za jana.”
Mwanakwetu akaenda akazungumza na kaka yake huyu ambaye alikuwa anamuheshimu sana, alikuwa mtu mwema, mungwana, mkweli na muaminifu kwa Mungu, hapo alikuwa ameegemea gari yake ndogo kama Noah.
“Makwega wewe haujaenda JKT, sisi tulioenda JKT kuna mambo tunayafahamu,lakini wewe umeikosa bahati hiyo sasa lazima tuwafundishe vijana wema kama wewe, hivi nikuulize swali dogo, mfano wewe ni kiongozi, umesimama na kuna mtu anakulinda nyuma yako au katika makazi yako unaamini vipi yule anayekulinda ni mtu salama kwako? Au wewe raia hapo ulipo unaamini vipi kama upo salama hapo ulipo?”
Sued Mwinyi anauliza maswali magumu, Mwanakwetu hana majibu, Sued Mwinyi akasema,
“Bwana Mdogo hauna majibu, ninakwambia, popote ulipo kila mmoja lazima awe mlinzi wa mwenzake, wewe uliye nyuma ya kiongozi yuko mtu anakufuatilia hatua kwa hatua, naye kiongozi anafuatiliwa hatua kwa hatua.Naye kiongozi asijiamini 100 kwa 100. Yule anayemlinda kiongozi asione yeye ni kila kitu anaweza kufanya atakalo, akijua hilo naye kiongozi asiamini hilo na hata wewe raia usiamini hilo upo salama 100 kwa 100.”
Wakati mazungumzo haya yanaendelea akaingia mchungaji & mwalimu John Magafu ambaye alikuwa ndiye mtayarishaji wa vipindi vya redio na runinga vya Christian Council of Tanzania (CCT) wakati huo hapo Shirika la Utangazaji Tanzania, akawasalimia akina Mwanakwetu alafu akaita,
“Makwegaaa…Makwega …….Njoo…. njoooo…
njoo nikupe Injili ya Bwana Yesu.”
Mwanakwetu akaagana na Sued Mwinyi na kumfuata Mchungaji John Magafu, akamsalimia Bwana Yesu Apewe Sifa, hapo hapo Mchungaji Magafu akampa pongezi Mwanakwetu kwa kushinda ile tuzo ya MCT alafu akasema maneno haya,
“Wewe bado kijana mdogo, nakwambia jitahidi sana kufanya kazi kwa bidii, maana unapofanya kazi ni sawa na mtu anayesali kwa Mungu wetu, kazi ni ibada, usione utani. Maisha ya mwanadamu ni ya kazini kwako na nyumbani kwako. Kazi yako unapoifanya tumia nguvu na akili zako zote kuifanikisha vizuri, kazi yako usichukulie kwa mzaha. Watu wanafanya kazi kwa utani wakifikiria wanamfurahisha mwanadamu/mwajiri la hasha. Sifa ya kazi bora si kwa mwajiri bali kwa mwenyeenzi Mungu na ndiyo maana Wakolosai 3,23-24 inasema,’Lo lote mfanyalo, lifanyeni kwa moyo kama watu wanaomtumikia Bwana na siyo wanadamu. Kwa maana mnafahamu kwamba mtapokea urithi wenu kwa Bwana kama tuzo yenu.’ ”
Mwanakwetu hapa akasiikia aya hii kutoka kwa Mchungaji Magafu na kuinukuu katika shajara yake na kuipenda kweli kweli na neno hilo likamuingia vilivyo,hapa hapa akaagana na Mchungaji John Magafu na kurudi zake nyumbani kwao Mbagala Sabasaba.
Kumbuku msomaji wangu Mwanakwetu aaongea na simu na hapo anamjibu huyu ndugu namna aya hii Wakolosai 3, 23-24 anavyoikumbuka vizuri baada ya kuambiwa na huyu huyu mchungaji John Magafu mwaka ule wa 2011. Ndugu huyu alicheka na kuagana na Mwanakwetu katika simu na kujiandaa kuelekea kibaruani kwake na ndipo akaamua kuyaandika makala haya.
Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?
Kwa hakika shabaha ya makala haya ni kwa Dkt Tulia Ackson Dada wa Mwanakwetu ambaye hivi sasa ni Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano Tanzania dada yangu Dkt Tulia unalalamikiwa mno kwanini unakataza wabunge wasijadili juu ya hoja za watu kutekwa na kupotea? Watu wanajiuliza inakuwaje mhe Spika umeamua hilo ? Dkt Tulia, dada yangu Mwanakwetu ninauomba yakumbuke haya maelezo katika makala haya,
“…ninakwambia popote ulipo kila mmoja lazima awe mlinzi wa mwenzake, wewe uliye nyuma ya kiongozi yuko mtu anakufuatilia hatua kwa hatua, naye kiongozi anafuatiliwa hatua kwa hatua.Naye kiongozi asijiamini 100 kwa 100. Yule anayemlinda kiongozi asione yeye ni kila kitu anaweza kufanya atakalo akijua hilo naye kiongozi asiamini hilo na hata wewe raia usiamini hilo upo salama 100 kwa 100.”
Suala la usalama wa raia si la watu wa chini tu ni la kila mmoja mkubwa kwa mdogo, popote ulipo iwe shambani, kazini, nyumbani, bungeni, safarini, ukiwa unatembea kwa miguu, ukiwa ndani ya gari/ndege au meli ukiwa umelala, ukiwa unatibiwa kila moja anahitaji uhakika wa usalama. Dkt Tulia dada yangu kumbuka hata tukiwa kanisani/msikitini sote tunahitaji usalama. Dada yangu kipenzi Dkt Tulia Ackson nakupenda sana na ndiyo maana nakupa hii aya aliyonipa mchungaji John Magafu wakati huo nikiwa kijana pale Radio Tanzania Dar es Saaam kuwa,
“Lo lote mfanyalo, lifanyeni kwa moyo kama watu wanaomtumikia Bwana na siyo wanadamu. Kwa maana mnafahamu kwamba mtapokea urithi wenu kwa Bwana kama tuzo yenu.”
Dkt Tulia suala la watu kutekwa ni suala la usalama wa jamii na lilitakiwa kujadiliwa kwa manufaa yetu sote ule mjadali ulikuwa unawapa jamii uhakika wa usalama wao, au dada yangu Dkt Tulia Hauitaki Tuzo ya Bwana ? Umelidhika na tuzo za Duniani?
Mwanakwetu upo?
Kumbuka,
“HAUITAKI TUZO YA BWANA.”
Nakutakia Siku Njema.
0717649257
Post a Comment